Thursday, November 09, 2006

Hii makala yangu kuhusu katuni ya waandishi wa habari wa Bongo kumlamba miguu mheshimiwa ilikuwa itoke kwenye
kolamu yangu ya gazeti la kila jumapili. haikutoka
.

Aha, mkuki kwa kitimoto hai, sio...?


Kiasi cha wiki mbili hivi zilizopita, vyombo vya habari vya nchi njema ya Bongo hususani magazeti, viliibua kinachoweza kuitwa kuwa ni 'tufani ndani ya kikombe cha chai' kuhusiana na kibonzo kilichokuwa kimechorwa kwenye gazeti moja la jumapili la nchi jirani ya Kenya.

Kibonzo hicho kilikuwa kinaonyesha waliolezwa kuwa ni waandishi wa habari wa Bongo wakifanya kile mchoraji alichoona ni kama kumlamba miguu, kumtetemekea na kujigonga gonga kwa mheshimiwa wa awamu ya ari, nguvu na kasi mpya, JK.

Kupitia mchoro wake, mchoraji wa kibonzo ambaye kama kumbukumbu za muandika katikati ya mistari hazijaathirika sana na masika 47 ambazo ameishanyeshewa mpaka leo hii, ni mbongo mwenzetu anayefanya kazi huko kitambo sasa, ametumia uhuru na haki yake kuonyesha kile anachodhani kuwa kinaendelea katika medani ya uandishi wa habari hapa Bongo.

Inaelekea kibonzo kile kiliwakera mno wanahabari wa nchi njema ya Bongo ambao kila mara wamekuwa msitari wa mbele kudai haki na uhuru wa mtu kutoa na kupokea habari bila kuingiliwa na mtu alimradi tu havunji sheria za nchi.

Wakamuibukia mchora kibonzo husika na kwa kutumia silaha zao kali kabisa zisizo Patriot wala Mig wala AK 47 bali kalamu zao, kukemea, kuasa, kumuonya na kumtaka mchora katuni huyo aachane nao na ashike lake. Kwamba medani ya uandishi wa habari hapa Bongo ilikuwa na kanuni zake ambazo kufanya kazi kwa kumfurahisha mtu kamwe hakukuwa moja ya kanuni hizo!

Naam, baadhi ya makala zikawa na muelekeo wa wanahabari wetu kumwaga mboga kwa vile mchora kibonzo husika alikuwa amemwaga ugali. kwamba mchora katuni anaona ajabu gani waandishi wa habari wa Bongo kulamba miguu ya watawala wakati wao walikuwa wanfanya hayo hayo. ndio, yale yale ya shughuli afanye bata, akifanya kuku inakuwa balaa.

Step fulani, mtaaluma anayesimamia masuala ya habari kwenye ofisi ya mheshimiwa wa kasi, nguvu na ari mpya naye pia akatia timu kwenye sakata hilo kwa kutamka kuwa jumba jeupe lililoko Magogoni lilikuwa halijafurahishwa sana na katuni hiyo, lakini hata hivyo wasingeijibu mapigo.

Kidoogo hapa muandika katikati ya mistari akatatizika. hivi mtaaluma huyu anayesimamia habari pale Ikulu alikuwa akitegemea mchora katuni wa nchi jirani achore katuni kwa ajili ya kuifurahisha Ikulu ya Bongo? hivi mtaaluma alikuwa na maana kuwa kigezo cha kuchora katuni kwa nchi jirani kilikuwa ni katuni hiyo kuifurahisha ama kutoifurahisha Ikulu ya Dizim?

Waama, ilisisimua mno kuona vyombo hivi vya habari vya nchi njema ya Bongo ambavyo vinakuwaga mstari wa mbele kutetea uhuru wa mtu kutoa na kupokea habari bila kuingiliwa na mtu vikizusha 'tufani ndani ya kikombe cha chai' dhidi ya mwenzao aliyetumia uhuru wake wa kutoa na kupokea habari bila kuingiliwa na mtu!

Kilichomtatiza zaidi muandika katikati ya mistari ni kuona kuwa katika nyingi ya makala za ukali zilizoandikwa dhidi ya kibonzo husika, nyingi zililenga zaidi kujikosha jinsi taaluma ya habari ya Bongo inavyofanya kazi kwa kanuni zake badala ya kujibu hoja ya katuni ya kama waandishi wa habari wa Bongo walikuwa wanafanya kazi kwa muelekeo wa kumlamba na kujigongagonga kwa mheshimiwa ama la!

Ndio, muandika katikati ya mistari hakumbuki kusoma makala iliyokiri kwa uwazi kabisa bila kumung'unya maneno kwamba ndio, wapo baadhi ya waandishi na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vinafanya kazi kwa namna ambayo ingebidi mtu ujilazimishe sana kuamini kwamba sio kujigonga gonga kwa waheshimiwa wa kasi, ari na nguvu mpya!

Kwamba baadhi ya makala zilizokuwa zikiandikwa magazetini na baadhi ya waandishi kuhusiana na mheshimiwa zilikuwa ni pungufu kidogo tu ya barua za maombi ya kazi kutoka kwa waandishi husika kwenda kwa mheshimiwa na ofisi yake!

Kwa mawazo ya muandika katikati ya mistari, hili ndio lilikuwa la kujadili. sio lile la 'mbona wao wanafanya hivyo hivyo'. Hivi mtu akikuambia kuwa umeshika kinyesi unakimbilia kumjibu kuwa 'mbona wewe umeshika!', ama unakimbilia kunawa mkono na kumuacha yeye akiendelea kushika kinyesi!

Muandika katikati ya mistari anaamini kuwa suala la vyombo vya habari kufagilia na kujigongagonga kwa watawala ni suala ambalo limekuwepo tangia Adamu. kwa maana hiyo hakukuwa na haja ya watu kutoana macho. badaala yake, anaamini kuwa yapo mambo kadhaa ambayo watu wanaweza kuyafanya na yakapunguza kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari kuonekana vinalamba miguu ya watawala.

Wakati zogo hilo la 'wanamlamba ama hawamlambi miguu' likiendelea, tukaanza kushuhudia baadhi ya waandishi na vyombo vya habari vikiibatiza jina timu yetu ya mpira wa miguu, Taifa Stars,kutokana na mafanikio iliyokuwa ikiendelea kuyapata kwenye michuano, jina la 'JK Eleven'!

Muandika katikati ya mistari amejikuta akiiangalia ile katuni iliyowafanya watu wateme cheche na kisha kuwaza juu ya muandishi wa habari anayeamka asubuhi na kuamua mwenyewe kuwa kuanzia siku hiyo timu ya taifa itakuwa sio Taifa Stars tena bali 'JK Eleven'

Maana, kwa mtazamo wa kawaida kabisa muandika katikati ya mistari alidhani kuwa jambo kubwa na muhimu kama la kuipa jina jipya timu yetu ya mpira wa miguu, kama kuna ulazima wa kufanya hivyo, lilifaa kujadiliwa kwanza na wadau wa eneo husika na kisha wote kwa ujumla wetu tukafikia muafaka wa kuibalisha jina timu yetu ya Taifa.

Muandika katikati ya mistari hapingi mheshimiwa wetu kupendwa mno kiasi cha baadhi ya watu kuona ipo haja ya kuibatiza tinu yetu ya taifa jina lake. hata hivyo anaona picha inayokuja huko mbele iwapo kila mara tutapenda kubadili majina ya vitu kutokana na watawala waliopo madarakani wakati husika.

Anaona baada ya miaka kumi timu ya taifa ikibadilishwa jina na kuitwa 'CM Eleven' kwa tu vile raisi wa nchi wa wakati huo, mheshimiwa sana Chesi Mpilipili atakuwa ameinunulia jezi na baada ya miaka kumi mingine timu itabadilishwa jina na kuitwa 'DM Eleven' kwa vile raisi wa wakati huo Mtukufu sana Desi Mpilipili atakayekuwa amemrithi baba yake naye atakuwa ameinunulia mipira!

Waandishi wetu wana haki ya kuhoji mchora vibonzo wa nchi jirani kuwachora kuwa wanalamba miguu ya watawala. na wao basi angalau wajitahidi tahidi wasimpe mtu sababu ya kufanya hivyo. alamsik.

3 comments:

Ndesanjo Macha said...

Kwanini makala hii haikutoka? Mbona hakuna baya ulilosema? Napenda unavyoandika kwa kejeli fulani ingawa unaongelea mambo mazito.

Chesi said...

hata sina hakika kwanini haikutoka...pengine ndio ushahidi kamili wa alichokuwa amechora Gado. tunapenda mno kiasi cha kutokubali tunachopenda kikakosolewa......

Ndesanjo Macha said...

Umepotelea wapi?