Friday, August 24, 2007

Kuna hii fasheni mpya ambayo imeshika kasi kama moto wa nyika ya kufanyia vikao vya maandalizi ya mazishi ya mtu kwenye Bar. Nimeliandikia hili.

Kwanza, huyu wenu mpendwa alidhani hakusikia vizuri tangazo lile. Akatenga vizuri sikio lake kuukuu lililokwisha ona, kama sio kusikia, siku njema na kusikiliza tena kwa makini.

Na si kwamba alichokuwa anataka kusikia kwa ukamilifu kilikuwa ni jina la marhum, la hasha. Hilo alikuwa amelisikia vizuri na kutambua kuwa alikuwa ni mtu ambaye japo hakuwa ndugu yake, alikuwa akimfahamu vizuri. Kulikuwa na kingine kilichomvuta kusikiliza tena tangazo lile.

Na bila khiyana mtoa matangazo akarudia tena. Kwamba alikuwa anasikitika kutangaza kifo cha fulani bin fulani kilichotokea hukoo katika hospitali ya nanihii, habari ziwafikie huyu, huyo na yule wa nanihii na nanihii na mipango ya mazishi ilikuwa inafanywa kwenye baa ya nanihino!

Mipango ya mazishi inafanywa kwenye baa ya nanihii! Hiki ndicho mchangiaji wa Blogu alichodhani kuwa alikuwa hajasikia vizuri. Akawa amedhibitishiwa kwamba alichokuwa amesikia ni kweli na kwamba antena zake, kwa maana ya masikio, hazikuwa kuu kuu kiasi hicho!
Kwamba marehemu fulani bin fulani alikuwa amefariki dunia na ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanakutana kwenye Grosari fulani ili kupanga mipango ya kusafirisha mwili wake kwenda kuzikwa alikozaliwa. Mipango ya mazishi Bar!


Muandika katikati ya mistari na my wife wake wakakumbuka kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa watu wachache hasa ambao ni wacha mungu kwa maana halisi tofauti na akina Chesi ambao ucha Mungu wao unaonekana zaidi siku za jumamosi kwenye harusi badala ya jumapili kwenye misa!

Haya, wakanyanyuana na kuelekea huko kwenye msiba njiani wakiulizana ni masahibu gani yaliyokuwa yameikumba nyumba ya marehemu hadi ikaamuliwe mipango ya mazishi yake ikafanyiwe kwenye baa.

Ndio, wakajiuliza maswali kibao yasiyokuwa na majibu huku kubwa kuliko yote likiwa lile la jinsi marehemu alivyokuwa mcha Mungu na jinsi atakavyokuwa anjisikia huko aliko akiangalia mipango ya kuuzika ya mwili wake ikifanyika Bar!

Tukafika pale nyumbani kwa marehemu ambapo palikuwa na liuwanja likubwa tu la kumwaga na kwa maana hiyo kuondoa dhana kwamba labda watu walikuwa wameamua kwenda kufanyia mipango ya kuusafirisha mwili wake Bar kutokana na kukosa nafasi kwenye makazi yake.

Muandika katikati ya mistari akambwaga mkuu mwenzie pale na kuelekea kule alikoambiwa ndiko mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu na mazishi yake ilikuwa inafanyika. Nanihino Bar.
Akafika pale na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wake kwa waume wakipanga na kupangua kipi kifanyike na kipi kisifanyike kuhusiana na msiba wa ndugu yetu huku mezani kukiwa kumesheheni vituliza majonzi’ kibao.


Kwa hakika, mtu yoyote ambaye angefika pale na kuona kilichokuwa kikiendelea, asingelaumiwa iwapo angedhani kuwa kilichokuwa kikiendelea pale ni kikao cha maandalizi ya harusi! Dhahiri angeshituka mno kuambiwa kuwa kile kilikuwa ni kikao cha maandalizi ya mazishi ya mtu!

Muandika katikati ya mistari anaomba kukiri wazi kuwa alijiunga kukaa kwenye kikao kile kwa machale huku kila mara akigeuka huku na kule akitegemea saa yoyote marehemu mcha Mungu kuwazukia pale na kuwauliza kwa kulikoni walikuwa wanafanyia Bar mipango ya kuzika mwili wake!

Ndio, kwa nini walikuwa wanafanya mipango ya kusafirisha na kuzika mwili wake kwenye eneo ambalo meza ya pembeni kulikuwa na kikao cha maandalizi ya harusi, kandokando yake kulikuwa na kikao cha maandalizi Send-off ya mtu na pembeni kulikuwa pia na kikao cha usuluhishi wa ndoa ya mtu iliyokuwa juu ya mawe!

Muandika katikati ya mistari ameishakiri mara kadhaa huko nyuma kuwa huwa huwa anafanya jitihada za za ziada kuhakikisha kuwa haachwi nyuma na anakwenda sambamba na wakati lakini karibuni mara zote amekuwa akijikuta akiachwa kwenye mataa!

Ndio, aliachwa akishangaa watu walipoanza kuvaa sare za misiba, watu walipoanza kubeba makamera ya video makaburini, watu walipoanza kuwavalisha suti marehemu wakati hawakupata kuwanunulia suti walipokuwa hai na wafiwa walipoanza kwenda saluni kabla ya shughuli ya kuaga miili ya marehemu wao.

Kwa hakika, kushangaa kwake hili lililoanza kushika kasi siku za karibuni la vikao vya mipango ya kusafirisha na mazishi ya marehemu kufanyikia kwenye kumbi za starehe linamfanya adhibitishe wazi kabisa kuwa bado yeye ni mshamba aliyepitwa na wakati. Kwa hili, anakubali aendelee kubaki hivyo.


No comments: