Friday, May 05, 2006

chesimpilipili

hii niliiandika wakati nchi yetu njema ya Bongo inatimiza miaka 41 tangia tupate uhuru......


tuwaite, waje kuona ... ?

Mwandika hekaya alikuwa dogo wa miaka kumi na mbili tu na akisoma darasa la nne hapo katika shule ya msingi ya Chang'ombe wakati nchi njema hii ya bongo ikisherehekea miaka kumi ya uhuru wake pale mwaka na 1971.

Anakumbuka mno jinsi yeye binafsi alivyoshiriki kikamilifu katika sherehe hizo kwa kuwa miongoni mwa mamia ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za jiji jema la Dizim walioshiriki katika maonyesho kabambe ya halaiki yaliyofanyika pale uwanja wa taifa.

Naam, maonyesho ya halaiki ambayo mpaka leo hii wachokozi wa mambo bado wanakubaliana kwamba hayajapata kutokea tena mfano wake, pengine kutokana na ukweli kwamba ilifundishwa na waalimu wa kichina orijino kutoka china!

Haya, mwandika hekaya pia anakumbuka mno nyimbo kadhaa za muziki wa dansi zilizotungwa na wasanii wetu kwa ajili ya kipindi cha sherehe hizo.

Anakumbuka mno ule wa bendi marehemu ya Urafiki jazz, wakati huo ikiongozwa na mzee Mrisho, Ngulimba wa Ngulimba, wimbo ambao pamoja na mambo mengine, ulielezea mafanikio yaliyokuwa yamepatikana katika kipindi hicho cha miaka kumi ya uhuru.

Ikatajwa reli ya Tazara, chuo chetu kikuu, vyama vyetu vya ushirika, jeshi letu la mgambo( wakati huo likiwa jeshi la mgambo kweli na sio haya masulupwete tunayoshuhudia siku hizi!) na hata kisomo cha watu wazima kikatajwa kama moja ya mafanikio yetu!

Haya, mwandika hekaya pia akakumbuka mwimbo mwingine uliokuwa umeimbwa na hayati Mbaraka Mwishehe Mwaruka ambao ulielezea jinsi wakoloni walivyokuwa wametuchelewesha na hatua ambayo tulikuwa tumeifikia baada ya wao kung'atuka.

Lakini, zaidi mno muandishi wa hekaya anakumbuka mno wimbo ulioimbwa na Nuta jazz, kama hajakosea sana, ambao maneno yake anayakumbuka vizuri mpaka leo hii:

'sasa tutawaita waje kuona wenyewe,

hatutafanya kitu tukashindwa,

sasa tutawaita waje kuona wenyewe,

maendeleo yetu yanakwenda vyema....'



Naam, mwandika hekaya hana uhakika sawa sawa, lakini anadhani kwamba maneno ya wimbo huu yalikuwa yametokana na hotuba moja ya raisi wa nchi wa wakati huo, mwalimu Julius Nyerere, ambapo alikuwa amesema kwamba tungewaita wale waliotutawala waje kuona tulipokuwa tumefika katika kipindi cha miaka kumi.

Na kwa hakika wakati huo tulikuwa kweli na jeuri ya kuweza kuwaita waliotutawala na kudai kwamba tulikuwa bado kustahili uhuru, waje kuona mambo makubwa tuliyokuwa tumefanya katika kipindi hicho cha miaka kumi. ndio, tulikuwa na jeuri hio!

Ukiachilia mbali mambo makubwa kama yale ya ujenzi wa chuo kikuu, viwanda kama kile cha nguo cha Urafiki,na Mwatex na cha zana za kilimo cha Ufi na kadhalika na kadhalika, nchi hii ilikuwa imepiga hatua kubwa mno katika huduma za jamii.

Huyu muandishi wa hekaya anakumbuka mno kwamba katika kipindi hicho alikuwa akiishi na shemeji yake mmoja pale Chang'ombe mtaa wa Ngorogoro nyumba namba 98, na anakumbuka mno pia kwamba hakupata kushuhudia kitu kinachoitwa kukatika umeme ama maji kukatika kwa siku tatu nzima, never!

Kila mara muandika hekaya anapowahadithia haya wanawe, huishia kuona huruma jinsi wanawe wanavyobaki kung'aa macho kutoana na mshangao kwa vile wao katika kipindi hiki cha mgawo, umeme huja saa tano usiku na 'kuondoka'
saa kumi na mbili alfajiri!

Anakumbuka pia mno jinsi mitaa ya Magomeni, Ilala na kwingineko ilivyokuwa misafi ikiwa na lami, mbali na kila nyumba kuwa na pipa lake la takataka ambalo lilikuwa likija kuchukuliwa takataka zake na gari la site kila baada ya siku mbili!

Siku hizi ukiweka pipa la taka nje kesho hulikuti maana unakuwa umewapa watu kifaa cha kuhifadhia maji kutokana na maji kuwa ya mgawo!

Na hapa chesi anaogopa hata kudokeza kwamba yeye alisoma darasa la pili hadi la sita katika shule hio ya msingi ya Chang'ombe akiwa amekalia dawati lake la mtu mmoja mmoja tu, sio watatu, kwa kuchelea kwamba watu hawatamuamini, kwa vile hata watoto ake tu wanadhani anayowaambia ni fiksi zake tu!

Ni wazi basi kwamba baada ya wabongo walio wengi kushuhudia mafanikio haya ya miaka kumi, walitegemea kwamba hadi nchi hii itakapofikia miaka thelathini ama arobaini ya uhuru, ingekuwa pungufu kidogo tu ya peponi! ole wao. ole wetu.

Muandika hekaya angependa kuwahoji wabongo wenzake. ni kweli kwamba katika kipindi hiki wakati nchi njema ya bongo inasherehekea kutimiza miaka arobaini na moja ya uhuru wake, tunayo jeuri ya kuwaita waliotutawala waje kuona mafanikio yetu, kama alivyofanya baba wa Taifa wakati wa kusherehekea miaka kumi ya uhuru wetu mwaka na 1971??

Tuwaite? waje kuona nini? barabara za katikati ya jiji walizoziacha na lami na ambazo sasa baada ya miaka 40 ya Uhuru ni vumbi tupu, hata zile za kwao akina chesi kule Bumbuli zina nafuu?

Waje kuona nini? bomba kuu kukuu la kuleta maji jijini ambalo toka waondoke wao hakuna mtu ambaye ameishapata angalau kuwaza kutafuta vyanzo vingine vya maji badala ya waheshimiwa kila mara kujazana mahali bomba linapopasuka na kuahidi wananchi kwamba maji yatatoka baada ya siku mbili tatu!!

Tuwaite waje kuona nini? hospitali zisizokuwa na dawa? shule zisizokuwa na madawati? nyumba za watumishi wa serikali walizoziacha ambazo sasa kwa kisingizio cha sirikali kushindwa kuzimeintein, sasa zinapigwa bei kama nguo za mitumbani?

Mwandika hekaya anaweza kuandika mengi lakini lililo wazi ni kwamba, pamoja na kwamba kuna watu watabisha, yeye haoni kama tunao ubavu wa kuwaita walee waliotuwala ili waje kuona maendeleo yetu baada ya miaka AROBAINI NA MOJA ya uhuru wetu! alamsik.

No comments: