...kuna haya maneno mawili ambayo matamshi yake yanasumbua sana wabongo. Ama wabongo ndio wanaopenda wenyewe kujisumbua...?
Lipo neno moja na herufi moja ambavyo kila mara muandika katikati ya mistari anaposikia yanavyotamkwa na wabongo wenzake walio wengi amekuwa akijiuliza mno juu ya umakini wetu katika lugha.
Ni neno na herufi ambavyo kukosewa kwake umakini katika kuyatamka hakuwezi kusingiziwa lafudhi ya kabila Fulani ama kisomo cha mtu.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba kukosa umakini katika kuyatamka maneno haya kunafanywa na kiila mtu ndani ya jamii hii ya wabongo. Kuanzia maprofesa hadi wauza gongo, walimu na wanafunzi wao na wanamuziki kwa wacheza ngoma.
Kwanza kuna hili neno ‘kudipu’ ambalo wengi wa watamkaji wake wanapolitamka wana maana ya neno ku’beep’, neno ambalo katika pekua pekua ya muandika katikati ya mistari kwenye makabrasha na madikishenari yake amekuta lina maana ya kutoa aina Fulani ya mlio.
Muandika katikati ya mistari amekuwa akisikia baadhi ya wabongo wenzake wakikazana kusema kwa uhakika kabisa ‘kudipu’ wakiwa na maana ya ‘kubeep’ ama ‘kubipu’ neno ambalo kwa tafsiri ya jamii ya wabongo lina maana ya kutaka kumtia demeji mwenzio wakati simu ulinunua mwenyewe.
Katika pekua pekua yake ndani ya makabrasha na madikishenari yake, muandika katikati ya mistari amejaribu kutafuta tafsiri ya neno dipu kwa maana ya ‘deep’ na anachopata ni kitu ambacho hakina uhusiano wowote na mambo ya kupiga simu.
Ndio, kwa mujibu wa makabrasha na madikishenari ya Chesi, neno ‘dipu’ linalotoholewa kutoka ‘deep’ kwa tafsiri hafifu na ya haraka haraka lina maana ya ndani, ndani zaidi ama kwenda ndani zaidi, mbali na maana nyingine kibao ambazo tukiamua kuziorodhesha zote, patakuwa hapatoshi hapa...
Kubwa ni kwamba katika maana zote za neno hili, muandika katikati hakuona hata inayoelekea kufanana fanana na mambo ya simu. Hii ina maana kwamba watu wanapokazania kusema ‘promota anadipu’ wanakuwa na maana ya kwamba promota ameingia ndani zaidi ama sijui vipi. Hata haiji.
Hapa muandika katikati ya mistari anawaomba wanajamii wenzake kukubaliana naye tu kwamba ni kuBeep ama ‘kubipu’ na sio ‘kuDipu’ ama kuDeep’. Unakwenda ndani zaidi wapi?
Halafu kuna hii herufi inayokanganya mno watu ya H. tayari nawasikia baadhi ya wanajamii wakiitamka kwa namna ile ile iliyo chanzo cha makala hii., ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’.
Muandika katikati ya mistari anakumbuka jinsi walimu wake wote wa Kiswahili aliopitia kuanzia chekechea ya shule ya vidudu ya kindergarten ya awali hadi alipofika pa kufika kimadarasa walivyokuwa wakimsisitizia kwamba herufi H ilikuwa inatamkwa ‘Echi’ na kamwe sio ‘Hechi’!
Anakumbuka jinsi baadhi ya walimu wake hao walivyofikia hatua ya kumtembezea fito makalioni ama kumgonga na rula kichwani hata pale ulimi wake ulipoteleza tu na kuitamka H kama 'Hechi' badala ya H, na kumuacha ajaze mwenyewe kwamba ulimi hauna mfupa.
Waama, kwa watembeza fito na wagonga rula vichwani hawa, yalikuwepo maneno mengi ambayo binadamu angeweza kukosea kuyatamka na kusingia ulimi wake kukosa mfupa lakini kamwe sio herufi H, maana hata kutamka 'Hechi' ama 'Echi' kwenyewe kulikuwa hakuhitaji matumizi ya ulimi kiasi hicho!
Ni kwa mantiki hii ndio maana muandika katikati ya mistari anashangazwa mno na idadi kubwa ya wanajamii ambao wanasikika wakitamka kwa mapana na marefu na bila wasiwasi wa aina yoyote herufi H kama ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’ huku wengi wakitamka hivyo wakiwa wameshiba kabisa ugali!
Muandika katikati ya mistari amekuwa kila apatapo nafasi akijaribu kurekebisha mapungufu haya akianzia na nyumbani kwake mwenyewe lakini haoni kama anapata mafanikio sana katika hili.
Hawasemi kwa mdomo lakini huwa anaona sura za watoto wake zikimuambia wazi kabisa kuwa aache fiksi, maana kama watangazaji wenye majina makubwa kabisa wa vituo vya Tiivii na redio wanatamka ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’, yeye ni nani hata awakosoe. Kama ni yeye anayekosea?
Naam, ndio maana hatuishi kusikia taarifa za habari za akina ‘hAli’ badala ya ‘Ali’ wanaosafiri hadi ‘Harusha’ badala ya Arusha kwenda kuongeza ‘Helimu’ badala ya Elimu! fikiria matamshi haya yanapotamkwa na mtu aliyetoka kushiba ugali na anatumia nguvu ya ugali huo kutamka hiyo 'Hechi'!
Huku mitaani anakopita ndio kabisaa hawamkopeshi. Wabishi wamekuwa wakimuuliza wazi kabisa kuwa tatizo ni nini, si mradi anaelewa? Hawataki kukubali kabisa kuwa tatizo sio kuelewa, bali ni kufuata kanuni.
Muandika katikati ya mistari hajakubali kushindwa na kamwe hatakubali ili tu yaishe. Na ndio maana anazidi kukandamiza. Kwa wale wote wanaosema ‘kudipu’ badala ya kubeep na ‘Hechi’ badala ya ‘Echi’…samahani Regina…Acheeni hizoo!
2 comments:
Muandika katika ya mistari nakubaliana na wewe kabisa
Lazima ucheke na hili jambo la kudipu.
Lakini pengine wanaathiriwa na lafudhi za lugha za majumbani kwao. Kwa sababu watu wengine hawawezi kusema neno "labda" wanasema "lamda" au "mtu" wanasema "ntu" au "afadhali" wanasema "asavali" Na ukiangalia sana utakuta ni watu wanaotokea sehemu chache tu za nchi.
Post a Comment