Friday, May 05, 2006

chesimpilipili

Wakati kheshimiwa mpya wa Bongo alipotimiza siku mia moja ofisini, kila mtu aliandika makala. mimi niliamua kungoja hadi siku kumi baadaya ndio nikaandika hii niliyoiita...

Siku 110 ofisini...!



Alhamisi ileee, kama siku hivi kumi zilizopita, wakati hii awamu ya nne ya uongozi wa nchi njema ya Bongo inatimiza siku mia moja, tulishuhudia jinsi kila aliyekuwa anajua kuandika alivyochongoa kalamu yake na kuchonga.

Napenda kuamini kuwa maneno haya ni ya kistaarabu zaidi kuliko kama ningesema kuwa kila mwenye mdomo aliuchongoa na kuchonga.

Naam, siku ile ya Alhamisi wakati awamu ya nne ya uongozi inatimiza siku mia moja ofisini kila mwenye kalamu yake aliishika na kuandika kile alichoamini kuwa ni bonge ya makala.

Zilikuwa makala za kusisimua mno kiasi kwamba ungedhani watu wanasherehekea kutimiza miaka mia moja ya uongozi na kumbe ni SIKU mia moja tu!

Mwandika katikati ya mistari hataki kuamini kwamba siku mia moja zinatosha katika kukupa muelekeo wa jambo fulani.

Pengine ndio maana akaamua kuacha kitim tim cha kuandika kuhusu siku mia moja kitulie kwanza ndipo na yeye atie neno lake. maana wote tungeandika wakati ule sijui nani angemsoma mwenziwe.

Kikubwa alichogundua mwandika katikati ya mistari katika kitim tim kile ni kuwa nchi njema ya Bongo haina uhaba wa wafagiliaji na eeee, kidedea.

Wapo wa kumwaga. kulikuwa na makala nyingi zaidi za kufagilia kuliko zilizokuwa na alama za kuuliza.

Si nia ya muandika katikati ya mistari kuingilia uhuru wa mtu kutoa maoni yake. na ndio maana hata yeye hategemei mtu kuanza kumuona kuwa si mwenzetu kwa vile tu makala yake itakuwa imejaa maswali mengi zaidi kuliko mafagio. ndio, wenzake weengi wameishafagilia. yeye anaomba kuzungumzia zaidi upande wa pili wa gwala.

Haya, siku mia na kumi. kikubwa alichoona huyu last born wa marehemu mzee Mpilipili katika kipindi hiki cha siku mia moja na kumi ni maagizo, maelekezo na maonyo meengi ambayo wakati fulani yalianza kumfanya aone kama tulikuwa tumerudi tulikotoka. maagizo na maelekezo kibao yaliyokuwa na muelekeo wa kuishia kuwa hivyo hivyo, maagizo na maelekezo tu.

Anadhani kwamba waheshimiwa wa awamu ya nne walikuwa wanaenda kasi mno kiasi cha kutuacha sisi wengine wote nyuma. waama, Chesi anadhani kwamba sio vibaya iwapo waheshimiwa hawa wakasimama kidogo kutusubiri na pia kufuatilia kama yale maagizo na maelekezo yote wanayotoa huku nyuma yanatekelezwa.

Kuna hili la sirikali kuanza na migulu baja kwenye suala kubwa la kubana matumizi yake. tumeshuhudia tumizi kubwa la waheshimiwa walioteuliwa kuja Dizim na kuishi kwenye hoteli za bei mbaya wakisubiri nyumba, ushahidi kamili kwamba uamuzi wa kuuza nyumba za taifa kwa watu wawili watatu ni mchemsho wa karne, ingawaje nafasi bado ipo ya kulirekebisha hili kwa kurudisha nyumba zile kwa wananchi na kuwarudishia chao waliozinunua.

Basi waheshimiwa wenyewe waje peke yao, aa wapi. wengine walikuja na wake zao, na watoto wao na labda hata vijukuu na hivyo badala ya mheshimiwa kuchukua chumba kimoja tu katika hoteli ya bei mbaya, anachukua vitatu. cha kwake na mamaaa, cha watoto na sebule, maana wageni anaomtembelea mhishimiwa hawawezi wakaingia chumbani kwake moja kwa moja wasije wakaona deshi deshi zake zimeanikwa kwenye tendegu la kitanda!

Naam, hii ni tofauti iliyoje na pale huyu Chesi alipohamishiwa Darisalama mara ya kwanza miaka hiyoo ya 47 ambapo ili kubana matumizi alilazimika kutangulia yeye na bi mkubwa kwanza na kuishi kwenye kijigesti fulani cha uchochoroni hadi pale alipopata makazi ndipo aliporusu umati wake wote kutia timu jijini!

Muandika katikati ya mistari anatamani mno kuwa badala ya kugharamiwa na sirikali, kila mmoja katika waheshimiwa hawa angekatiwa kabisa posho yake ya safari na manaiti yake kama anavyofanyiwa yeye anapobahatisha kwenda safari, kisha tuone. thubutu kama mtu angekaa kwenye hoteli ya bei mbaya na kadamnasi yake!

Haya, katika siku mia moja na kumi tumemsikia pia mheshimiwa wetu akitamka bayana kuwa ana majina ya wala rushwa wote lakini anawapa muda kwanza ili kujirekebisha. hii ni kauli iliyomkumbusha sana mwandika katikati ya mstari juu ya kauli fulani ya hapo zamani za kale juu ya kwamba wala rushwa wote wangekiona cha mtema kuni lakini baadaye ikabadilika na kuwa ya kutaka ushahidi kwanza kabla ya cha mtema kuni!

Hawa watu wameishaitafuna sana kama mchwa nchi yetu njema hii ya Bongo. kuwapa tena muda wamalizie malizie kuitafuna haimuingii akilini muandika katikati ya mistari. hawa kwa hakika ni watu waliostahili kufanyiziwa kwa kasi ile ile iliyotumika kuwatoa mkuku wagonga kokoto kule kwenye machimbo yao ama wenye vibanda vyao katikati ya jiji. staili ya hakuna cha mswalie mtume!

Ndio, ili kuepusha kuonekana ni ' yale yale', kasi mpya inapaswa kuwa ni upanga wenye makali ya kukata kote kote badala ya kuwa na ukali wa ajabu pale tu inapokuwa ni suala la kuvunja vibanda vya Big Brother Manzese, lakini inapokuwa ni suala la kukata manyangumi na mapapa wala rushwa ghafla unakuwa butu na kuanza kusua sua!

Katika siku mia moja na kumi hizi pia tukaambiwa kukaa standby kusikiliza orodha ya majina ya wale walioaminika kuwa ni majambazi makubwa. muandika katikati ya mistari na walala hoi wenzake wakakaa mkao wa kula wakisubiri mijina mikubwa mikubwa ya mijambazi iliyokuwa inaivuruga Bongo yetu njema hii.

Jiji jema la Dizim likatangaza kile kilichosemekana kwamba ni majina ya mijambazi mikubwa mikubwa na muandika katikati ya mistari akajikuta akishindwa kuzua muayo wake. hakuna jina lolote lililoshitua mtu na kwa hakika muandika katikati ya mistari hatashangaa sana iwapo miongoni mwa orodha ile kutakuwa na wauza karanga wawili watatu. Hivi watu wanajua maana ya majambazi wakubwa kweli?

Ni kweli, yalikuwepo majina mawili matatu yaliyoshitua watu kiasi fulani lakini watajwa walipofikishwa mahakamani wakiwa wametinga magold na masuti yao huku wakitabasamu muandika katikati ya mistari akakata tamaa na kuona kama ni aina fulani ya mchezo wa kuigiza hasa pale anapokumbuka kuwa wadogo zake wanapofikishwa 'kaunta' (kama unadhani ni ya Bar, pole!) huamrishwa kuvua kila kinachoweza kuvuliwa, na kama huna bahati hata nywele!

Hapo hapo kwenye orodha ya majina tukaambiwa kuwa tungetajiwa pia orodha ya majina ya askari wa vyeo vya juu ambao walikuwa wakishirikiana na majambazi. tukasubiri, tukasubiri, tukasubiri wee. wakatajwa wawili watatu wenye vyeo ambavyo sio kitu cha kuandikia barua nyumbani kisha, kimya.
habari iliyokuwa ukurasa wa mbele sasa imeishia kuwa ya ukurasa wa matangazo...!

Ni mambo kama haya ambayo yanamfanya muandika katikati ya mistari aombe kwanza kuweka fagio lake mfukoni. ni mpaka hapo atakapoona mtu mzima ananyolewa nywele kwa kigae cha chupa ndipo labda, laabda atalitoa na kufagilia mtu. Asalaam aleikum.

2 comments:

Jeff Msangi said...

Makala safi kabisa hii Chesi.Tujifunze kusifia vitendo na sio maneno.

boniphace said...

Chsei makala hizi zatakiwa sana ewe mpita katikati ya maanishi safi sana kupita pia katikati ya hoja na kufunua mambo kuliko kukimbilia mbali na kuimba mapambio na njuga tu.