'Nyungo' mbili kubwa zilizo kichwani mwa huyu muandika katikati ya mistari ambazo pia hujulikana kama masikio zimedaka taarifa muhimu kuhusu wafanya biashara wa nchi njema ya Bongo ambazo zimemsisimua mno mmiliki wa 'nyungo' hizo.
Hizi ni zile taarifa zilizotangazwa majuzi na waheshimiwa wetu kuwa kuanzia tarehe fulani huko mbele wafanya biashara ‘waaminifu’ wataruhusiwa kupitisha mzigo yao pale bandarini chap chap bila kukaguliwa, wakauze wanachouza kisha baadae wao wenyewe waseme walipitisha nini na wanapaswa kulipa nini!
Yapo mambo ambayo muandika katikati ya mistari husisimka mno anapoyasikia.Hili ni mojawapo. Hii ni pamoja na kujijazia maujiko kila mara kwamba ngozi yake imeshakuwa sugu na politiki za nchi njema ya bongo kiasi kwamba hakuna kinachoweza kumsisimua tena kutoka kwa wanene wa nchi.
Kwamba ati kuanzia tarehe fulani huko mbele ya safari wanaosemekana kuwa wafanya biashara waaminifu wa Bongo wataruhusiwa kupitisha bandarini chap chap lumbesa, magunia, maboksi, matenga na makontena yao bila kuulizwa na mtu kilichomo.
Kwamba baada ya kupitisha mizigo yao bila kulazimika kueleza kilichomo wataenda kuuza kilichomo kisha watarudi kunako husika na kulipa wanachotakiwa kulipa kutokana na walichouza!
Wafanya biashara waaminifu! Kwanza muandika katikati ya mistari anashituka na kushangaa kuwa maneno haya mawili ‘wafanya biashara waaminifu’ bado yapo kwenye msamiati wa lugha yetu njema ya Kiswahili. Wafanya biashara waaminifu! Bongo hii??
Muandika katikati ya mistari anapata tabu mno kuamini kuwa ndani ya Bongo yetu njema hii katika karne hii bado kuna kabila la watu linaloitwa ‘wafanya biashara waaminifu’. Kwa hakika, ni wale wenye roho ya Paka tu, ambao wanaweza kuamini uwepo wa kabila hilo!
Kwamba bado tunao wafanya biashara ambao ni waaminifu vya kutosha kiasi kwamba tunaweza kuwaruhusu kupitisha vijikontena vyao viwili vitatu bila kulazimika kutuambia kilichomo, wakaenda kuuza kisha wakarudi na kutuambia wameuza nini na kulipa wanachopaswa kulipa kama kodi kutokana na mauzo yao!
Kuna mtu mahali anataka kufanya mzaha mbaya. Huu wa kuwaruhusu wafanya biashara wanaosemekana kuwa ni waaminifu kupitisha mizigo bandarini bila kukaguliwa, wakauze kisha ndipo warudi kulipa kodi inayotakiwa ni mzaha mbaya hata kwa nchi iliyobobea katika mizaha kama Bongo!
Muandika katikati ya mistari anajiuliza mno iwapo hapa waheshimiwa walikuwa wanazungumzia Mitume ama Watawa fulani hivi ama tulikuwa tunazungumzia wafanya biashara dizaini ya Rada ama wale wa mashine za umeme za kufua giza badala ya kufua mwanga!
Wafanyabiashara waaminifu? Wepi? Hawa tusioisha kuwasoma kwenye magazeti wakikopeshana na kuchezea akiba ya uzeeni ya Chesi kwa kununua, kukarabati na kisha kuyapiga bei mbaya magofu kadha wa kadha huku Chesi mwenye akiba yake akikosa hata haki tu ya kukopa akiba yake mwenyewe!
Ndio, wafanya biashara waaminifu wepi? Hawa hawa wanaopita mlango wa nyuma kupewa mikopo inayogeuka makopo ya chooni baada ya siagi iliyokuwemo kuliwa?
Kwa hakika, muandika katikati ya mistari anasubiri kwa hamu mno kutangazwa kwa vigezo vya mfanyabiashara muaminifu ili na yeye atie timu na kuuagiza kijikontena chake chenye vijenereta alfu mbili ambavyo kutokana na sifa ya uaminifu, vitapita pale bandarini chap chap bila kukaguliwa!
Ni utume na utawa, ambao hana, ama uwendawazimu tu utakaomfanya Chesi arudi kunakohusika baada ya mauzo yake na kwa akili zake timamu kabisa aseme kweli kwamba kijikontena chake kilikuwa na vijenereta alfu mbili na kodi yake hii hapa!
Bongo haiishiwi na mapya yanayokufanya ujiulize mara mbili mbili juu ya utashi wa baadhi ya watu. Hili ni mojawapo. Tutafakari.