Friday, March 30, 2007

labda ni woga wake tu, lakini huyu muandika blogu ana wasiwasi sana na hizi dawa mpya zinazoingizwa na kutangazwa kwa nguvu zote nchini...!


Miongoni mwa maneno ambayo yalipata kumtatanisha mno huyu mwanablogu mwenzenu
mwanzoni mwanzoni kabisa mwa safari yake ndeefu ya kujua kusoma na kuandika, yalikuwa haya; Human Guinea Pigs.
Alikuwa anatatizika mno kila aliposoma mahali kuwa walikuwepo binadamu ambao walikuwa wamekubali, ama kwa hiyari ama kwa malipo maalumu, kuwa ‘Guinea Pigs’, neno ambalo mpaka hapo huyu muandika katikati ya mistari alikuwa hana tafsiri yoyote anayofahamu zaidi ya ile ya ‘Nguruwe wa Guinea’!

Alitatizika na kujiuliza mno ni kwa vipi binadamu, tena mara nyingi zaidi binadamu mwenyewe mzungu afikie hatua ya kuitwa na kukubali kuitwa Nguruwe, tena Nguruwe mwenyewe kutoka Guinea, nchi iliyo Bara la weusi la Afrika!

Ni baada ya makonzi mengi kichwani kutoka kwa walimu wake ndipo huyu mwanablogu alipofahamu kuwa kilichokuwa kimepewa jina la ‘Human Guinea Pigs’ hakikuwa Nguruwe wa nchi ya Guinea bali kitu kingine tofauti kabisa na alichokuwa akifikiri.

Ndio. Ni baadaye sana huyu Chizi wa mwisho wa mzee Mpilipili alipong’amua kuwa alichokuwa akidhani ni Kiti moto wa nchi ya Guinea ilikuwa ni binadamu waliokubali kutoa miili yao, kwa hiari ama kwa kukatiwa uchache, ili iwe chambo cha majaribio ya aina fulani ya dawa iliyokuwa inafanyiwa utafiti kabla haijapitishwa kwa matumizi ya binadamu.

Akatambua kuwa kumbe badala ya Human Guinea Pigs, kwa hapa nyumbani angeweza hata kutumia maneno ya Mbuzi wa Shughuli na yakakidhi haja, potelea mbali kwamba haya ya kwetu yalikuwa na muelekeo wa masuala ya msosi zaidi kuliko masuala ya kisayansi!

Kuna matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea kwenye nchi njema ya Bongo ambayo yamekuwa yakimfanya muandika blogu aanze kuhisi kuwa yeye na Ndugu zake wabongo wamekuwa wakigeuzwa Human Guinea Pigs ama Mbuzi wa shughuli bila wao wenyewe kujua.

Amekuwa akiangalia, na kushitukia, kasi ya madawa mapya yanayoingizwa kwa ajili ya matumizi ya wabongo na kuona dalili za wazi kabisa za Ndugu zake kugeuzwa Mbuzi wa shughuli.

Mchangiaji huyu wa blogu anakumbuka mno jinsi dawa iliyomtibu malaria tangia anazaliwa hadi uzeeni ya klorokwini ilivyoondolewa wangu wangu kwenye soko kwa maelezo kwamba ilikuwa imeshindwa kazi na badala ya kutibu ilikuwa imejenga urafiki na malaria.

Ikaondolewa hima kwenye soko na kukaingizwa dawa ya Esipi iliyotangazwa kwa mapana marefu kwamba ndio kiboko cha malaria yote. Sijui kama ilikuwa hivyo lakini dhahiri malalamiko ya baadhi ya watumiaji wake yalipunguza sana soko lake. Bado tuna kumbukumbu za baadhi ya Ndugu zetu waliotolewa malengelenge na kubabuliwa na dawa hizo ingawaje mara zote jamaa walikanusha.

Haya, kulikuwepo pia na dawa ya kuulia wadudu Kuanzia chawa, mende, papasi hadi wadudu waharibifu wa mimea, iliyokuwa inaitwa DDT. Ni wale waliokwisha kula kilo kadhaa za chumvi tu ndio watakuwa na kumbukumbu muhimu kuhusiana na dawa hii.

Ndio, ni wale tu ambao utotoni waliruhusu miguu yao kufanya urafiki na funza na kuziruhusu kujenga makazi ndio watakumbuka jinsi wakubwa wetu baada ya kututoa funza hizo na pini walivyochukua dawa ya DDT na kuipaka kwenye mashimo yaliyobaki wazi miguuni baada ya ‘dhahabu’ funza kuchimbwa!

Unaambiwa ukali wa dawa ya DDT kwenye mashimo yaliyobaki wazi miguuni baada ya kuondolewa funza ulitufanya tucheze ngoma za kikwetu pamoja na udogo wetu! Uzuri wake ni kuwa baada ya hapo hata funza zenyewe ziliogopa kusogelea miguu yetu kwa kipindi kirefu tu kilichofuata! DDT ilikuwa DDT kweli!

Miaka michache iliyopita, dawa hii mashuhuri ya wakati wetu ya kuulia wadudu ikapigwa stoop, kwa maelezo kwamba baada ya uchunguzi wa muda mrefu ilikuwa imegundulika kuwa inaharibu ardhi mbali na kuwa ni sumu na kadhalika na kadhalika na kadhalika, ambazo sisi tuliokuwa tukiifahamu hatukuzielewa.

Tukakubali. Tungefanyaje na hali waheshimiwa wameishaamua. Tukasubiri kuletewa dawa mbadala ambayo tungepaka kwenye miguu ya watoto wetu tuliyotoa funza na ambayo ingefanya funza hao kujiuliza mara mbili mbili kabla ya kurudi, hakuna kilichoendelea.

Badala yake, miaka michache tu baadaye, hivi majuzi, tukatangaziwa kuwa baada ya uchunguzi wa muda mrefu na kadhalika na kadhalika nyiingi ambazo hatukuzielewa, dawa ya DDT ingerudishwa tena kwenye soko ili kukabiliana na mbu ingawaje ingekuwa inapuliziwa kwenye kuta tu basi.

Hakuna aliyetuambia ilikuwaje uchunguzi wa muda mrefu wa kwanza ulionyesha kuwa DDT ilikuwa haifai kwa matumizi ya binadamu halafu uchunguzi mwingine wa muda mrefu ubaini sasa kuwa ilikuwa inafaa!

Haya. Katika siku mbili tatu hivi za karibuni mwanablogu anashuhudia kuingizwa sokoni kwa mchanyato wa dawa mpya ya kutibu malaria inayopigiwa chapuo kwa mapana na mareefu kwenye redio na tiivii zetu.

Kabla ya hapo, mchanyato pekee ambao Chesi alikuwa akiufahamu, na kuchangamkia, ni ule uliohusu ndizi zilizochanganywa ama na maharage ama na utumbo, uliokuwa ukipikwa na mama yake na baadaye huyu mwanamke wa maisha yake. Kwamba mchanyato sasa umeingia kwenye dawa amechoka kabisa!

Mchangiaji wa Blogu anazo pia taarifa za watoto wake na wetu wanaosoma shule za shule msingi kuchomwa sindano hii ama kunyweshwa dawa hii ama ile bila yeye angalau kupewa taarifa tu kabla ya jambo hilo kufanyika. Amekuwa pia akijiuliza mno iwapo haya yanafanyika hata kule kwenye shule za ‘Watakatifu’ ama ni huku uswazi kwetu tu.

Ndio, amekuwa akiishia kubaki mdomo wazi kila pale wanawe wanaporudi shule na kumfahamisha kumtaarifu kuwa siku hiyo shuleni wamechomwa sindano ya kinga hii ama ile ama kunyweshwa dawa hii ama ile, taarifa ambazo anadhani alipaswa kupewa kabla jambo hilo kufanyika ili ajiandae kwa Saidi-Efeckti yoyote inayoweza kutokea!

Ni mambo kama haya yanayomfanya muandika katikati ya mistari aanze kujiuliza iwapo, bila kujua na hivyo kuwa na haki ya kudai mgawo, hatujaanza kugeuzwa Nguruwe wa Guinea ama Mbuzi wa Shughuli! Tutafakari.