Wednesday, February 28, 2007

Tumeambiwa kuwa timu kabambe ya Real Madrid itakuja nchini na umati wa watu 80 na wanene wetu wametakiwa kujiandaa kutoa michango ili kufanikisha ujio wa miungu hao wadogo. Hili ndio tunalohitaji...??

Safari ya huyu mwanablogu mwenzenu ya kutafuta umaarufu, ujiko na ulaji kupitia soka, kandanda, kabumbu ama mpira wa miguu ilikatishwa rasmi alasiri ile ya tarehe ile ya 19 ya mwezi Juni mwaka wa 1975, miaka thelathini na mbili iliyopita.

Hii ndiyo siku ambayo goti lake lilivunjika na kubaki nyang’anyang’a wakati akiwa kwenye mechi ya michuano ya mabweni akiwa ‘nyoya’, jina walilobatizwa ma-form one wote, pale shule ya sekondari ya Musoma Alliance. Bila shaka Mwamoyo Hamza wa VOA bado anakumbuka hili maana yeye ndiye alikuwa nahodha wa bweni akiwa kidato cha sita.

Kwa shinikizo la wazazi, Ndugu na jamaa zake, mchezo wa soka ukawa kwake Kuanzia siku ile ukawa kama vile kibaka akionavyo kituo cha polisi. Kitu cha kupishia mbali kabisa kisichostahili kuguswa hata kwa upondo wa futi mia.

Mwanablogu mwenzenu huyu alijaribu kujiingiza kwenye michezo mingine kinyemela na kwa namna moja ama nyingine kufanikiwa kiasi cha kufikia hatua ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa mchezo wa handball mwaka 1981, lakini hiyo ni habari nyingine ambayo hatuna nafasi nayo hapa kwa leo.

Anachotaka kusema Chesi ni kwamba yeye ni mpenzi wa michezo ukiwemo huu wa mpira wa miguu lakini upenzi wake huu haujafikia pale baadhi ya watu wanapolazimisha kuwa ukiwa mpenzi wa mpira wa miguu hapa Bongo basi ni lazima uwe ama Jangwani ama Msimbazi.

Ndio, Chesi ni mpenzi wa soka kwa maana ya kwamba anapenda timu yoyote inayocheza soka la kufundishwa na kuvutia kama ilivyokuwa Ushirika ya Moshi na Coastal Union ya Tanga kwenye miaka ya katikati ya 80 ama Pamba ya Mwanza mwishoni mwa miaka hiyo ya themanini na ya Tisini mwanzoni.

Ukichukulia kwamba kwenye miaka hiyo hiyo huyu alikuwa tayari na eneo la kujidai kama hili lakini kwenye kurasa za michezo za gazeti la kiingereza la jumapili la siri-ukali, bila shaka anayo haki ya kuchangia jambo linalohusu michezo bila mtu kuibuka na kudai kuwa anaingia maeneo ya watu ya kujidai.

Haya, majuzi tumepokea taarifa kuwa katikati ya mwaka huu kutakuwa na ugeni mkuuubwa, kwa maana halisi, unaohusu mojawapo ya timu bora kabisa za kandanda ulimwenguni ya ‘kweli’ Madrid.

Tumeambiwa kuwa timu hiyo itawasili nchini na umati mkuuubwa wa watu themanini na tayari mipango inaandaliwa ya kuunda kamati ambayo pamoja na mambo mengi mengineyo itakuwa na kazi kubwa ya kukusanya masimbi kwa ajili ya kuukirimu ugeni huo mkubwa na kwa hakika, wa kutisha. Mtu themanini?

Mwanablogu anajua kabisa kwamba anatafuta kuzabwa vibao na watu huko manjiani maana kuna watu wakitaka lao jambo basi tena, huwa hawasikii la muadhini wala mshona kanzu!lakini anaamini kuwa kwa vile kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake ili mradi tu havunji sheria za nchi, anaomba kusema wazi kabisa. haifagilii ziara ya umati huo mkubwa wa watu. Angalau kwa wakati huu.

Chesi anadhani kuwa yapo mambo mengine kibao ambayo tunayo na hawa Billy Gates wetu wa kibongo wetu wanapaswa kupewa changamoto la kuyachangia na sio kuchangia ujio wa miungu wadogo hawa themanini katika medani ya soka.

Ndio, ni miungu wadogo katika medani ya soka na ndio maana ugeni wao mmoja unakuwa rundo la watu themanini. Hapana shaka kuwa ndani ya rundo kubwa hili la watu, kila galacha atakuja na mpishi wake, dakitari wake wa meno na pengine hata mrembeshaji wake!

Muandika katikati ya mistari hafagilii ziara ambayo tutalazimika kumlipa hata kinyozi ama mpiga kiwi viatu wa nyota wa timu hiyo.

Si hayo tu. Mchangia blogu mwenzenu huyu hataki ujio wa timu ambayo ana uhakika itamlazimu kutumia darubini kuwaona nyota wake maana mabaunsa wao watahakikisha kuwa akina Chesi watajuta na kuona ni afadhali vile wanavyowaona nyota hao kwenye tiivii maana angalau kuna wakati kamera zinawavuta karibu kiasi hata cha kuweza kuona hata machunusi yao!

Ndio, sana sana ukaribu mwingine tutakaowaona utakuwa ule wa kuwaona wakishikana mikono kusalimiana na wanene wa bongo ambao huwa hawapotezi nafasi yoyote ya kujipatia umaarufu hata kama ni wa bei ndogo namna gani!

Muandishi wa blogu huyu anahofia ugeni wa timu ya magalacha ambao unaweza ukaishia kwa wachezaji hao magalacha kucheza dakika mbili tu kisha wakatoka nje na kuwaacha watoto ama hata wapishi wao wakiwapelekesha puta wachezaji wetu wakati tumeishalipa kiingilio cha laki moja unusu ili kuwaona wao!

Kwa hakika, tunapaswa kujiuliza mno tutawalipa nini wachezaji ambao kwa wiki wanapokea mpaka shilingi milioni mia tatu, rudia tena, kwa wiki! Ni zahama gani hii tunayojitafutia? Kama ni kufungua tu uwanja si tushuke tu hapo bondeni kwa Ndugu zetu wa bafana? kwa nini tusiwaite ndugu zetu wa Naijeria ama Kameruni ama Ghana na kupanga kijiligi kidogo cha kufungulia uwanja wetu?

Mchangia Blogu anaanza kuuona ujio wa magalacha hawa kuwa kama sherehe za harusi za kibongo. Watu wanachanga malaki, siku ya harusi yenyewe wanaishia kupata shingo ya kuku aliyekonda na kijiwali ama tuchipsi tuwili halafu kesho yake hawana hata nauli ya daladala ya kuendea kazini huku maarusi wakiwa kwenye hoteli ya nyota tano wakijinafasi!

Muandika katikati hataki nchi yake njema ya bongo kuingizwa mjini potelea mbali kwamba tunao uzoefu wa kutosha tu wa kuingizwa ingizwa mjini.

2 comments:

Ndesanjo Macha said...

Mfano uliotumia wa michango ya harusi nakubaliana nao kuhusu hii timu ya Real.

Mfano wenyewe ni huu:

Mchangia Blogu anaanza kuuona ujio wa magalacha hawa kuwa kama sherehe za harusi za kibongo. Watu wanachanga malaki, siku ya harusi yenyewe wanaishia kupata shingo ya kuku aliyekonda na kijiwali ama tuchipsi tuwili halafu kesho yake hawana hata nauli ya daladala ya kuendea kazini huku maarusi wakiwa kwenye hoteli ya nyota tano wakijinafasi!

Chesi said...

asante, ndesanjo. nini maoni yako kuhusu ujio wa miungu hawa wa soka?
Habari za siku, mkuu?