Wednesday, February 28, 2007

Tumeambiwa kuwa timu kabambe ya Real Madrid itakuja nchini na umati wa watu 80 na wanene wetu wametakiwa kujiandaa kutoa michango ili kufanikisha ujio wa miungu hao wadogo. Hili ndio tunalohitaji...??

Safari ya huyu mwanablogu mwenzenu ya kutafuta umaarufu, ujiko na ulaji kupitia soka, kandanda, kabumbu ama mpira wa miguu ilikatishwa rasmi alasiri ile ya tarehe ile ya 19 ya mwezi Juni mwaka wa 1975, miaka thelathini na mbili iliyopita.

Hii ndiyo siku ambayo goti lake lilivunjika na kubaki nyang’anyang’a wakati akiwa kwenye mechi ya michuano ya mabweni akiwa ‘nyoya’, jina walilobatizwa ma-form one wote, pale shule ya sekondari ya Musoma Alliance. Bila shaka Mwamoyo Hamza wa VOA bado anakumbuka hili maana yeye ndiye alikuwa nahodha wa bweni akiwa kidato cha sita.

Kwa shinikizo la wazazi, Ndugu na jamaa zake, mchezo wa soka ukawa kwake Kuanzia siku ile ukawa kama vile kibaka akionavyo kituo cha polisi. Kitu cha kupishia mbali kabisa kisichostahili kuguswa hata kwa upondo wa futi mia.

Mwanablogu mwenzenu huyu alijaribu kujiingiza kwenye michezo mingine kinyemela na kwa namna moja ama nyingine kufanikiwa kiasi cha kufikia hatua ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa mchezo wa handball mwaka 1981, lakini hiyo ni habari nyingine ambayo hatuna nafasi nayo hapa kwa leo.

Anachotaka kusema Chesi ni kwamba yeye ni mpenzi wa michezo ukiwemo huu wa mpira wa miguu lakini upenzi wake huu haujafikia pale baadhi ya watu wanapolazimisha kuwa ukiwa mpenzi wa mpira wa miguu hapa Bongo basi ni lazima uwe ama Jangwani ama Msimbazi.

Ndio, Chesi ni mpenzi wa soka kwa maana ya kwamba anapenda timu yoyote inayocheza soka la kufundishwa na kuvutia kama ilivyokuwa Ushirika ya Moshi na Coastal Union ya Tanga kwenye miaka ya katikati ya 80 ama Pamba ya Mwanza mwishoni mwa miaka hiyo ya themanini na ya Tisini mwanzoni.

Ukichukulia kwamba kwenye miaka hiyo hiyo huyu alikuwa tayari na eneo la kujidai kama hili lakini kwenye kurasa za michezo za gazeti la kiingereza la jumapili la siri-ukali, bila shaka anayo haki ya kuchangia jambo linalohusu michezo bila mtu kuibuka na kudai kuwa anaingia maeneo ya watu ya kujidai.

Haya, majuzi tumepokea taarifa kuwa katikati ya mwaka huu kutakuwa na ugeni mkuuubwa, kwa maana halisi, unaohusu mojawapo ya timu bora kabisa za kandanda ulimwenguni ya ‘kweli’ Madrid.

Tumeambiwa kuwa timu hiyo itawasili nchini na umati mkuuubwa wa watu themanini na tayari mipango inaandaliwa ya kuunda kamati ambayo pamoja na mambo mengi mengineyo itakuwa na kazi kubwa ya kukusanya masimbi kwa ajili ya kuukirimu ugeni huo mkubwa na kwa hakika, wa kutisha. Mtu themanini?

Mwanablogu anajua kabisa kwamba anatafuta kuzabwa vibao na watu huko manjiani maana kuna watu wakitaka lao jambo basi tena, huwa hawasikii la muadhini wala mshona kanzu!lakini anaamini kuwa kwa vile kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake ili mradi tu havunji sheria za nchi, anaomba kusema wazi kabisa. haifagilii ziara ya umati huo mkubwa wa watu. Angalau kwa wakati huu.

Chesi anadhani kuwa yapo mambo mengine kibao ambayo tunayo na hawa Billy Gates wetu wa kibongo wetu wanapaswa kupewa changamoto la kuyachangia na sio kuchangia ujio wa miungu wadogo hawa themanini katika medani ya soka.

Ndio, ni miungu wadogo katika medani ya soka na ndio maana ugeni wao mmoja unakuwa rundo la watu themanini. Hapana shaka kuwa ndani ya rundo kubwa hili la watu, kila galacha atakuja na mpishi wake, dakitari wake wa meno na pengine hata mrembeshaji wake!

Muandika katikati ya mistari hafagilii ziara ambayo tutalazimika kumlipa hata kinyozi ama mpiga kiwi viatu wa nyota wa timu hiyo.

Si hayo tu. Mchangia blogu mwenzenu huyu hataki ujio wa timu ambayo ana uhakika itamlazimu kutumia darubini kuwaona nyota wake maana mabaunsa wao watahakikisha kuwa akina Chesi watajuta na kuona ni afadhali vile wanavyowaona nyota hao kwenye tiivii maana angalau kuna wakati kamera zinawavuta karibu kiasi hata cha kuweza kuona hata machunusi yao!

Ndio, sana sana ukaribu mwingine tutakaowaona utakuwa ule wa kuwaona wakishikana mikono kusalimiana na wanene wa bongo ambao huwa hawapotezi nafasi yoyote ya kujipatia umaarufu hata kama ni wa bei ndogo namna gani!

Muandishi wa blogu huyu anahofia ugeni wa timu ya magalacha ambao unaweza ukaishia kwa wachezaji hao magalacha kucheza dakika mbili tu kisha wakatoka nje na kuwaacha watoto ama hata wapishi wao wakiwapelekesha puta wachezaji wetu wakati tumeishalipa kiingilio cha laki moja unusu ili kuwaona wao!

Kwa hakika, tunapaswa kujiuliza mno tutawalipa nini wachezaji ambao kwa wiki wanapokea mpaka shilingi milioni mia tatu, rudia tena, kwa wiki! Ni zahama gani hii tunayojitafutia? Kama ni kufungua tu uwanja si tushuke tu hapo bondeni kwa Ndugu zetu wa bafana? kwa nini tusiwaite ndugu zetu wa Naijeria ama Kameruni ama Ghana na kupanga kijiligi kidogo cha kufungulia uwanja wetu?

Mchangia Blogu anaanza kuuona ujio wa magalacha hawa kuwa kama sherehe za harusi za kibongo. Watu wanachanga malaki, siku ya harusi yenyewe wanaishia kupata shingo ya kuku aliyekonda na kijiwali ama tuchipsi tuwili halafu kesho yake hawana hata nauli ya daladala ya kuendea kazini huku maarusi wakiwa kwenye hoteli ya nyota tano wakijinafasi!

Muandika katikati hataki nchi yake njema ya bongo kuingizwa mjini potelea mbali kwamba tunao uzoefu wa kutosha tu wa kuingizwa ingizwa mjini.

Monday, February 12, 2007

...kuna haya maneno mawili ambayo matamshi yake yanasumbua sana wabongo. Ama wabongo ndio wanaopenda wenyewe kujisumbua...?

Lipo neno moja na herufi moja ambavyo kila mara muandika katikati ya mistari anaposikia yanavyotamkwa na wabongo wenzake walio wengi amekuwa akijiuliza mno juu ya umakini wetu katika lugha.

Ni neno na herufi ambavyo kukosewa kwake umakini katika kuyatamka hakuwezi kusingiziwa lafudhi ya kabila Fulani ama kisomo cha mtu.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba kukosa umakini katika kuyatamka maneno haya kunafanywa na kiila mtu ndani ya jamii hii ya wabongo. Kuanzia maprofesa hadi wauza gongo, walimu na wanafunzi wao na wanamuziki kwa wacheza ngoma.

Kwanza kuna hili neno ‘kudipu’ ambalo wengi wa watamkaji wake wanapolitamka wana maana ya neno ku’beep’, neno ambalo katika pekua pekua ya muandika katikati ya mistari kwenye makabrasha na madikishenari yake amekuta lina maana ya kutoa aina Fulani ya mlio.

Muandika katikati ya mistari amekuwa akisikia baadhi ya wabongo wenzake wakikazana kusema kwa uhakika kabisa ‘kudipu’ wakiwa na maana ya ‘kubeep’ ama ‘kubipu’ neno ambalo kwa tafsiri ya jamii ya wabongo lina maana ya kutaka kumtia demeji mwenzio wakati simu ulinunua mwenyewe.

Katika pekua pekua yake ndani ya makabrasha na madikishenari yake, muandika katikati ya mistari amejaribu kutafuta tafsiri ya neno dipu kwa maana ya ‘deep’ na anachopata ni kitu ambacho hakina uhusiano wowote na mambo ya kupiga simu.

Ndio, kwa mujibu wa makabrasha na madikishenari ya Chesi, neno ‘dipu’ linalotoholewa kutoka ‘deep’ kwa tafsiri hafifu na ya haraka haraka lina maana ya ndani, ndani zaidi ama kwenda ndani zaidi, mbali na maana nyingine kibao ambazo tukiamua kuziorodhesha zote, patakuwa hapatoshi hapa...

Kubwa ni kwamba katika maana zote za neno hili, muandika katikati hakuona hata inayoelekea kufanana fanana na mambo ya simu. Hii ina maana kwamba watu wanapokazania kusema ‘promota anadipu’ wanakuwa na maana ya kwamba promota ameingia ndani zaidi ama sijui vipi. Hata haiji.

Hapa muandika katikati ya mistari anawaomba wanajamii wenzake kukubaliana naye tu kwamba ni kuBeep ama ‘kubipu’ na sio ‘kuDipu’ ama kuDeep’. Unakwenda ndani zaidi wapi?
Halafu kuna hii herufi inayokanganya mno watu ya H. tayari nawasikia baadhi ya wanajamii wakiitamka kwa namna ile ile iliyo chanzo cha makala hii., ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’.

Muandika katikati ya mistari anakumbuka jinsi walimu wake wote wa Kiswahili aliopitia kuanzia chekechea ya shule ya vidudu ya kindergarten ya awali hadi alipofika pa kufika kimadarasa walivyokuwa wakimsisitizia kwamba herufi H ilikuwa inatamkwa ‘Echi’ na kamwe sio ‘Hechi’!

Anakumbuka jinsi baadhi ya walimu wake hao walivyofikia hatua ya kumtembezea fito makalioni ama kumgonga na rula kichwani hata pale ulimi wake ulipoteleza tu na kuitamka H kama 'Hechi' badala ya H, na kumuacha ajaze mwenyewe kwamba ulimi hauna mfupa.

Waama, kwa watembeza fito na wagonga rula vichwani hawa, yalikuwepo maneno mengi ambayo binadamu angeweza kukosea kuyatamka na kusingia ulimi wake kukosa mfupa lakini kamwe sio herufi H, maana hata kutamka 'Hechi' ama 'Echi' kwenyewe kulikuwa hakuhitaji matumizi ya ulimi kiasi hicho!

Ni kwa mantiki hii ndio maana muandika katikati ya mistari anashangazwa mno na idadi kubwa ya wanajamii ambao wanasikika wakitamka kwa mapana na marefu na bila wasiwasi wa aina yoyote herufi H kama ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’ huku wengi wakitamka hivyo wakiwa wameshiba kabisa ugali!

Muandika katikati ya mistari amekuwa kila apatapo nafasi akijaribu kurekebisha mapungufu haya akianzia na nyumbani kwake mwenyewe lakini haoni kama anapata mafanikio sana katika hili.

Hawasemi kwa mdomo lakini huwa anaona sura za watoto wake zikimuambia wazi kabisa kuwa aache fiksi, maana kama watangazaji wenye majina makubwa kabisa wa vituo vya Tiivii na redio wanatamka ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’, yeye ni nani hata awakosoe. Kama ni yeye anayekosea?

Naam, ndio maana hatuishi kusikia taarifa za habari za akina ‘hAli’ badala ya ‘Ali’ wanaosafiri hadi ‘Harusha’ badala ya Arusha kwenda kuongeza ‘Helimu’ badala ya Elimu! fikiria matamshi haya yanapotamkwa na mtu aliyetoka kushiba ugali na anatumia nguvu ya ugali huo kutamka hiyo 'Hechi'!

Huku mitaani anakopita ndio kabisaa hawamkopeshi. Wabishi wamekuwa wakimuuliza wazi kabisa kuwa tatizo ni nini, si mradi anaelewa? Hawataki kukubali kabisa kuwa tatizo sio kuelewa, bali ni kufuata kanuni.

Muandika katikati ya mistari hajakubali kushindwa na kamwe hatakubali ili tu yaishe. Na ndio maana anazidi kukandamiza. Kwa wale wote wanaosema ‘kudipu’ badala ya kubeep na ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’…samahani Regina…Acheeni hizoo!

Tuesday, February 06, 2007

..Kuna huu mchezo ambao katika siku za karibuni umeshika kasi sana miongoni mwa wabongo. kufukuza kuku. sikubaliani nao...

Kwa sisi ambao tulizaliwa 'mitaa' ya mwaka 47, kuku ni miongoni mwa viumbe muhimu kabisa vilivyoumbwa na Muumba wetu na vinavyopaswa kuheshimiwa na kuenziwa kwa nguvu zetu zote.
Naomba kuharakisha kufafanua kabisa hapa kwamba ninapozungumzia kuku ninazungumzia kuku kwa maana halisi ya kuku na sio hii mizoga inayochinjiwa nchi fulani ya mbali mwezi wa tisa na kuja kuuzwa hapa mwezi wa kumi na mbili.

Ndio, sizungumzii hawa kuku wenu wa kisiku hizi ambao ukiingia kwenye banda ukikuta mmoja ni mwekundu basi ni wote ni wekundu kama vile wamevaa sare ya shule tofauti kabisa na wale kuku wetu ambao kuku moja anaweza kuwa na rangi arobaini kidogo, kahawia, njano, nyekundu na hata bluu ili mradi kwa raha zako...!

No. ninapozungumzia kuku nina maana ya yule kuku ambae anajua kubangaiza mwenyewe kutafuta msosi na chochote kinachokatisha mbele ya mdomo wake basi ni halali na ni msosi tosha. iwe ni jongoo, gololi, vigae vya chupa, mkaa, kinyesi cha binadamu na hata cha kwake mwenyewe, vyoote ni mbele kwa mbele!

Nazungumzia yule kuku ambaye kwa kawaida kule vijijini tunakotoka, kuchinjwakwake, ikianzia pale watu wanapoanza kunoa kisu ambacho kabla ya hapo kazi yake kuu ilikuwa ile ya kumenyea viazi vikuu, ndizi na mihogo ndio alama kuu ya kuwa nyumba fulani imefikiwa na wageni!
Nazungumzia yule kuku ambaye anapoona masanduku yakiingia tu kwenye nyumba kuashiria mgeni machale yanamcheza na anatoweka haraka kwenye maeneo jirani hadi pale mkuu wa nyumba anapotoa amri ya kumkamata na kumchinja kuku mwingine anayeshangaa shangaa wakati wenzake wameingia mitini kuepuka kuwa kitoweo cha mgeni!

Aha! namzungumzia kuku wa kienyeji ambaye ili kupata mnofu wake ni lazima mdomo wako na mkono wako kwanza vicheze mchezo usikokuwa na tofauti sana na mchezo wa kuvutana kamba. kutafuna mfupa? sahau. labda kama huna haja tena na taya lako!

Naam, namzungumzia huyu kuku wa kibantu ambaye mwanzoni kabisa mwa miaka ya sitini wakati makamasi yakiwa kitambulisho muhimu na cha kudumu usoni mwangu, marehemu mzee Mpilipili alikuwa nao kama alfu tatu ama nne hivi waliomfanya kuwa miongoni mwa wafugaji wa nguvu sana wa kuku mitaa ya huko usambaani enzi hizoo.

Na wakawa ni kuku hawa hawa ambao stepu fulani wakapitiwa na kombora lililokuwa likijulikana enzi hizo kama kideri ama mdondo ambapo walianza kufa kwa mamia yao kama hawana akili nzuri vile.

Ikamlazimu Mzee Mpilipili kutoa ruksa ya kumshughulikia kuku yeyote aliyeonekana kusinzia sinzia kulikokuwa ndio dalili ya kupatwa na kideri. ruksa ikawa imepewa watu ambao hawapigiwi wanacheza, sembuse wakipigiwa. ikawa ni mauaji ya kimbari ya kuku.

Unaambiwa mambo yote yakawa ni kuku 24 hours. Tena bila mrija, mwanangu. asubuhi kuku kwa uji. mchana kuku kwa makande na usiku kuku kwa Bada. hujui bada? Pole. tafuta rafiki yako wa kisambaa akujuze. ndipo utakapojua kuwa kuna vitu vyeusi kabisa kuliko giza ulimwenguni humu!

Pamoja na yote hayo, bado mzee Mpilipili aliendelea kuwa na kawaida ya kutusisitizia kumuheshimu kuku na mnyama mwingine yoyote kwani kila mnyama alistahili heshima. kwamba hata kule kubeba mifupa iliyokwanguliwa vyema na vinjino vyetu na kwenda kuwaringishia watoto wenzetu haikuwa imetulia na ilikuwa ni sawa na kuchezea chakula.

Naam, ndivyo tulivyokuzwa na tukakua tukiamini kwamba kweli, kila kiumbe kilichoumbwa na Muumba kilistahili heshima hata kama kilikuwa ni kitoweo tu.

Kwa bahati mbaya kabisa, katika siku za karibuni ama kwa kisingizio cha siku zote cha kwenda na wakati ama kwa kukosa busara tu, muandika katikati ya misatri anashuhudia kile ambacho kwa mzee Mpilipili kisingekuwa pungufu ya kuchezea chakula.

Muandika katikati ya mistari anashitushwa na kushangazwa na tabia iliyoshika kasi ya kuku kugeuzwa kuwa ni kifaa cha michezo kama ilivyo kwa mpira ama nyavu za magoli. anashangaa kuona kila watu wanapokusanyika kwa sherehe hii ama ile, miongoni mwa michezo inayopewa chati kwa sana unakuwa ule kufukuza kuku!

Tena basi afadhali mchezo wenyewe ungekuwa unafanywa na na watoto wadogo, sivyo. muandika katikati ya mistari anaachwa hoi kabisa pale anaposhuhudia mijitu mizima na mavitambi yao, sijui akili, eti yakifukuzana na kuku!

Yaani kukimbia na gunia ama na chupa kichwani ama na kijiko chenye yai mdomoni sasa si michezo tosha tena hadi watu wazima na fahamu zao wamtese kuku kwa kumfukuza huku na huko na kumfanya atoe ulimi nje huku wafukuzaji na mavitambi yao wakihema na kutoa ulimi nje maradufu! kwa hakika ni bahati yao tu kuwa kile chama cha kutetea haki za wanyama sasa kimebaki herufi kubwa tu!

Marehemu mzee Mpilipili alikuwa hakopeshi kusema ni kuchezea chakula pale alipomuona mtu anaviringisha tonge zaidi ya mara tatu nne zilizotakiwa ili kuliweka katika hali nzuri ya kupita kooni. mi mwanayenaamini kuwa kufukuza kuku kama aina fulani ya mchezo hakuna tofauti yoyote na kuchezea chakula. nawakilisha.