Kuna utata juu ya kutumika ama kutotumika kwa kile kinachoitwa 'Tiba ya mkojo'. Haya ndiyo mawazo
yangu...!!
Kuna mzee wangu mmoja wa kisambaa alipata kusema karne hizoo za zamani. Akili nyingi huondoa maarifa, bila shaka akimaanisha kwamba kuwa na akili ni kitu chema lakini ukizitumia vibaya ni hasara tupu.
Najua, kuna watu wamezaliwa na ubishi kisha wakachanjia ubishi ambao hapa wataanza kubishia kauli yangu hii na kuanza kunitaka nitoe ushahidi kwamba maneno hayo yalitamkwa na mzee fulani wa kisambaa. Salaam zao. Wao watoe ushahidi kwanza kwamba hayakutamkwa na mzee wangu mmoja wa kisambaa!
Haya, katika miaka hii ya karibuni mwandika katikati ya mistari amekuwa akishuhudia mambo kadhaa ambayo tunaweza tukakubaliana kuyachukulia kama ushahidi tosha wa kwamba mzee wangu wa kisambaa alikuwa ameona mbali na kwamba kweli akili nyingi huondoa maarifa.
Tuanze na huu mfano mmoja mkubwa. Karne kadhaa zilizopita, hawa watu weupe ambao kwa hakika ndio wanaotawala dunia ‘walivumbua’ mavazi na binadamu akaanza kuvaa nguo badala ya kuwa akitembea mambo hazalani, kama alivyokuwa akifanya kabla ya uzinduzi huo wa albam ya nguo!
Katika karne zilizofuata, binadamu weupe wakaendelea ‘kuvumbua’ aina mbali mbali za mitindo ya nguo. Kuanzia suti hadi kanzu hadi gauni hadi kaptura hadi pensi hadi sketi na kadhalika na kadhalika, yote ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa binadamu anajisetiri kwa namna mbali mbali huku akipendeza.
Inaelekea kuwa akili za kuvumbua zikazidi na miaka machache tu iliyopita, baadhi ya weupe hawa ‘wakavumbua’ kuwa kumbe kuvaa nguo sio mali kitu tena na kulikuwa na burudani zaidi katika kutembea mambo hazalani kama karne zilee za kiza kabla nguo hazijavumbuliwa!
Ndio maana katika baadhi ya nchi zinazosemekana kuwa ni za walioendelea, kuna maeneo ambayo yametengwa maalumu kwa ajili ya wadau ‘waliovumbua’ kuwa kuna wakati binadamu anapaswa kuweka minguo yake kando na kuishi kama alivyozaliwa. Mambo hazalani!
Yaani wewe ukiishafika maeneno hayo basi sarawili yako, sijui suti yako ama gauni lako unalichojoa na viambatanishi vyote ulivyonavyo mwilini unaweka kando na kuanza kuvinjari ukiwa kama ulivyoingia duniani. Mambo hazalani!
Tena basi unaambiwa unashauriwa kabisa kuwa ukitaka kutinga maeneo hayo basi ni vema uende na mkeo, mkweo na vitukutu vyenu pengine katika jitihada za wanaosimamia maeneo hayo kuhakikisha kuwa macho balbu yako yanaishia kwa uliye naye na sio kwa wa wenzako!
Muandika katikati ya mistari ana kawaida ya kujifagilia mno kuwa akili zake ziko dakika tatu mbele, lakini hapa ameinua mikono juu. Ameshindwa kabisa kuingiza kichwani mwake picha ya yeye akiwa na mkewe, vitukutu vyao na mkw…..stafirulahi, mungu apishe mbali!
Muandika katikati ya mistari ana matumaini kuwa ‘akili nyingi’ hizi za ‘kuvumbua’ maisha bila nguo hazitapata wadau wengi hapa nchini ingawaje nyakati kadhaa anapoangalia kilichovaliwa na baadhi ya mabinti zetu anajikuta akajiuliza iwapo kweli hatupo tayari kwenye maeneo ya watembea uchi!
Yapo mengi. Kuna wakati pia ‘akili nyingi’ za hawa ndugu zetu weupe zilipata kutuambia kuwa ngoma zetu za kunengua viuno ni za kishenzi na kwamba binadamu mstaarabu ni yule tu anayecheza ‘ngoma’ zao za kistaarabu kama Tango, Waltz, Rumba na nini tena sijui.
Akili nyingi huondoa maarifa. Katika miaka ya karibuni tunashuhudia wasanii wa kizungu ‘wakivumbua’ kukatika na kunengua viuno kwenye video zao sio tu kama hawana akili nzuri bali pia kwa namna ambayo hata wanasindimba wetu hawaoni ndani..
Yapo mengi ya kudhibitisha kuwa kweli akili nyingi huondoa maarifa, lakini kiboko ni hili lililotuzukia katika miaka ya hivi karibuni la watu ‘kuvumbua’ kunywa…ashakum, mikojo yao wenyewe kwa kisingizio kwamba ati ni tiba!
Ndio, tunaambiwa na ‘wavumbuzi’ hawa wenye ‘akili nyingi’ kwamba ati iwapo mtu unataka mwili wako usiandamwe andamwe na magonjwa ya kiajabu ajabu na pia usizeeke haraka basi ulitakiwa kunywa glasi moja ya mkojo wako mwenyewe kila siku asubuhi.
Tukaambiwa pia kuwa kama kulikuwa na dawa bora kabisa ambayo ilikuwa na uwezo wa kutibu magonjwa sugu kibao tu yakiwemo yale yaliyowashindwa waganga wengine basi ilikuwa ni mkojo wako mwenyewe. Glasi moja iliyojaa mkojo kila siku asubuhi basi wee mambo yako swafi tu! Ukitoka hapo unaenda kumbusu mshikaki wako, raha tupu!
Katika kuhalalisha kwao hili, wadau hawa wa tiba ya mkojo wakanukuu hata maneno ya vitabu vitakatifu vya dini yasemayo ‘unywe maji kutoka birika lako mwenyewe’ na kujaribu kutushawishi kwamba yalikuwa na maana ya kumtaka mtu kunywa mkojo wake mwenyewe! Tumbaku kabisa!
Wadau hawa wanatuambia kuwa mkojo unapotoka mwilini unatoka na chembechembe za madini fulani ambayo yana faida kubwa mwilini. Swali la Chesi ni kuwa kama yana faida kubwa mwilini kwa nini yatolewe kupitia mkojo? Si ina maana madini hayo yamejaa tele mwilini ndio maana ziada yake inaondolewa kupitia mkojo??
Kwa vile kuna watu hawakawiagi kutupa ngumi, mwandika katikati ya mistari anaomba kuharakisha kusema kabisa kuwa hapa hapingi haki ya mtu kunywa mkojo wake mwenyewe. Na anywe tani yake maana kila mtu ana Uhuru wa kufanya anavyotaka mradi tu havunji sheria na hili ninaamini kwamba halijawekewa sheria ingawaje limeishapiga hodi kwa waheshimiwa pale Domdom na limeishatolewa tamko.
Labda tu hapa tuombe kutungiwa sheria ya kuzuia mtu kunywa limkojo lake na kisha kwenda kumbusu mwandani wake bila kumtahadharisha kwanza kuwa asubuhi alikuwa amepiga glasi moja ya mkojo na hivyo kumpa nafasi mwandani wake huyo ya kuamua mwenyewe kama aendelee na busu hilo ama la!
Ufahamu mdogo alionao chesi kuhusu mwili wake unamuambia kuwa mkojo ni njia maalumu iliyowekwa na Muumba kwa ajili ya mwili kutoa takataka zake za majimaji, full stop. hakuna cha madini wala nini. ni uchafu tu!
Ni kichekesho cha karne basi mwili ukusanye takataka zake za majimaji na kuzitoa mwilini halafu sisi kutokana na akili zetu nyingi kuzidi maarifa tukinge glasi zetu na kuurudisha tena mwilini kupitia mdomoni!
Kuna wakati mpaka muandika katikati ya mistari akawaza kimzaha kuwa isije ikawa jamaa walisikia kuwa tunakunywa 'mkojo wa punda' kama dawa ya kikohozi basi wakashawishika kudhani kuwa kama tunaweza kunywa mkojo wa punda basi wakituchomekea kunywa wa binadamu itakuwa ni kwa kwenda mbele!
Mwandika katikati ya mistari anaanza kuhofu pia kuwa iwapo leo tunakubali akili zetu nyingi zilizozidi maarifa zitushawishi kurudisha mkojo mwilini, basi kesho itakuwa ni jasho, kesho kutwa makamasi na mtondogoo ni mambo makubwa zaidi yanayotolewa mwilini mwetu kama uchafu!
Kumrandhi kwa kukuchefua, mdau wa eneo hili lakini huku ndiko tunakojilengesha maana kama alivyobainisha mzee wangu mmoja wa kisambaa (acha ubishi!), akili nyingi huondoa maarifa. Alamsik
1 comment:
Uko likizo sio? Lakini umepotea kidogo. Tunahitaji makala ili tucheke huku tukitafakari.
Post a Comment