Friday, August 24, 2007

Kuna maamuzi yanayopitishwa na waheshimiwa ambayo yanakufanya mtu ujiulize iwapo nchi hii ina wenyewe. Kama hili la wafanya biashara 'waaminifu' kuruhusiwa kupitisha mizigo yao bandarini chap chap bila kukaguliwa. Ndio maana nikalikejeli...

'Nyungo' mbili kubwa zilizo kichwani mwa huyu muandika katikati ya mistari ambazo pia hujulikana kama masikio zimedaka taarifa muhimu kuhusu wafanya biashara wa nchi njema ya Bongo ambazo zimemsisimua mno mmiliki wa 'nyungo' hizo.

Hizi ni zile taarifa zilizotangazwa majuzi na waheshimiwa wetu kuwa kuanzia tarehe fulani huko mbele wafanya biashara ‘waaminifu’ wataruhusiwa kupitisha mzigo yao pale bandarini chap chap bila kukaguliwa, wakauze wanachouza kisha baadae wao wenyewe waseme walipitisha nini na wanapaswa kulipa nini!

Yapo mambo ambayo muandika katikati ya mistari husisimka mno anapoyasikia.Hili ni mojawapo. Hii ni pamoja na kujijazia maujiko kila mara kwamba ngozi yake imeshakuwa sugu na politiki za nchi njema ya bongo kiasi kwamba hakuna kinachoweza kumsisimua tena kutoka kwa wanene wa nchi.

Kwamba ati kuanzia tarehe fulani huko mbele ya safari wanaosemekana kuwa wafanya biashara waaminifu wa Bongo wataruhusiwa kupitisha bandarini chap chap lumbesa, magunia, maboksi, matenga na makontena yao bila kuulizwa na mtu kilichomo.

Kwamba baada ya kupitisha mizigo yao bila kulazimika kueleza kilichomo wataenda kuuza kilichomo kisha watarudi kunako husika na kulipa wanachotakiwa kulipa kutokana na walichouza!

Wafanya biashara waaminifu! Kwanza muandika katikati ya mistari anashituka na kushangaa kuwa maneno haya mawili ‘wafanya biashara waaminifu’ bado yapo kwenye msamiati wa lugha yetu njema ya Kiswahili. Wafanya biashara waaminifu! Bongo hii??

Muandika katikati ya mistari anapata tabu mno kuamini kuwa ndani ya Bongo yetu njema hii katika karne hii bado kuna kabila la watu linaloitwa ‘wafanya biashara waaminifu’. Kwa hakika, ni wale wenye roho ya Paka tu, ambao wanaweza kuamini uwepo wa kabila hilo!

Kwamba bado tunao wafanya biashara ambao ni waaminifu vya kutosha kiasi kwamba tunaweza kuwaruhusu kupitisha vijikontena vyao viwili vitatu bila kulazimika kutuambia kilichomo, wakaenda kuuza kisha wakarudi na kutuambia wameuza nini na kulipa wanachopaswa kulipa kama kodi kutokana na mauzo yao!

Kuna mtu mahali anataka kufanya mzaha mbaya. Huu wa kuwaruhusu wafanya biashara wanaosemekana kuwa ni waaminifu kupitisha mizigo bandarini bila kukaguliwa, wakauze kisha ndipo warudi kulipa kodi inayotakiwa ni mzaha mbaya hata kwa nchi iliyobobea katika mizaha kama Bongo!

Muandika katikati ya mistari anajiuliza mno iwapo hapa waheshimiwa walikuwa wanazungumzia Mitume ama Watawa fulani hivi ama tulikuwa tunazungumzia wafanya biashara dizaini ya Rada ama wale wa mashine za umeme za kufua giza badala ya kufua mwanga!

Wafanyabiashara waaminifu? Wepi? Hawa tusioisha kuwasoma kwenye magazeti wakikopeshana na kuchezea akiba ya uzeeni ya Chesi kwa kununua, kukarabati na kisha kuyapiga bei mbaya magofu kadha wa kadha huku Chesi mwenye akiba yake akikosa hata haki tu ya kukopa akiba yake mwenyewe!

Ndio, wafanya biashara waaminifu wepi? Hawa hawa wanaopita mlango wa nyuma kupewa mikopo inayogeuka makopo ya chooni baada ya siagi iliyokuwemo kuliwa?

Kwa hakika, muandika katikati ya mistari anasubiri kwa hamu mno kutangazwa kwa vigezo vya mfanyabiashara muaminifu ili na yeye atie timu na kuuagiza kijikontena chake chenye vijenereta alfu mbili ambavyo kutokana na sifa ya uaminifu, vitapita pale bandarini chap chap bila kukaguliwa!

Ni utume na utawa, ambao hana, ama uwendawazimu tu utakaomfanya Chesi arudi kunakohusika baada ya mauzo yake na kwa akili zake timamu kabisa aseme kweli kwamba kijikontena chake kilikuwa na vijenereta alfu mbili na kodi yake hii hapa!

Bongo haiishiwi na mapya yanayokufanya ujiulize mara mbili mbili juu ya utashi wa baadhi ya watu. Hili ni mojawapo. Tutafakari.



Hakuna kitu kinachowaumiza wazazi kama wakati wa wanafunzi kurudi shule baada ya likizo unapowadia. Ni kasheshe tupu. Nikaona niliandikie hili....

Binti wa mama yangu mdogo amefaulu kwenda shule ya sekondari kubwa lakini ameniacha nikijiuliza iwapo kweli anakwenda shule ama kambi ya skauti.

Nimeangalia barua yake ya maelezo ya kujiunga na shule husika na vifaa na michango anayotakiwa kuwa nayo na kubaini kuwa kama sio kujiunga na kambi ya skauti basi bila shaka itakuwa ni kuhudhuria kikao cha harusi lakini kamwe sio shule.

Nasema huenda binti ya mama yangu mdomo anakwenda kambi ya skauti kutokana na ukweli kwamba baadhi ya vifaa anavyotakiwa kuwa navyo wakati anajiunga na shule husika havihusiani kabisa na kwa namna yoyote na masomo tunayofahamu ya sekondari.

Nasema pia kuwa huenda binti yetu huyu anakwenda kuhudhuria kikao cha michango ya harusi kwa vile baadhi ya michango kwenye orodha ndeefu ya michango anayotakiwa kuwasilisha shule haihusiani kwa namna yoyote ile na masomo ya kawaida ya sekondari tunayofahamu sisi.

Naangalia kivuli cha barua ya kujiunga na shule husika nilichotumiwa na mama yangu mdogo akiniomba kuangalia ni kipi ninachoweza kuchangia miongoni mwa orodha ndeefu ya vifaa na michango anayotakiwa kuwa nayo binti yetu kabla hajaruhusiwa kukalia dawati la shule.

Bila mzaha, nimemuandikia barua mama yangu mdogo na kumjibu kuwa katika yoote hayo mimi nitachangia kukodisha Fuso pale Jangwani kwa ajili ya kusafirisha binti yetu na rundo lake la vifaa na michango anavyotakiwa kuwasili navyo shule!

Ndio, barua ya kujiunga na shule husika inamtaka binti yetu aende shule na godoro, aende na mto wa kulalia, aende na chandarua, aende na ndoo ya plastiki, aende na sahani na kikombe na kijiko, aende na jembe na aende na kiila kitu ambacho muandika katikati ya mistari anajilazimisha kuamini kuwa kwa namna moja ama nyingine kinahusika na kusoma!

Naam, ndoo, sahani, kijiko na kikombe! Kwa hakika nikashangaa sana kwamba orodha ile haikumalizia kabisa kwa kumtaka aende pia na mwiko na jiko la mchina tukajua moja kuwa alikuwa anakwenda kuanza maisha mapya ya ajira na sio kwenda shule!

Yakafuata yanayohusiana na kusoma. Akatakiwa aende na rundo la madaftari, sare za shule rundo, sare za michezo rundo, viatu na soksi vya masomo na michezo rundo na kadhalika na kadhalika ambavyo ukijumlisha na vile vingine ilikuwa dhahiri kuwa ninalazimika kumkodishia binti yetu usafiri wa Fuso kumbeba yeye na vifaa vyake rundo!

Kukafuata orodha ya michango. Nikadhani kwamba ile ilikuwa ni taarifa ya kamati fulani ya michango ya harusi na kamwe sio barua ya mwanafunzi ya kujiunga na masomo ya shule za sekondari!

Kukawa na mchango wa dawati, mchango wa choo cha shule, mchango wa beji mbili za shule, mchango wa mtambo maalumu wa shule wa kuzuia vibaka, yaani mlinzi, mchango wa matibabu na kadhalika na kadhalika.

Na katika kudhihirisha kuwa kiendacho kwa Mganga hakirudi, barua imefafanua wazi kabisa kuwa hela inayotolewa kama mchango wa matibabu haitarudi hata kama binti yetu atadunda mwaka mzima shuleni hapo bila kuuugua!

Kwa hakika, ilikuwa ni orodha ndeefu ya michango kiasi kwamba nikashangaa ilipofika mwisho bila kuona mchango wa MC, mchango usafiri wa Bwana na Bibi Harusi, mchango wa matarumbeta na mchango unaoendana na chochote kinachohusu sherehe za harusi!

Ndio, ilikuwa ni orodha ndeefu ya michango iliyonifanya nikumbuke mno wakati ulee tulipotakiwa kuchangia timu yetu ya taifa ya vijana na kila mtu kutoa chochote alicho nacho kuanzia Ndoo mbili za suruali, boksi mbili za vitumbua hadi debe mbili za mashuka katika kuitikia wito wa “jamani, isaidieni Serengeti Boys!”

Naam, ilikuwa orodha ndeefu ya michango iliyonifanya nijiulize iwapo binti yetu alikuwa anakwenda shule ama kwenye kikao cha harusi!

Ndio, ilikuwa pia ni orodha ndeefu ya vitu iliyonifanya nijiulize mno ziko wapi zile siku kama za mwaka ulee wa 1974 nilipotoka pale shule ya Msingi Mfaranyaki Songea na kwenda fomu wani kule Musoma Alliance ambacho nilichotakiwa kubeba kilikuwa ni sare za shule tu nilizofungia ndani ya msanduku wangu wa mbao uliokuwa na ziinga la kufuli!

Ndio, kwa hakika nimekuwa nikijiuliza mno juu ya mwanafunzi wa kidato cha tano anayetakiwa kwenda shule na ndoo ya plastiki ambayo ni salamu tosha kwake kuwa kama kwao alikuwa amezoea kuoga maji ya bomba la mvua, basi sasa atatakiwa agawe muda wake katika kusoma na kusaka maji!

Katika yote haya, nimemuandikia mama mdogo barua kuwa ninachoweza kuchangia kwenye hili ni kukodisha Fuso pale Jangwani kwa ajili ya kumsafirisha binti yetu na rundo lake la vifaa anavyotakiwa kuripoti navyo shule!
Sasa tunatafuna nyama kama vile hakuna kesho. lakini siku chache za nyuma, gonjwa baya la Rift Valley Fever, RVF, lilifanya watafuna nyama wote waone nyama kama kituo cha Polisi. katikati ya dhahama hiyo niliandika makala hii...

Muandika katikati ya mistari anakatiza mitaani na kuangalia nyama ya ng’ombe inavyoshangaa shangaa kwenye mabucha kama vile haina mwenyewe na anaishia kujiuliza iwapo ni majuzi tu mambo yote yalipokuwa yeye na nyama, nyama na yeye.

Anaangalia jinsi minofu ya nyama ilivyobakia kuwa maeneo ya kujidai ya nzi badala ya kuwa maeneo ya kujidai ya meno yake na anaishia kujiuliza ni lini kiama hiki cha kuona nyama kama kituo cha Polisi kitakapoishia.

Waama, muandika katikati ya mistari anajiuliza mno juu ya watu hawa waliokuwa mabingwa mno wa kumtangazia na kumtaka kuiona nyama kama kibaka akionavyo kituo cha Polisi ghafla bin vuu kugeuka mabubu linapokuja suala la kumruhusu kukandamiza manyama kwa kwenda mbele.

Kwa hakika, huyu wenu mpendwa haoni aibu kukiri kwamba kama walivyo wanaume wengi wa kibongo linapokuja suala la kula nyama, yeye ni mroho plus.Ndio, kwamba linapokuja suala la supu, mishikaki, utumbo na vitengo vingine vyote vya nyama, yeye ni Simba wa Tsavo.

Ndio, kama ilivyo kwa wanaume wengi wa kibongo, yeye alikuwa ni adui nambari wani wa Ng’ombe na Mbuzi, akiteketeza bila huruma kilo juu ya kilo za nyama za wanyama hao saa ishirini na nne na siku saba za wiki.

Unaambiwa ratiba ilikuwa asubuhi kabla ya kuingia mzigoni ni supu ya ng’ombe ama Mbuzi pale mitaa ya Kisutu, mchana anafakamia wali nyama kwa mama lishe, jioni anaungana na kampani na kwenda kurarua nyama za kuchomwa na mishikaki kabla ya kumalizia nyumbani usiku wali na nyama. Naam, nyama kwa kwenda mbele!

Wakazuka hawa jamaa ambao muandika katikati ya mistari anahisi kwamba walimuona anafaidi sana na hivyo kumfanyia fitna kwa kutangaza kuwa kile alichokuwa akipenda sana kilikuwa kimeingiwa na homa ya bonde la Ufa na sasa kimekuwa tiketi tosha ya kukupeleka maeneo ya juu kwa Muumba wako.

Hakuna apendaye ku-rest in peace bila sababu za msingi. Ghafla bin vuu nyama ikageuka kuwa kituo cha Polisi mdomoni mwa muandika katikati ya mistari na Simba wa Tsavo wenzake!

Badala ya kula nyama ya Ng’ombe muandika katikati ya mistari sasa akajikuta akilazimika kula kilichokuwa chakula cha Ng’ombe, yaani majani. Kuanzia mchicha hadi kabichi hadi kisamvu hadi nyasi nyinginezo! Supu yake sasa ikawa ile ya karoti tupu!

Hapo nyuma kidogo huyu muandika katikati ya mistari alikuwa na kawaida ya kuwashangaa kwa kebehi wala mboga mboga bila nyama waliokuwa wamejipa jina la ‘vejetarian’. Akajikuta yeye sasa akigeuka kuwa vejetarian wa nguvu kuliko hata vejetarian wenyewe orijino!

Naam, kwa siku kadhaa kukawepo na taarifa za kuwataka wakazi wa jiji jema la Dizim kukaa chonjo kwa sababu homa ya ng’ombe ilikuwa hapo Boma la Ng’ombe tu, mara ikawa Dodoma, mara Morogoro, na mara Kibaha.

Kwa hakika, kuna wakati huyu Chesi alikuwa anaona kabisa kuwa magazeti yalikuwa kwenye ushindani usio rasmi wa gazeti lipi litakuwa la kwanza kuandika juu ya ugonjwa huo kuingia jijini!
RVF ikawa kushoto, kulia na katikati.
Muandika katikati ya mistari haoni aibu kukiri kwamba alikuwa akisononeka mno kuona minofu ya nyama ikizagaa zagaa tu kwenye bucha huku wanaozifaidi wakiwa mainzi tu!

Siku kadhaa baadaye muandika katikati ya mistari na waroho wa nyama wenzake anashuhudia kupungua kwa kiasi kikubwa kwa taarifa muhimu juu ya RVF. Anashangaa kuona hata ule ushindani wa vyombo vya habari wa kuandika juu ya ugonjwa huo unavyosogelea jijini ukiwa umepungua mno, kama sio kwisha kabisa.

Pamoja na upungufu huu wa taarifa za ugonjwa huo, bado muandika katikati ya mistari hajapata ujasiri wa kusimama mbele ya Bucha na kumtaka muuza nyama akamtie kiuno na kukichukua kiuno hicho hadi nyumbani kwa ajili ya kitoweo.

Naam, ameishia kuwaonea donge majasiri wanaomhadithia kuwa jana walinunua nyama na kuigagadua tani yao bila kujali cha RVF wala nini! na donge linazidi zaidi pale anapoona wagagaduaji hao wakiendelea kudunda bila hata hata dalili ya kuugua angalau kamalaria ama kamafua tu! laiti na yeye angekuwa na ujasiri huu!

Anashindwa kujidai na hilo kwa sababu hakuna mhusika yoyote miongoni mwa wale waliojitokeza kwa nguvu zao zote kumchimbia mkwara kuhusu RVF ambaye ameishajitokeza hadi sasa kutamka kuwa tishio limeishapungua hivyo mwenye kutaka kula nyama,aale. Anayetaka kula utumbo, aale. Anayetaka kukatiwa kiuno, na akatiwee!

Ndio, ni kwa vile hakuna mhusika yeyote ambaye ameishatoa tamko rasmi kuwa tishio la VRF limepungua hivyo Chesi na Simba wa Tsavo wenzake ruxa kuanza kurarua nyama, ni wazi kuwa nyama zitaendelea kuning’inia kwenye mabucha kama nguo kwa dobi panoja na bei yake kupungua kuwa kwa asilimia inayosogelea mia sasa!

Waama, mpaka atakapojitokeza mhusika yoyote kumtoa wasiwasi kwa herufi kubwa kabisa, chesi ataendelea kukodolea tu macho minofu ya nyama inayoshangaa shangaa kwenye bucha huku akiendelea kuchurizikwa na mate ya umero. Alamsik.




Kuna hii fasheni mpya ambayo imeshika kasi kama moto wa nyika ya kufanyia vikao vya maandalizi ya mazishi ya mtu kwenye Bar. Nimeliandikia hili.

Kwanza, huyu wenu mpendwa alidhani hakusikia vizuri tangazo lile. Akatenga vizuri sikio lake kuukuu lililokwisha ona, kama sio kusikia, siku njema na kusikiliza tena kwa makini.

Na si kwamba alichokuwa anataka kusikia kwa ukamilifu kilikuwa ni jina la marhum, la hasha. Hilo alikuwa amelisikia vizuri na kutambua kuwa alikuwa ni mtu ambaye japo hakuwa ndugu yake, alikuwa akimfahamu vizuri. Kulikuwa na kingine kilichomvuta kusikiliza tena tangazo lile.

Na bila khiyana mtoa matangazo akarudia tena. Kwamba alikuwa anasikitika kutangaza kifo cha fulani bin fulani kilichotokea hukoo katika hospitali ya nanihii, habari ziwafikie huyu, huyo na yule wa nanihii na nanihii na mipango ya mazishi ilikuwa inafanywa kwenye baa ya nanihino!

Mipango ya mazishi inafanywa kwenye baa ya nanihii! Hiki ndicho mchangiaji wa Blogu alichodhani kuwa alikuwa hajasikia vizuri. Akawa amedhibitishiwa kwamba alichokuwa amesikia ni kweli na kwamba antena zake, kwa maana ya masikio, hazikuwa kuu kuu kiasi hicho!
Kwamba marehemu fulani bin fulani alikuwa amefariki dunia na ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanakutana kwenye Grosari fulani ili kupanga mipango ya kusafirisha mwili wake kwenda kuzikwa alikozaliwa. Mipango ya mazishi Bar!


Muandika katikati ya mistari na my wife wake wakakumbuka kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa watu wachache hasa ambao ni wacha mungu kwa maana halisi tofauti na akina Chesi ambao ucha Mungu wao unaonekana zaidi siku za jumamosi kwenye harusi badala ya jumapili kwenye misa!

Haya, wakanyanyuana na kuelekea huko kwenye msiba njiani wakiulizana ni masahibu gani yaliyokuwa yameikumba nyumba ya marehemu hadi ikaamuliwe mipango ya mazishi yake ikafanyiwe kwenye baa.

Ndio, wakajiuliza maswali kibao yasiyokuwa na majibu huku kubwa kuliko yote likiwa lile la jinsi marehemu alivyokuwa mcha Mungu na jinsi atakavyokuwa anjisikia huko aliko akiangalia mipango ya kuuzika ya mwili wake ikifanyika Bar!

Tukafika pale nyumbani kwa marehemu ambapo palikuwa na liuwanja likubwa tu la kumwaga na kwa maana hiyo kuondoa dhana kwamba labda watu walikuwa wameamua kwenda kufanyia mipango ya kuusafirisha mwili wake Bar kutokana na kukosa nafasi kwenye makazi yake.

Muandika katikati ya mistari akambwaga mkuu mwenzie pale na kuelekea kule alikoambiwa ndiko mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu na mazishi yake ilikuwa inafanyika. Nanihino Bar.
Akafika pale na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wake kwa waume wakipanga na kupangua kipi kifanyike na kipi kisifanyike kuhusiana na msiba wa ndugu yetu huku mezani kukiwa kumesheheni vituliza majonzi’ kibao.


Kwa hakika, mtu yoyote ambaye angefika pale na kuona kilichokuwa kikiendelea, asingelaumiwa iwapo angedhani kuwa kilichokuwa kikiendelea pale ni kikao cha maandalizi ya harusi! Dhahiri angeshituka mno kuambiwa kuwa kile kilikuwa ni kikao cha maandalizi ya mazishi ya mtu!

Muandika katikati ya mistari anaomba kukiri wazi kuwa alijiunga kukaa kwenye kikao kile kwa machale huku kila mara akigeuka huku na kule akitegemea saa yoyote marehemu mcha Mungu kuwazukia pale na kuwauliza kwa kulikoni walikuwa wanafanyia Bar mipango ya kuzika mwili wake!

Ndio, kwa nini walikuwa wanafanya mipango ya kusafirisha na kuzika mwili wake kwenye eneo ambalo meza ya pembeni kulikuwa na kikao cha maandalizi ya harusi, kandokando yake kulikuwa na kikao cha maandalizi Send-off ya mtu na pembeni kulikuwa pia na kikao cha usuluhishi wa ndoa ya mtu iliyokuwa juu ya mawe!

Muandika katikati ya mistari ameishakiri mara kadhaa huko nyuma kuwa huwa huwa anafanya jitihada za za ziada kuhakikisha kuwa haachwi nyuma na anakwenda sambamba na wakati lakini karibuni mara zote amekuwa akijikuta akiachwa kwenye mataa!

Ndio, aliachwa akishangaa watu walipoanza kuvaa sare za misiba, watu walipoanza kubeba makamera ya video makaburini, watu walipoanza kuwavalisha suti marehemu wakati hawakupata kuwanunulia suti walipokuwa hai na wafiwa walipoanza kwenda saluni kabla ya shughuli ya kuaga miili ya marehemu wao.

Kwa hakika, kushangaa kwake hili lililoanza kushika kasi siku za karibuni la vikao vya mipango ya kusafirisha na mazishi ya marehemu kufanyikia kwenye kumbi za starehe linamfanya adhibitishe wazi kabisa kuwa bado yeye ni mshamba aliyepitwa na wakati. Kwa hili, anakubali aendelee kubaki hivyo.


Friday, March 30, 2007

labda ni woga wake tu, lakini huyu muandika blogu ana wasiwasi sana na hizi dawa mpya zinazoingizwa na kutangazwa kwa nguvu zote nchini...!


Miongoni mwa maneno ambayo yalipata kumtatanisha mno huyu mwanablogu mwenzenu
mwanzoni mwanzoni kabisa mwa safari yake ndeefu ya kujua kusoma na kuandika, yalikuwa haya; Human Guinea Pigs.
Alikuwa anatatizika mno kila aliposoma mahali kuwa walikuwepo binadamu ambao walikuwa wamekubali, ama kwa hiyari ama kwa malipo maalumu, kuwa ‘Guinea Pigs’, neno ambalo mpaka hapo huyu muandika katikati ya mistari alikuwa hana tafsiri yoyote anayofahamu zaidi ya ile ya ‘Nguruwe wa Guinea’!

Alitatizika na kujiuliza mno ni kwa vipi binadamu, tena mara nyingi zaidi binadamu mwenyewe mzungu afikie hatua ya kuitwa na kukubali kuitwa Nguruwe, tena Nguruwe mwenyewe kutoka Guinea, nchi iliyo Bara la weusi la Afrika!

Ni baada ya makonzi mengi kichwani kutoka kwa walimu wake ndipo huyu mwanablogu alipofahamu kuwa kilichokuwa kimepewa jina la ‘Human Guinea Pigs’ hakikuwa Nguruwe wa nchi ya Guinea bali kitu kingine tofauti kabisa na alichokuwa akifikiri.

Ndio. Ni baadaye sana huyu Chizi wa mwisho wa mzee Mpilipili alipong’amua kuwa alichokuwa akidhani ni Kiti moto wa nchi ya Guinea ilikuwa ni binadamu waliokubali kutoa miili yao, kwa hiari ama kwa kukatiwa uchache, ili iwe chambo cha majaribio ya aina fulani ya dawa iliyokuwa inafanyiwa utafiti kabla haijapitishwa kwa matumizi ya binadamu.

Akatambua kuwa kumbe badala ya Human Guinea Pigs, kwa hapa nyumbani angeweza hata kutumia maneno ya Mbuzi wa Shughuli na yakakidhi haja, potelea mbali kwamba haya ya kwetu yalikuwa na muelekeo wa masuala ya msosi zaidi kuliko masuala ya kisayansi!

Kuna matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea kwenye nchi njema ya Bongo ambayo yamekuwa yakimfanya muandika blogu aanze kuhisi kuwa yeye na Ndugu zake wabongo wamekuwa wakigeuzwa Human Guinea Pigs ama Mbuzi wa shughuli bila wao wenyewe kujua.

Amekuwa akiangalia, na kushitukia, kasi ya madawa mapya yanayoingizwa kwa ajili ya matumizi ya wabongo na kuona dalili za wazi kabisa za Ndugu zake kugeuzwa Mbuzi wa shughuli.

Mchangiaji huyu wa blogu anakumbuka mno jinsi dawa iliyomtibu malaria tangia anazaliwa hadi uzeeni ya klorokwini ilivyoondolewa wangu wangu kwenye soko kwa maelezo kwamba ilikuwa imeshindwa kazi na badala ya kutibu ilikuwa imejenga urafiki na malaria.

Ikaondolewa hima kwenye soko na kukaingizwa dawa ya Esipi iliyotangazwa kwa mapana marefu kwamba ndio kiboko cha malaria yote. Sijui kama ilikuwa hivyo lakini dhahiri malalamiko ya baadhi ya watumiaji wake yalipunguza sana soko lake. Bado tuna kumbukumbu za baadhi ya Ndugu zetu waliotolewa malengelenge na kubabuliwa na dawa hizo ingawaje mara zote jamaa walikanusha.

Haya, kulikuwepo pia na dawa ya kuulia wadudu Kuanzia chawa, mende, papasi hadi wadudu waharibifu wa mimea, iliyokuwa inaitwa DDT. Ni wale waliokwisha kula kilo kadhaa za chumvi tu ndio watakuwa na kumbukumbu muhimu kuhusiana na dawa hii.

Ndio, ni wale tu ambao utotoni waliruhusu miguu yao kufanya urafiki na funza na kuziruhusu kujenga makazi ndio watakumbuka jinsi wakubwa wetu baada ya kututoa funza hizo na pini walivyochukua dawa ya DDT na kuipaka kwenye mashimo yaliyobaki wazi miguuni baada ya ‘dhahabu’ funza kuchimbwa!

Unaambiwa ukali wa dawa ya DDT kwenye mashimo yaliyobaki wazi miguuni baada ya kuondolewa funza ulitufanya tucheze ngoma za kikwetu pamoja na udogo wetu! Uzuri wake ni kuwa baada ya hapo hata funza zenyewe ziliogopa kusogelea miguu yetu kwa kipindi kirefu tu kilichofuata! DDT ilikuwa DDT kweli!

Miaka michache iliyopita, dawa hii mashuhuri ya wakati wetu ya kuulia wadudu ikapigwa stoop, kwa maelezo kwamba baada ya uchunguzi wa muda mrefu ilikuwa imegundulika kuwa inaharibu ardhi mbali na kuwa ni sumu na kadhalika na kadhalika na kadhalika, ambazo sisi tuliokuwa tukiifahamu hatukuzielewa.

Tukakubali. Tungefanyaje na hali waheshimiwa wameishaamua. Tukasubiri kuletewa dawa mbadala ambayo tungepaka kwenye miguu ya watoto wetu tuliyotoa funza na ambayo ingefanya funza hao kujiuliza mara mbili mbili kabla ya kurudi, hakuna kilichoendelea.

Badala yake, miaka michache tu baadaye, hivi majuzi, tukatangaziwa kuwa baada ya uchunguzi wa muda mrefu na kadhalika na kadhalika nyiingi ambazo hatukuzielewa, dawa ya DDT ingerudishwa tena kwenye soko ili kukabiliana na mbu ingawaje ingekuwa inapuliziwa kwenye kuta tu basi.

Hakuna aliyetuambia ilikuwaje uchunguzi wa muda mrefu wa kwanza ulionyesha kuwa DDT ilikuwa haifai kwa matumizi ya binadamu halafu uchunguzi mwingine wa muda mrefu ubaini sasa kuwa ilikuwa inafaa!

Haya. Katika siku mbili tatu hivi za karibuni mwanablogu anashuhudia kuingizwa sokoni kwa mchanyato wa dawa mpya ya kutibu malaria inayopigiwa chapuo kwa mapana na mareefu kwenye redio na tiivii zetu.

Kabla ya hapo, mchanyato pekee ambao Chesi alikuwa akiufahamu, na kuchangamkia, ni ule uliohusu ndizi zilizochanganywa ama na maharage ama na utumbo, uliokuwa ukipikwa na mama yake na baadaye huyu mwanamke wa maisha yake. Kwamba mchanyato sasa umeingia kwenye dawa amechoka kabisa!

Mchangiaji wa Blogu anazo pia taarifa za watoto wake na wetu wanaosoma shule za shule msingi kuchomwa sindano hii ama kunyweshwa dawa hii ama ile bila yeye angalau kupewa taarifa tu kabla ya jambo hilo kufanyika. Amekuwa pia akijiuliza mno iwapo haya yanafanyika hata kule kwenye shule za ‘Watakatifu’ ama ni huku uswazi kwetu tu.

Ndio, amekuwa akiishia kubaki mdomo wazi kila pale wanawe wanaporudi shule na kumfahamisha kumtaarifu kuwa siku hiyo shuleni wamechomwa sindano ya kinga hii ama ile ama kunyweshwa dawa hii ama ile, taarifa ambazo anadhani alipaswa kupewa kabla jambo hilo kufanyika ili ajiandae kwa Saidi-Efeckti yoyote inayoweza kutokea!

Ni mambo kama haya yanayomfanya muandika katikati ya mistari aanze kujiuliza iwapo, bila kujua na hivyo kuwa na haki ya kudai mgawo, hatujaanza kugeuzwa Nguruwe wa Guinea ama Mbuzi wa Shughuli! Tutafakari.

Wednesday, February 28, 2007

Tumeambiwa kuwa timu kabambe ya Real Madrid itakuja nchini na umati wa watu 80 na wanene wetu wametakiwa kujiandaa kutoa michango ili kufanikisha ujio wa miungu hao wadogo. Hili ndio tunalohitaji...??

Safari ya huyu mwanablogu mwenzenu ya kutafuta umaarufu, ujiko na ulaji kupitia soka, kandanda, kabumbu ama mpira wa miguu ilikatishwa rasmi alasiri ile ya tarehe ile ya 19 ya mwezi Juni mwaka wa 1975, miaka thelathini na mbili iliyopita.

Hii ndiyo siku ambayo goti lake lilivunjika na kubaki nyang’anyang’a wakati akiwa kwenye mechi ya michuano ya mabweni akiwa ‘nyoya’, jina walilobatizwa ma-form one wote, pale shule ya sekondari ya Musoma Alliance. Bila shaka Mwamoyo Hamza wa VOA bado anakumbuka hili maana yeye ndiye alikuwa nahodha wa bweni akiwa kidato cha sita.

Kwa shinikizo la wazazi, Ndugu na jamaa zake, mchezo wa soka ukawa kwake Kuanzia siku ile ukawa kama vile kibaka akionavyo kituo cha polisi. Kitu cha kupishia mbali kabisa kisichostahili kuguswa hata kwa upondo wa futi mia.

Mwanablogu mwenzenu huyu alijaribu kujiingiza kwenye michezo mingine kinyemela na kwa namna moja ama nyingine kufanikiwa kiasi cha kufikia hatua ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa mchezo wa handball mwaka 1981, lakini hiyo ni habari nyingine ambayo hatuna nafasi nayo hapa kwa leo.

Anachotaka kusema Chesi ni kwamba yeye ni mpenzi wa michezo ukiwemo huu wa mpira wa miguu lakini upenzi wake huu haujafikia pale baadhi ya watu wanapolazimisha kuwa ukiwa mpenzi wa mpira wa miguu hapa Bongo basi ni lazima uwe ama Jangwani ama Msimbazi.

Ndio, Chesi ni mpenzi wa soka kwa maana ya kwamba anapenda timu yoyote inayocheza soka la kufundishwa na kuvutia kama ilivyokuwa Ushirika ya Moshi na Coastal Union ya Tanga kwenye miaka ya katikati ya 80 ama Pamba ya Mwanza mwishoni mwa miaka hiyo ya themanini na ya Tisini mwanzoni.

Ukichukulia kwamba kwenye miaka hiyo hiyo huyu alikuwa tayari na eneo la kujidai kama hili lakini kwenye kurasa za michezo za gazeti la kiingereza la jumapili la siri-ukali, bila shaka anayo haki ya kuchangia jambo linalohusu michezo bila mtu kuibuka na kudai kuwa anaingia maeneo ya watu ya kujidai.

Haya, majuzi tumepokea taarifa kuwa katikati ya mwaka huu kutakuwa na ugeni mkuuubwa, kwa maana halisi, unaohusu mojawapo ya timu bora kabisa za kandanda ulimwenguni ya ‘kweli’ Madrid.

Tumeambiwa kuwa timu hiyo itawasili nchini na umati mkuuubwa wa watu themanini na tayari mipango inaandaliwa ya kuunda kamati ambayo pamoja na mambo mengi mengineyo itakuwa na kazi kubwa ya kukusanya masimbi kwa ajili ya kuukirimu ugeni huo mkubwa na kwa hakika, wa kutisha. Mtu themanini?

Mwanablogu anajua kabisa kwamba anatafuta kuzabwa vibao na watu huko manjiani maana kuna watu wakitaka lao jambo basi tena, huwa hawasikii la muadhini wala mshona kanzu!lakini anaamini kuwa kwa vile kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake ili mradi tu havunji sheria za nchi, anaomba kusema wazi kabisa. haifagilii ziara ya umati huo mkubwa wa watu. Angalau kwa wakati huu.

Chesi anadhani kuwa yapo mambo mengine kibao ambayo tunayo na hawa Billy Gates wetu wa kibongo wetu wanapaswa kupewa changamoto la kuyachangia na sio kuchangia ujio wa miungu wadogo hawa themanini katika medani ya soka.

Ndio, ni miungu wadogo katika medani ya soka na ndio maana ugeni wao mmoja unakuwa rundo la watu themanini. Hapana shaka kuwa ndani ya rundo kubwa hili la watu, kila galacha atakuja na mpishi wake, dakitari wake wa meno na pengine hata mrembeshaji wake!

Muandika katikati ya mistari hafagilii ziara ambayo tutalazimika kumlipa hata kinyozi ama mpiga kiwi viatu wa nyota wa timu hiyo.

Si hayo tu. Mchangia blogu mwenzenu huyu hataki ujio wa timu ambayo ana uhakika itamlazimu kutumia darubini kuwaona nyota wake maana mabaunsa wao watahakikisha kuwa akina Chesi watajuta na kuona ni afadhali vile wanavyowaona nyota hao kwenye tiivii maana angalau kuna wakati kamera zinawavuta karibu kiasi hata cha kuweza kuona hata machunusi yao!

Ndio, sana sana ukaribu mwingine tutakaowaona utakuwa ule wa kuwaona wakishikana mikono kusalimiana na wanene wa bongo ambao huwa hawapotezi nafasi yoyote ya kujipatia umaarufu hata kama ni wa bei ndogo namna gani!

Muandishi wa blogu huyu anahofia ugeni wa timu ya magalacha ambao unaweza ukaishia kwa wachezaji hao magalacha kucheza dakika mbili tu kisha wakatoka nje na kuwaacha watoto ama hata wapishi wao wakiwapelekesha puta wachezaji wetu wakati tumeishalipa kiingilio cha laki moja unusu ili kuwaona wao!

Kwa hakika, tunapaswa kujiuliza mno tutawalipa nini wachezaji ambao kwa wiki wanapokea mpaka shilingi milioni mia tatu, rudia tena, kwa wiki! Ni zahama gani hii tunayojitafutia? Kama ni kufungua tu uwanja si tushuke tu hapo bondeni kwa Ndugu zetu wa bafana? kwa nini tusiwaite ndugu zetu wa Naijeria ama Kameruni ama Ghana na kupanga kijiligi kidogo cha kufungulia uwanja wetu?

Mchangia Blogu anaanza kuuona ujio wa magalacha hawa kuwa kama sherehe za harusi za kibongo. Watu wanachanga malaki, siku ya harusi yenyewe wanaishia kupata shingo ya kuku aliyekonda na kijiwali ama tuchipsi tuwili halafu kesho yake hawana hata nauli ya daladala ya kuendea kazini huku maarusi wakiwa kwenye hoteli ya nyota tano wakijinafasi!

Muandika katikati hataki nchi yake njema ya bongo kuingizwa mjini potelea mbali kwamba tunao uzoefu wa kutosha tu wa kuingizwa ingizwa mjini.

Monday, February 12, 2007

...kuna haya maneno mawili ambayo matamshi yake yanasumbua sana wabongo. Ama wabongo ndio wanaopenda wenyewe kujisumbua...?

Lipo neno moja na herufi moja ambavyo kila mara muandika katikati ya mistari anaposikia yanavyotamkwa na wabongo wenzake walio wengi amekuwa akijiuliza mno juu ya umakini wetu katika lugha.

Ni neno na herufi ambavyo kukosewa kwake umakini katika kuyatamka hakuwezi kusingiziwa lafudhi ya kabila Fulani ama kisomo cha mtu.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba kukosa umakini katika kuyatamka maneno haya kunafanywa na kiila mtu ndani ya jamii hii ya wabongo. Kuanzia maprofesa hadi wauza gongo, walimu na wanafunzi wao na wanamuziki kwa wacheza ngoma.

Kwanza kuna hili neno ‘kudipu’ ambalo wengi wa watamkaji wake wanapolitamka wana maana ya neno ku’beep’, neno ambalo katika pekua pekua ya muandika katikati ya mistari kwenye makabrasha na madikishenari yake amekuta lina maana ya kutoa aina Fulani ya mlio.

Muandika katikati ya mistari amekuwa akisikia baadhi ya wabongo wenzake wakikazana kusema kwa uhakika kabisa ‘kudipu’ wakiwa na maana ya ‘kubeep’ ama ‘kubipu’ neno ambalo kwa tafsiri ya jamii ya wabongo lina maana ya kutaka kumtia demeji mwenzio wakati simu ulinunua mwenyewe.

Katika pekua pekua yake ndani ya makabrasha na madikishenari yake, muandika katikati ya mistari amejaribu kutafuta tafsiri ya neno dipu kwa maana ya ‘deep’ na anachopata ni kitu ambacho hakina uhusiano wowote na mambo ya kupiga simu.

Ndio, kwa mujibu wa makabrasha na madikishenari ya Chesi, neno ‘dipu’ linalotoholewa kutoka ‘deep’ kwa tafsiri hafifu na ya haraka haraka lina maana ya ndani, ndani zaidi ama kwenda ndani zaidi, mbali na maana nyingine kibao ambazo tukiamua kuziorodhesha zote, patakuwa hapatoshi hapa...

Kubwa ni kwamba katika maana zote za neno hili, muandika katikati hakuona hata inayoelekea kufanana fanana na mambo ya simu. Hii ina maana kwamba watu wanapokazania kusema ‘promota anadipu’ wanakuwa na maana ya kwamba promota ameingia ndani zaidi ama sijui vipi. Hata haiji.

Hapa muandika katikati ya mistari anawaomba wanajamii wenzake kukubaliana naye tu kwamba ni kuBeep ama ‘kubipu’ na sio ‘kuDipu’ ama kuDeep’. Unakwenda ndani zaidi wapi?
Halafu kuna hii herufi inayokanganya mno watu ya H. tayari nawasikia baadhi ya wanajamii wakiitamka kwa namna ile ile iliyo chanzo cha makala hii., ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’.

Muandika katikati ya mistari anakumbuka jinsi walimu wake wote wa Kiswahili aliopitia kuanzia chekechea ya shule ya vidudu ya kindergarten ya awali hadi alipofika pa kufika kimadarasa walivyokuwa wakimsisitizia kwamba herufi H ilikuwa inatamkwa ‘Echi’ na kamwe sio ‘Hechi’!

Anakumbuka jinsi baadhi ya walimu wake hao walivyofikia hatua ya kumtembezea fito makalioni ama kumgonga na rula kichwani hata pale ulimi wake ulipoteleza tu na kuitamka H kama 'Hechi' badala ya H, na kumuacha ajaze mwenyewe kwamba ulimi hauna mfupa.

Waama, kwa watembeza fito na wagonga rula vichwani hawa, yalikuwepo maneno mengi ambayo binadamu angeweza kukosea kuyatamka na kusingia ulimi wake kukosa mfupa lakini kamwe sio herufi H, maana hata kutamka 'Hechi' ama 'Echi' kwenyewe kulikuwa hakuhitaji matumizi ya ulimi kiasi hicho!

Ni kwa mantiki hii ndio maana muandika katikati ya mistari anashangazwa mno na idadi kubwa ya wanajamii ambao wanasikika wakitamka kwa mapana na marefu na bila wasiwasi wa aina yoyote herufi H kama ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’ huku wengi wakitamka hivyo wakiwa wameshiba kabisa ugali!

Muandika katikati ya mistari amekuwa kila apatapo nafasi akijaribu kurekebisha mapungufu haya akianzia na nyumbani kwake mwenyewe lakini haoni kama anapata mafanikio sana katika hili.

Hawasemi kwa mdomo lakini huwa anaona sura za watoto wake zikimuambia wazi kabisa kuwa aache fiksi, maana kama watangazaji wenye majina makubwa kabisa wa vituo vya Tiivii na redio wanatamka ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’, yeye ni nani hata awakosoe. Kama ni yeye anayekosea?

Naam, ndio maana hatuishi kusikia taarifa za habari za akina ‘hAli’ badala ya ‘Ali’ wanaosafiri hadi ‘Harusha’ badala ya Arusha kwenda kuongeza ‘Helimu’ badala ya Elimu! fikiria matamshi haya yanapotamkwa na mtu aliyetoka kushiba ugali na anatumia nguvu ya ugali huo kutamka hiyo 'Hechi'!

Huku mitaani anakopita ndio kabisaa hawamkopeshi. Wabishi wamekuwa wakimuuliza wazi kabisa kuwa tatizo ni nini, si mradi anaelewa? Hawataki kukubali kabisa kuwa tatizo sio kuelewa, bali ni kufuata kanuni.

Muandika katikati ya mistari hajakubali kushindwa na kamwe hatakubali ili tu yaishe. Na ndio maana anazidi kukandamiza. Kwa wale wote wanaosema ‘kudipu’ badala ya kubeep na ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’…samahani Regina…Acheeni hizoo!

Tuesday, February 06, 2007

..Kuna huu mchezo ambao katika siku za karibuni umeshika kasi sana miongoni mwa wabongo. kufukuza kuku. sikubaliani nao...

Kwa sisi ambao tulizaliwa 'mitaa' ya mwaka 47, kuku ni miongoni mwa viumbe muhimu kabisa vilivyoumbwa na Muumba wetu na vinavyopaswa kuheshimiwa na kuenziwa kwa nguvu zetu zote.
Naomba kuharakisha kufafanua kabisa hapa kwamba ninapozungumzia kuku ninazungumzia kuku kwa maana halisi ya kuku na sio hii mizoga inayochinjiwa nchi fulani ya mbali mwezi wa tisa na kuja kuuzwa hapa mwezi wa kumi na mbili.

Ndio, sizungumzii hawa kuku wenu wa kisiku hizi ambao ukiingia kwenye banda ukikuta mmoja ni mwekundu basi ni wote ni wekundu kama vile wamevaa sare ya shule tofauti kabisa na wale kuku wetu ambao kuku moja anaweza kuwa na rangi arobaini kidogo, kahawia, njano, nyekundu na hata bluu ili mradi kwa raha zako...!

No. ninapozungumzia kuku nina maana ya yule kuku ambae anajua kubangaiza mwenyewe kutafuta msosi na chochote kinachokatisha mbele ya mdomo wake basi ni halali na ni msosi tosha. iwe ni jongoo, gololi, vigae vya chupa, mkaa, kinyesi cha binadamu na hata cha kwake mwenyewe, vyoote ni mbele kwa mbele!

Nazungumzia yule kuku ambaye kwa kawaida kule vijijini tunakotoka, kuchinjwakwake, ikianzia pale watu wanapoanza kunoa kisu ambacho kabla ya hapo kazi yake kuu ilikuwa ile ya kumenyea viazi vikuu, ndizi na mihogo ndio alama kuu ya kuwa nyumba fulani imefikiwa na wageni!
Nazungumzia yule kuku ambaye anapoona masanduku yakiingia tu kwenye nyumba kuashiria mgeni machale yanamcheza na anatoweka haraka kwenye maeneo jirani hadi pale mkuu wa nyumba anapotoa amri ya kumkamata na kumchinja kuku mwingine anayeshangaa shangaa wakati wenzake wameingia mitini kuepuka kuwa kitoweo cha mgeni!

Aha! namzungumzia kuku wa kienyeji ambaye ili kupata mnofu wake ni lazima mdomo wako na mkono wako kwanza vicheze mchezo usikokuwa na tofauti sana na mchezo wa kuvutana kamba. kutafuna mfupa? sahau. labda kama huna haja tena na taya lako!

Naam, namzungumzia huyu kuku wa kibantu ambaye mwanzoni kabisa mwa miaka ya sitini wakati makamasi yakiwa kitambulisho muhimu na cha kudumu usoni mwangu, marehemu mzee Mpilipili alikuwa nao kama alfu tatu ama nne hivi waliomfanya kuwa miongoni mwa wafugaji wa nguvu sana wa kuku mitaa ya huko usambaani enzi hizoo.

Na wakawa ni kuku hawa hawa ambao stepu fulani wakapitiwa na kombora lililokuwa likijulikana enzi hizo kama kideri ama mdondo ambapo walianza kufa kwa mamia yao kama hawana akili nzuri vile.

Ikamlazimu Mzee Mpilipili kutoa ruksa ya kumshughulikia kuku yeyote aliyeonekana kusinzia sinzia kulikokuwa ndio dalili ya kupatwa na kideri. ruksa ikawa imepewa watu ambao hawapigiwi wanacheza, sembuse wakipigiwa. ikawa ni mauaji ya kimbari ya kuku.

Unaambiwa mambo yote yakawa ni kuku 24 hours. Tena bila mrija, mwanangu. asubuhi kuku kwa uji. mchana kuku kwa makande na usiku kuku kwa Bada. hujui bada? Pole. tafuta rafiki yako wa kisambaa akujuze. ndipo utakapojua kuwa kuna vitu vyeusi kabisa kuliko giza ulimwenguni humu!

Pamoja na yote hayo, bado mzee Mpilipili aliendelea kuwa na kawaida ya kutusisitizia kumuheshimu kuku na mnyama mwingine yoyote kwani kila mnyama alistahili heshima. kwamba hata kule kubeba mifupa iliyokwanguliwa vyema na vinjino vyetu na kwenda kuwaringishia watoto wenzetu haikuwa imetulia na ilikuwa ni sawa na kuchezea chakula.

Naam, ndivyo tulivyokuzwa na tukakua tukiamini kwamba kweli, kila kiumbe kilichoumbwa na Muumba kilistahili heshima hata kama kilikuwa ni kitoweo tu.

Kwa bahati mbaya kabisa, katika siku za karibuni ama kwa kisingizio cha siku zote cha kwenda na wakati ama kwa kukosa busara tu, muandika katikati ya misatri anashuhudia kile ambacho kwa mzee Mpilipili kisingekuwa pungufu ya kuchezea chakula.

Muandika katikati ya mistari anashitushwa na kushangazwa na tabia iliyoshika kasi ya kuku kugeuzwa kuwa ni kifaa cha michezo kama ilivyo kwa mpira ama nyavu za magoli. anashangaa kuona kila watu wanapokusanyika kwa sherehe hii ama ile, miongoni mwa michezo inayopewa chati kwa sana unakuwa ule kufukuza kuku!

Tena basi afadhali mchezo wenyewe ungekuwa unafanywa na na watoto wadogo, sivyo. muandika katikati ya mistari anaachwa hoi kabisa pale anaposhuhudia mijitu mizima na mavitambi yao, sijui akili, eti yakifukuzana na kuku!

Yaani kukimbia na gunia ama na chupa kichwani ama na kijiko chenye yai mdomoni sasa si michezo tosha tena hadi watu wazima na fahamu zao wamtese kuku kwa kumfukuza huku na huko na kumfanya atoe ulimi nje huku wafukuzaji na mavitambi yao wakihema na kutoa ulimi nje maradufu! kwa hakika ni bahati yao tu kuwa kile chama cha kutetea haki za wanyama sasa kimebaki herufi kubwa tu!

Marehemu mzee Mpilipili alikuwa hakopeshi kusema ni kuchezea chakula pale alipomuona mtu anaviringisha tonge zaidi ya mara tatu nne zilizotakiwa ili kuliweka katika hali nzuri ya kupita kooni. mi mwanayenaamini kuwa kufukuza kuku kama aina fulani ya mchezo hakuna tofauti yoyote na kuchezea chakula. nawakilisha.