wapo wanasi-hasa wengi tu wakibongo ambao wakiisha wekewa maikrofoni mbele ya midomo yao, basi. kwao, time inakuwa sio money tena...!
siku ya May Day mheshimiwa aliliona hili na kwa vile yeye huwa hakopeshagi, akalizungumzia kwa kuwaambia wanasi-hasa hawa.....
‘Sio lazima kila mtu aongee, jamani'...!
Naam, siku ile ya jumatatu ya wiki hii ambayo ilikuwa ni siku ya watumwa duniani, nikawa nimekaa mbele ya kijiredio changu cha mwaka 47 ili kusikiliza kile ambacho mkuu wa nchi alikuwa anataka kukisema.
Naomba kwanza nisisitize kusema kwamba sina kawaida ya kusikiliza redio kwa mantiki kwamba kuna faida gani kutumia masikio peke yake kusikiliza kitu ambacho Kumbe unaweza pia kukiona kwa macho kupitia kwenye kioo a.k.a tiivii.
Kwa Bahati mbaya, safari hii vituo vyote vya tiivii vikawa havina mpango wa kuonyesha live kile kilichokuwa kikiendelea Shinyanga, mji ambao tangia muandika katikati ya mistari alipouondoka mwaka 1977 akiwa denti wa pale Shaibushi ni kama alikung’uta mavumbi, chembilecho vitabu vya dini, maana mpaka leo hii hajaingiza mguu tena!
Haya basi, ili kupata live hotuba ya mheshimiwa tukalazimika kukumbuka viredio vyetu ambavyo wengine tuliisha vifungasha zamani tukingoja mtu anayekwenda kijijini awapelekee ndugu na jamaa zetu nao wajidai. ganda la muwa la jana ni kivuno kwa chungu.
Kama nilivyokwisha sema. Sina kawaida ya kusikiliza redio hasa ukichukulia kuwa nyingi ya redio zetu zinazosikika vyema siku hizi ni madebe masaa ishirini na tano. Kilichonisukuma kusikiliza redio siku ile ilikuwa ni kutaka tu kujua iwapo iwapo Mheshimiwa ataongeza chochote kitu kwenye masihara yetu ya mshahara, basi.
Nikanunua betri mpya na kisha nikakaa kusikiliza kilichokuwa kikiendelea kule Shinyanga. Waheshimiwa wakaanza kukaribishana jukwaani kuhutubia kwa staili yao ile ile ya miaka nenda rudi tangia mwaka 47aa ambayo sio ngeni sana kwetu…
Mheshimiwa huyu anamkaribisha yule ili amkaribishe huyo ambaye atamkaribisha huyu ambaye atashukuru kwa kupewa nafasi ya kumkaribisha huyu ambaye atazungumza maneno machache (yanayoishia kuwa rundo!) ya kumkaribisha yule ambaye atamkaribisha wa kumkaribisha huyu, ilimradi Kizunguzungu kitupu!
Ni kwa utaratibu huu ndio maana masaa kadhaa baadaye, muandika katikati ya mistari akawa hajamsikia yule ambaye alikuwa amemfanya aibue kiredio chake huko kilikokuwa na anunue betri mpya ili kumsikiliza.
Mwandika katikati ya mistari akajiuliza iwapo waheshimiwa wale waliokuwa wakiendelea kupokezana vijiti vya kukaribishana walikuwa kweli hawafahamu kuwa watu walikuwa wamejaa uwanjani pale kumsikiliza mheshimiwa na sio mtu mwingine yoyote.
kwamba wengine, kama huyu Chizi, walikuwa wamelazimika hata kuibua viredio vyao vya zamani kutoka walikokuwa wamevichimbia ili tu kusikia live kitakachosemwa na Mheshimiwa badala ya kutegemea RedioMbao FM!
Kwa hakika, muandika katikati ya mistari hakuona umuhimu wa kuanza kusomeshwa historia ya vyama vya wafanyakazi pale maana ameishahudhuria siku za wafanyakazi kama thelathini mfululizo kwa kwenda nyuma na kila siku yanayosemwa ni yale yale tu na anaweza kuyakariri hata kwa kinyume nyume!
Haya, unaambiwa stepu fulani pia tukachomekewa ratiba ya kuzawadia wanamichezo. Mwandika katikati ya mistari akajiuliza mno. Ile ilikuwa ni sikukuu ya wafanyakazi, wafukuza upepo na wacheza mpira walikuwa wapi na wapi pale, potelea mbali kwamba nao pia walikuwa wafanyakazi!
Ndio, kwa nini zawadi zao kwa washindi zisingekabidhiwa jana yake na siku ile wakatuacha tuendelee na programu nyingine? Ina maana tulitakiwa tutegemee sasa kwamba siku ya kuzawadia wanamichezo bora wa mwaka basi watazawadiwa pia dakitari bora wa mwaka, mwalimu bora wa mwaka na pengine hata mpiga debe bora wa mwaka?
Jamani wabongo, mbona tunapenda kuchanganya mambo hivi? Si ndio haya haya ya ile shughuli ya klabu bingwa ya warembo nchini kuchukua zaidi ya masaa matano hadi saba na pengine mpaka alfajiri wakati ile ya dunia inachukua masaa mawili tu?
Hatimaaaaaye, wakati huyu muandika katikati ya mistari akiwa ameishaanza kusinzia kwenye kochi ndipo watu wakakumbuka kuwa ala, Kumbe Mheshimiwa naye anatakiwa kuhutubia na hivyo kumualika jukwaani.
Nnachompendea huyu Mheshimiwa ni kutokukopesha maneno. Utafikiri ni mdau wa ‘katikati ya mistari’. Bila kuuma uma maneno cha kwanza alichotamka kikawa kile kile kilichokuwa kichwani mwa Chizi, kwamba siri moja ya shughuli kama zile ilikuwa ni ile ya kuamua kuwa sio lazima kila mtu azungumze!
Kwamba kulikuwa hakuna ulazima wowote wa kusoma kila salamu iliyotumwa kuanzia mwanzo hadi mwisho kwani ingetosha tu kusema kuwa tumepokea salamu kutoka kwa huyu na huyu na yule basi, bila kuanza kuzisoma zote! Makofi, tafadhali!
Kwamba hatari kuu ya kutaka kila mtu jukwaani azungumze ilikuwa ni ile ya kujikuta waheshimiwa mlioko jukwaani mko peke yenu na mnahutubiana wenyewe kwa wenyewe maana kila mwananchi ameishachoka na kuishia zake.
Kwa kifupi kabisa, ujumbe wa Mheshimiwa kwa waheshimiwa wale ulikuwa ni kukumbuka kuwa ‘time is money’. Kwamba kulikuwa kuna taratibu nyingine ambazo kwa hakika kwa karne tuliyonayo hazikuwa za lazima sana kuzifanya.
Kama tumemualika Mheshimiwa kuhutubia May day, basi na tumpe nafasi ya kufanya hivyo. salamu kibao na kuwazawadia wanariadha kwanza nako kunatoka wapi. Time is money, jamani.
1 comment:
Hawa jamaa wanapenda "air time" na ndio maana hata maswali yao bungeni mengine wala hayana maana...
Post a Comment