Monday, July 10, 2006

Kuna utata juu ya kutumika ama kutotumika kwa kile kinachoitwa 'Tiba ya mkojo'. Haya ndiyo mawazo
yangu...!
!


Kuna mzee wangu mmoja wa kisambaa alipata kusema karne hizoo za zamani. Akili nyingi huondoa maarifa, bila shaka akimaanisha kwamba kuwa na akili ni kitu chema lakini ukizitumia vibaya ni hasara tupu.

Najua, kuna watu wamezaliwa na ubishi kisha wakachanjia ubishi ambao hapa wataanza kubishia kauli yangu hii na kuanza kunitaka nitoe ushahidi kwamba maneno hayo yalitamkwa na mzee fulani wa kisambaa. Salaam zao. Wao watoe ushahidi kwanza kwamba hayakutamkwa na mzee wangu mmoja wa kisambaa!

Haya, katika miaka hii ya karibuni mwandika katikati ya mistari amekuwa akishuhudia mambo kadhaa ambayo tunaweza tukakubaliana kuyachukulia kama ushahidi tosha wa kwamba mzee wangu wa kisambaa alikuwa ameona mbali na kwamba kweli akili nyingi huondoa maarifa.

Tuanze na huu mfano mmoja mkubwa. Karne kadhaa zilizopita, hawa watu weupe ambao kwa hakika ndio wanaotawala dunia ‘walivumbua’ mavazi na binadamu akaanza kuvaa nguo badala ya kuwa akitembea mambo hazalani, kama alivyokuwa akifanya kabla ya uzinduzi huo wa albam ya nguo!

Katika karne zilizofuata, binadamu weupe wakaendelea ‘kuvumbua’ aina mbali mbali za mitindo ya nguo. Kuanzia suti hadi kanzu hadi gauni hadi kaptura hadi pensi hadi sketi na kadhalika na kadhalika, yote ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa binadamu anajisetiri kwa namna mbali mbali huku akipendeza.

Inaelekea kuwa akili za kuvumbua zikazidi na miaka machache tu iliyopita, baadhi ya weupe hawa ‘wakavumbua’ kuwa kumbe kuvaa nguo sio mali kitu tena na kulikuwa na burudani zaidi katika kutembea mambo hazalani kama karne zilee za kiza kabla nguo hazijavumbuliwa!

Ndio maana katika baadhi ya nchi zinazosemekana kuwa ni za walioendelea, kuna maeneo ambayo yametengwa maalumu kwa ajili ya wadau ‘waliovumbua’ kuwa kuna wakati binadamu anapaswa kuweka minguo yake kando na kuishi kama alivyozaliwa. Mambo hazalani!

Yaani wewe ukiishafika maeneno hayo basi sarawili yako, sijui suti yako ama gauni lako unalichojoa na viambatanishi vyote ulivyonavyo mwilini unaweka kando na kuanza kuvinjari ukiwa kama ulivyoingia duniani. Mambo hazalani!

Tena basi unaambiwa unashauriwa kabisa kuwa ukitaka kutinga maeneo hayo basi ni vema uende na mkeo, mkweo na vitukutu vyenu pengine katika jitihada za wanaosimamia maeneo hayo kuhakikisha kuwa macho balbu yako yanaishia kwa uliye naye na sio kwa wa wenzako!

Muandika katikati ya mistari ana kawaida ya kujifagilia mno kuwa akili zake ziko dakika tatu mbele, lakini hapa ameinua mikono juu. Ameshindwa kabisa kuingiza kichwani mwake picha ya yeye akiwa na mkewe, vitukutu vyao na mkw…..stafirulahi, mungu apishe mbali!

Muandika katikati ya mistari ana matumaini kuwa ‘akili nyingi’ hizi za ‘kuvumbua’ maisha bila nguo hazitapata wadau wengi hapa nchini ingawaje nyakati kadhaa anapoangalia kilichovaliwa na baadhi ya mabinti zetu anajikuta akajiuliza iwapo kweli hatupo tayari kwenye maeneo ya watembea uchi!

Yapo mengi. Kuna wakati pia ‘akili nyingi’ za hawa ndugu zetu weupe zilipata kutuambia kuwa ngoma zetu za kunengua viuno ni za kishenzi na kwamba binadamu mstaarabu ni yule tu anayecheza ‘ngoma’ zao za kistaarabu kama Tango, Waltz, Rumba na nini tena sijui.

Akili nyingi huondoa maarifa. Katika miaka ya karibuni tunashuhudia wasanii wa kizungu ‘wakivumbua’ kukatika na kunengua viuno kwenye video zao sio tu kama hawana akili nzuri bali pia kwa namna ambayo hata wanasindimba wetu hawaoni ndani..

Yapo mengi ya kudhibitisha kuwa kweli akili nyingi huondoa maarifa, lakini kiboko ni hili lililotuzukia katika miaka ya hivi karibuni la watu ‘kuvumbua’ kunywa…ashakum, mikojo yao wenyewe kwa kisingizio kwamba ati ni tiba!

Ndio, tunaambiwa na ‘wavumbuzi’ hawa wenye ‘akili nyingi’ kwamba ati iwapo mtu unataka mwili wako usiandamwe andamwe na magonjwa ya kiajabu ajabu na pia usizeeke haraka basi ulitakiwa kunywa glasi moja ya mkojo wako mwenyewe kila siku asubuhi.

Tukaambiwa pia kuwa kama kulikuwa na dawa bora kabisa ambayo ilikuwa na uwezo wa kutibu magonjwa sugu kibao tu yakiwemo yale yaliyowashindwa waganga wengine basi ilikuwa ni mkojo wako mwenyewe. Glasi moja iliyojaa mkojo kila siku asubuhi basi wee mambo yako swafi tu! Ukitoka hapo unaenda kumbusu mshikaki wako, raha tupu!

Katika kuhalalisha kwao hili, wadau hawa wa tiba ya mkojo wakanukuu hata maneno ya vitabu vitakatifu vya dini yasemayo ‘unywe maji kutoka birika lako mwenyewe’ na kujaribu kutushawishi kwamba yalikuwa na maana ya kumtaka mtu kunywa mkojo wake mwenyewe! Tumbaku kabisa!

Wadau hawa wanatuambia kuwa mkojo unapotoka mwilini unatoka na chembechembe za madini fulani ambayo yana faida kubwa mwilini. Swali la Chesi ni kuwa kama yana faida kubwa mwilini kwa nini yatolewe kupitia mkojo? Si ina maana madini hayo yamejaa tele mwilini ndio maana ziada yake inaondolewa kupitia mkojo??

Kwa vile kuna watu hawakawiagi kutupa ngumi, mwandika katikati ya mistari anaomba kuharakisha kusema kabisa kuwa hapa hapingi haki ya mtu kunywa mkojo wake mwenyewe. Na anywe tani yake maana kila mtu ana Uhuru wa kufanya anavyotaka mradi tu havunji sheria na hili ninaamini kwamba halijawekewa sheria ingawaje limeishapiga hodi kwa waheshimiwa pale Domdom na limeishatolewa tamko.

Labda tu hapa tuombe kutungiwa sheria ya kuzuia mtu kunywa limkojo lake na kisha kwenda kumbusu mwandani wake bila kumtahadharisha kwanza kuwa asubuhi alikuwa amepiga glasi moja ya mkojo na hivyo kumpa nafasi mwandani wake huyo ya kuamua mwenyewe kama aendelee na busu hilo ama la!

Ufahamu mdogo alionao chesi kuhusu mwili wake unamuambia kuwa mkojo ni njia maalumu iliyowekwa na Muumba kwa ajili ya mwili kutoa takataka zake za majimaji, full stop. hakuna cha madini wala nini. ni uchafu tu!

Ni kichekesho cha karne basi mwili ukusanye takataka zake za majimaji na kuzitoa mwilini halafu sisi kutokana na akili zetu nyingi kuzidi maarifa tukinge glasi zetu na kuurudisha tena mwilini kupitia mdomoni!

Kuna wakati mpaka muandika katikati ya mistari akawaza kimzaha kuwa isije ikawa jamaa walisikia kuwa tunakunywa 'mkojo wa punda' kama dawa ya kikohozi basi wakashawishika kudhani kuwa kama tunaweza kunywa mkojo wa punda basi wakituchomekea kunywa wa binadamu itakuwa ni kwa kwenda mbele!

Mwandika katikati ya mistari anaanza kuhofu pia kuwa iwapo leo tunakubali akili zetu nyingi zilizozidi maarifa zitushawishi kurudisha mkojo mwilini, basi kesho itakuwa ni jasho, kesho kutwa makamasi na mtondogoo ni mambo makubwa zaidi yanayotolewa mwilini mwetu kama uchafu!

Kumrandhi kwa kukuchefua, mdau wa eneo hili lakini huku ndiko tunakojilengesha maana kama alivyobainisha mzee wangu mmoja wa kisambaa (acha ubishi!), akili nyingi huondoa maarifa. Alamsik
kombe la dunia lina kasheshe zake. hususani kwa akina siye tunaolicheza kwa mdomo....

Kwa muda wa wiki mbili sasa, hii sehemu ambayo muandika katikati ya mistari haoni hata aibu ya kuiita ati sebule yake, imekuwa ni kijiwe ama kongamano la makocha, wachambuzi, wachambaji wataalamu na wataaluma wa soka ambao uchambuzi wao kuhusu mechi za kombe la dunia umemfanya Chizi kujiuliza kila mara watu hawa wanangoja nini hapa bongo!

Ndio, ni wataalamu na wataaluma mno wa soka kiasi kwamba nina hakika kabisa kuwa iwapo watajisumbua kidogo tu kuandika barua za maombi ya ukocha pale jiji la Manchester, basi kibarua cha mtafuna Big G mmoja aitwaye Sir Alex Ferguson kitaota magugu! hakya nani tena vile!

Halafu nimegundua pia mara nyingi kwamba utaalamu na utaaluma wa soka wa waheshimiwa hawa walio marafiki, majirani na ndugu zangu wanaokuja kukodolea macho haka katiivii kangu ka nchi kumi na mbili, huongezeka maradufu pale bi mkubwa wa nyumba na wadogo zake kadhaa wa kike wanapojiunga kuwa miongoni mwa watazamaji wa mechi husika. hapo tena, hakuna anayekubali kushindwa!

Nikagundua pia kuwa wengi wa waataluma na wataalamu wangu hawa wa soka la sebuleni walikuwa hawakuwahi kucheza japo chandimu utotoni mwao afadhali hata mimi ambaye niliishakipiga hadi ngani ya unahodha wa timu yetu ya darasa la tano mwaka 1972 pale Chang'ombe shule ya msingi!!

Naam, kwa hakika ni maoni ya wataaluma na wataalamu hawa wa kibongo yanayonifanya niamini kwamba ninachotizama sebuleni kwangu sio kombe la dunia bali soka la sebuleni la kimataifa!

Kwa mfano, kuna huyu mmoja ambaye ana shahada ya juu ya ukocha wa kuwakosoa wachezajiwa timu zinazocheza uwanjani: "Ayaa! mwangalie sasa yule migulu baja anakopeleka mpira! pale alitakiwa arudishe mpira nyuma kwa mwanangu mwenyewe Figo ama atie majalo kwa mzee mzima nanihii apige bao, badala yake anacheza mdundiko na mpira! mwangalie kwanza, jibukta kubwa kaa kisafleti!"

Ama: "Tatizo hawa Uingereza hawaijui hii infomesheni ya 3-5-2, sana sana wanalazimisha tu! pale yule Cole alitakiwa apande (sio mchicha, ndugu msomaji!) halafu huyu Ferdinand ashuke chini kama Libero, lakini waapi! ubishololo na baraka ya kuvaa mijikaptura mireeefu tu!"

Halafu yupo huyu mtaalamu mwenye shahada ya juu ya ukocha wa kuwakosoa makocha wenzake wa kombe la dunia...na hali yeye ni kocha wa sebuleni kwa chesi tu!! "Ama huyu kocha wa Uruguay ndio amepanga timu gani sasa hii! hawa lazima leo wapigwe bao tu! pale alitakiwa amtoe yule namba kumi na moja ambae anazunguka tu uwanjani kaa daladala na sio amtoe yule namba tisa ambaye mambo makubwa yake tunayaona! mii nakwambia hawa makoccha wengine basi tu! muone kwanza, suruali kaa yangu!!"

Alikuwepo pia mkereketwa mmoja aliyekuwa akiiona Ghana kama ni mkoa wa.. waaa... wa..ah, sijui wa ngapi vile wa bongo; "Angalieni wanaume hao! mi nakwambieni hawa ndio mabingwa wapya wa dunia mwaka huu! Si unaona mwenyewe alivyomtungua bao mbili kwa gurudumu yule mcheki?

Yatosha tu kusema kwamba baada ya Ghana kufungishwa virago, mkereketwa huyu hatukumuona tena kwenye uwanja wetu wa sebuleni na kwa kweli tukaukosa mno utaalamu wake mkubwa katika soka la kimataifa, hususani ilipokuja suala la 'mkoa' wake wa Ghana!

Alikuwepo pia huyu bwana mdogo wangu mmoja ambaye yeye alikuwa na kazi moja tu ya kufananisha mambo: "Ebwanaee! umecheki darizi lile la mzee Patrick Viera! Duh! yaani kama lile lile alilofanya yule nanihii wa wekundu wa Msimbazi kwenye ile mechi kati ya nanihii na nanihii pale uwanja wa taifa!"

Au: "Duh! Ebwanaee! hii midfield ya Ureno mwanangu sio mchezo! inagawa mavyumba na mapande kama anavyogawaga Nanihino wa Wanjano wa Jangwani! yaani, wee acha tu!"

Step fulani bwana mdogo wangu huyu katika kujaribu kwake kujijazia maujiko kwa mabinti zangu, akajaribu hata kufananisha viwanja: "Dah! lile jukwaa la uwanja wa Munich sio mchezo, mwanangu mwenyewe! Yaani, dah! kaa lile dude letu la Kirumba!"

Kauli hii ikaufanya uzalendo wa watazamaji walio wengi uyeyuke. wakamtaka bwaa mdogo wangu yule afunge bakuli lake, ama aende akalale na awaachie watu waangalie mpira. akakubali kufunga bakuli. nahisi alikuwa hana hata kitanda.

Alikuwepo pia mtaalamu wa kukandya: "Mii nawaambia hizi timu nyingine sijui hata zinafikaje kwenye fainali hizi, kama sio kubebwa tu! mtu utafungwaje gongo sita, bwana? ee? mtu utafungwaje gongo sita kaa umesimama! mi nawaambia hata taifa stars yetu ingepeta kichizi kwenye fainali hizi!"

Hata hivyo mtaaluma huyu akashindwa kutufafanulia ni kwa vipi basi hio Taifa stars yetu haijafanikiwa hata kunusa tu huko kwenye watu wanaopigwa gongo sita kaa wamesimama, na hali yenyewe ingepeta tu kwa sana!

Kipindi fulani, hata huyu bi mkubwa wa nyumba naye pia akataka kuonyesha kwamba hayuko nyuma katika mambo ya kandanda na kwamba akiamua kujisumbua kidogo tu kwenda Uingereza kutafuta kazi ya ukocha, kibarua cha mfaransa Arsene Wenge kitaota mbawa: "Yule kocha naye mbona amezubaa hivyo, kaa mkono wa kanzu! si anatakiwa awaambie wachezaji wake kwamba kila pale mwenzao anapopiga penati(akimaanisha kona!) wao waende wakamvamie kipa na kumsukuma ili wafunge goli!"

Ni ajabu kwamba pamoja na wataalamu na wataaluma kibao wa soka waliojazana sebuleni mwangu mule hakuna hata mmoja aliyediriki kuinua mdomo wake na kumsahihisha bi mkubwa wa nyumba kwamba kilichokuwa kikipigwa ni kona na wala sio penati! hakukuwa na mwenye jeuri hio.

Kiboko cha wote hata hivyo alikuwa huyu lastborn wangu wa miaka saba, mheshimiwa sana Desi. wakati wenzake tukiendelea kuangalia mpira yeye alikuwa akiendelea na michezo yake mingine. pale goli lilipoingia ndipo alipokuja mbio na kutaka kujua...ni rangi gani ambayo imefunga!

Naam, yeye alichokuwa anamaindi ni rangi tu, hayo mambo ya sijui Ghana, sijui Brazili ama Uingereza ama Trinidadi na Tumbaku alituachia tujaze wenyewe!!

Yote kwa yote, katika kipindi hiki kigumu ambacho kila kitu kimepanda bei, wataalamu na wataaluma hawa wa soka la kimataifa , kupitia tiivii ya nchi kumi na mbili iliyo kwenye sebule langu, wananipa angalau sababu ya kutabasamu!! jumapili njema ya kushabikia wenzetu!