Thursday, April 27, 2006

chesimpilipili

kuna hii ambayo inawahusu hawa waheshimiwa wanaotutunzia vi-akiba vyetu vya uzeeni......




Kwa hesabu za haraka haraka, huyu mwanaGlobu mpya atatimiza birthday yake ya sitini mnamo mwaka 2019, miaka michache sana kumi na mbili tu ijayo.

Huo ndio mwaka ambao hawa watu wanaomtunzia vijisenti vyake vya uzeeni wamemuambia kwamba ndio ataweza kuchukua kilicho chake, kwa maana ya hatimaye kulia kivulini baada ya miaka kibao ya kuchumia juani.

Kwa jinsi kazi ya kuuza kila kilicho chetu ilivyoshika kasi na hao wanaovinunua wanavyotustaafisha kushoto, kulia na katikati kama vile hawana akili nzuri, Chesi ana uhakika kwamba kufikia mwaka huo wa 2019 yeye atakuwa aliishastaafishwa kazi miaka miaka kumi na nne kabla, yaani mwaka 2008.

Atakuwa ameachishwa kazi mwaka huo wa 2008 akiwa dogo wa miaka 49 tu, lakini kutokana na hii sheria ambayo kwa hakika inaweza kupitishwa nchi kama ya bongo tu, atakuwa amezuiwa kuchukua chake ati mpaka afikishe miaka sitini, yaani huoo mwaka wa 2019! mungu wangu!

Ndio, kwa hakika hii ni sheria ambayo inaweza ikapitishwa nchi kama ya bongo tu! yaani mtu ufanye kazi miaka thelathini, ustaafishwe ukiwa na miaka hamsini halafu mtu akuambie huwezi kuchukua akiba yako mpaka utakapofikisha miaka sitini!

MwanaGlobu anajiuliza kama sheria hii ingepitishwa iwapo hawa walioipitisha nao wangeambiwa hawawezi kuvuta kiinua mgongo chao cha milioni thelathini na kitu,(baada ya 'kufanya kazi' kwa miaka mitano tu) hadi pale na wao watakapofikisha miaka 60, hapana,80, kutokana na ukweli kwamba wengi wao tayari wako kwenye anga za miaka 60!!!

Thubutu kama sheria hii ingeona jua la nje!

Haya, kwa rehema za Mungu huyu mwanaGlobu anafanikiwa kufikisha miaka yake sitini. bila shaka atakuwa amejichimbia huko kwao Bumbuli, kutokana na ukweli kwamba baada ya kustaafishwa kazi, hakuwa na jeuri yoyote ya kuendelea kubanana hapa hapa mjini kama wenzake!

Atafikisha miaka yake sitini na atajikongoja kutoka huko kwao na kuliingia jiji la Dizim la mwaka 2019. labda wakati huo stend ya mabasi itakuwa Kibaha. Pengine pale mtaa wa Samora jengo fupi kuliko yote litakuwa la tughorofa thelathini. mengine yote yatakuwa mawinguni.

Anaweza pia akakuta hata ile sanamu ya askari pale imebinafsishwa na mwekezaji kuamua kuivunja na kuweka kijifast food cha nguvu katikati ya ule mzunguko! hakuna kisichowezekana Bongo.

Na ni kutokana na wingi wa majengo mareeeefu, ndio maana pengine Chesi atapata tabu sana kulipata jengo ambalo lilikuwa ndio makao makuu ya shirika ambalo lilikuwa linamtunzia visenti vyake hadi atakapofikisha miaka 60.

Ni hatimaye sana, na baada ya kuzunguka mno ndipo pengine Chesi atabahatisha kuliona jengo hilo nje kabisa ya mji likiwa na tugorofa thelathini tu! bila shaka nje ya mji wakati huo itakuwa kibaha maili moja!

Ataingia mapokezi na kumkuta huyu binti ambaye bila shaka bibi yake mzaa mama alifanya kazi na chesi miaka hio, sio ofisi moja bali kwa rika.

Na kwa vile pengine enzi hizo watu watakuwa bize sana zaidi ya ilivyo sasa, binti yule hatapoteza muda kumuamkia kizee Chesi na moja kwa moja: "sema shida yako, wee mzee!"

Chesi ataeleza shida yake, kwamba amekuja kuchukua masimbi yake kwa vile amefikisha miaka sitini. binti atamuelekeza chesi kwa ofisi husika. atamuelekeza, huku macho yake 'yakiuliza' wazi kabisa inakuwaje mpaka siku ile chesi awe bado anapeta tu wakati vizee vyenzake vimeishauona ufalme wa mbingu kitambo!

Haya, chesi anapanda gorofa ya kumi na saba kwa muhusika ambaye anamuelekeza gorofa ya tatu kwa muhusika ambaye anamuelekeza gorofa ya saba kwa nuhusika ambaye anamuelekeza gorofa ya kumi na nane kwa muhusika mwingine na mwingine tena. mpaka hapa, mambo kwa Babu Chesi ni kizunguzungu kitupu!

Hatimaaaye, anampata huyu muhusika ambaye anamfahamisha Babu Chesi kwamba Ofisi yake haina kumbukumbu zozote zinazohusu kampuni aliyokuwa akidundia mzigo chesi, hivyo... chesi alie tu....! na labda miaka hio msemo utakuwa....chesi acheke tu!

Na kweli, chesi anatamani kulia na kucheka kwa pamoja. Yaani baada ya kusubiri kwa miaka kumi na tatu mizima baada ya kustaafu, leo hii anaambiwa hana chake!kwa hakika ni jambo la kushukuru kwamba haanguki na kufaint na kufariki pale pale kutokana na mshituko!

Huyu mhusika wa mwisho angalau anaonyesha kutaka kumsaidia chesi kadri ya uwezo wake,hususani baada ya kutamka kwamba "alaa! kumbe wewe ndio mzee chesi mpilipili! mama huwa ananihadithia kwamba alipokuwa kijana alikuwa akipenda sana kusoma makala za mwindishi mmoja aliyekuwa akiitwa chesi mpilipili! kumbe ndio weewee!"

Kijana yule anamsaidia chesi kwa kupanda gorofa hili na kushukia lile, kuingia ofisi hii na kutokea ile na kufungua disketi hii na CD ile, lakini waaapi. mwisho wa yote hakuna rekodi yoyote inayopatikana kuonyesha kwamba chesi anapaswa kulipwa masimbi yake wakati atakapofikisha miaka sitini!

"unajua, mzee chesi, hapa katikati tumehama hama sana kiasi kwamba bila shaka baadhi ya nyaraka zetu zitakuwa zimemisiplesiwa na tarakilishi zetu zimekrashi !"

"eniwei, wee njoo tena baada ya miezi sita na nitaangalia ni vipi!ninaweza kukusaidia! napenda kukufahamisha pia kwamba mama atafurahi sana leo nikimfahamisha kwamba nimekutana na mzee chesi!" kijana anatoa tamati na mchezo unaishia hapo.

chesi anaondoka jijini kipara na kurudi kijijini Bumbuli akiwa amezeeka ghafla na kuonekana ni kizee wa miaka 85 badala ya 60 aliyonayo. anazeeka zaidi anapokumbuka kwamba kijijini aliondoka kwa mkwara mzito kwamba atakaporudi kutoka mjini, watu watajua yeye ni nani!

Naam, ni kwa mlolongo huu wa mawazo ndio maana chesi anadhani kwamba anapostaafishwa ni afadhali akamilishiwe chake kabisa aangaze mbele, na kama kuna kasoro katika rekodi zake, aweze kuzishughulikia akiwa bado na nguvu zake.

Ndio, hii 'bahati nasibu' ya kusubiri hadi afikishe miaka sitini, potelea mbali kwamba ni hapo kwenye kona tu, ndipo aambiwe ahana chake yeye haafikiani nayo.

vinginevyo, hata wale walioipitisha sheria hii ya ajabu nao wanapomaliza miaka yao mitano ya kudunda mzigo, waambiwe kiinua mgongo cha cha milionizao 30 watalipwa pale watakapofikisha miaka 80, kwa mantiki ile ile kwamba wengi wao tayari wapo kwenye anga za miaka 60, tuone kama watakubali! nawakilisha.

Tuesday, April 25, 2006

chesimpilipili

Kuna hii ya majina yetu kwanza....


Wiki kama mbili tatu hivi nyuma, huyu mwandika katikati ya mistari alipata bahati ya kuhudhuria kijikongamano fulani hivi kuhusu mawasiliano kilichofanyika kwenye kijihoteli flani cha kitalii (wapi kwingine!) cha bei mbaya katikati ya jiji jema hili la Mzee Makamba la Dizim.

Mwandika katikati ya mistari bado anaamini kwamba kuteuliwa kwake na wahusika kuhudhuria kijisemina hicho kulitokana na ukweli kwamba kijiposho kilichokuwa kinatolewa kwenye kijikongamano hichi kilikuwa ni kijiposho mbuzi. kingekuwa beberu mwandika katikati ya mistari angeisikilizia kwenye bomba!

Ndio, unategemea nini kwa nchi ambayo kwenye kongamano la wasioona nje ya nchi inawakilishwa na wanaoona wengi kuliko wasioona.

Mwasikia sana? kabla ya kijikongamano hicho kuanza rasmi, washiriki tukatakiwa kuandika majina yetu, ya kwanza, ili yakatengenezewe beji ambazo tungetakiwa kuzivaa katika kipindi choote cha kijikongamano hicho kwa kile tulichoambiwa kuwa ni kurahisisha mawasiliano kati ya washiriki na watoa mada wazungu.

Basi bwana, huyu muandika hekaya akaandikisha jina lake la Mpilipili akiamini kwamba lilikuwa linajulikana zaidi kuliko lile la Chizi, mbali ya ile mantiki pana zaidi kwamba sisi wabantu tuna kawaida ya kujuana kwa majina ya ukoo zaidi kuliko yake 'kuazima' kutoka kwa wazungu na waarabu!

Akaja huyu mweupe mmoja mtayarishaji wa kijikongamano hicho na kuwasisitizia washiriki wote, lakini akielekea kumlenga zaidi muandika katikati ya mistari, kwamba tulitakiwa kuandika majina yetu ya kwanza, yaani yale ya kizungu na kiarabu, kwa vile haya yetu ya kibantu yalikuwa magumu na yangeweza kuzitoa jasho ndimi za weupe waliotarajiwa kutoa mada kwenye kijikongamano hicho!

Yaani, kwa maana ya kwamba washiriki walitakiwa kuandika majina yao 'mazuri' ya Noel, Gilbert, Priscah, Peter, Evelyn, David, Roy, Desmond na mengineyo ya dizaini hiyo kwa kile tulichoelezwa kuwa ingesaidia sana katika kuokoa muda ambao ungepotea wakati ndimi za watoa mada weupe zikijikanyaga kanyaga katika kutamka majina yetu ya kibantu!

Ndio, kwamba ati majina ya Mpambalyoto, Rugarabamu, Mwakambaya, Khasimbago Khaabuka, Ambakyise, Masayanyika, Mamtogolo, Shekuavu, Shengoto, Mambazi, Mamkai na kadhalika na kadhalika, yalikuwa na muelekeo wa kusababisha ndimi za weupe wa watu kurudi kwao zikiwa mahututi kama sio kuvishwa POP kabisa!

Kwa vile akili za muandika katikati ya mistari huwa ziko mbele kwa madakika kadhaa, papo hapo akatoa hoja kwamba yeye angefurahi zaidi kuandikwa Mpilipili kwenye beji yake badala ya chesi, pamoja na kwamba hata hio chesi yenyewe ni jina la kiswahili tofauti kabisa na baadhi ya watu wanavyodhani kwamba limetoholewa kutoka jina la kiingereza la Chase ama Charles!

Mwandika katikati ya mistari akatoa hoja pia kwamba kwa vile weupe hao walikuwa wamekuja kwetu, basi wao ndio walipaswa kuzipa mazoezi ndimi zao ili kuhakikisha kwamba zinaweza kula sahani moja na majina yetu na sio sisi kuwarahisishia kazi kwa hasara ya kuukana ubantu wetu!

Ndio, kama weupe wale walikuwa wanataka sana sisi tuachane na majina yetu ya kibantu, basi ilikuwa ni kiasi cha wao kutusubiri tu tukienda kwenye balozi zao kuomba viza na kutufanyizia, badala ya kuja hapa na kutaka tujikane kwa ajili tu ya kijiwarsha cha siku mbili tatu@

Naam, weupe hao wangejuaje kwamba waliishawahi kufika Afrika na Bongo, bila kwanza ndimi zao kupata 'frakcha' na kuwekewa POP wakati wakijaribu kutamka jina la Masalakulangwa, kama sio lile la Mwakamsondole!

Angalia basi kilichotokea na kumuacha hoi bin twaabani mwandika hekaya. mweupe yule wala hakuwa hata na haja ya kubishana na chesi. kazi hio waliifanya vizuri kabisa wabantu wenzake chesi waliong'ang'ania kwamba kulikuwa na umuhimu wa kutumia majina yetu ya kizungu ili kumrahisishia mweupe mmoja tu kazi yake!

Kwamba eti hata kama tungeamua kutumia majina yetu ya kibantu, mengi yao yalikuwa ni marefu mno kiasi kwamba yasingeenea kwenye beji tulizokuwa tunatayarishiwa! Wakafikia hata hatua ya kumtaka kikejeli muandika katikati ya mistari ajaribu kuandika kwenye kibeji chake jina la kibantu la Mzanzugwamko ama Jigulamajambazi!

Mwandika katikati ya mistari akajikuta akijuta mno kwa nini marehemu baba yake hakuwa na jina reeefu kama lile la mfalme Shokolokobangoshei wa enzi zilee Bulicheka na mkewe walipokwenda Mombasa kuiona nchi. kwa hakika angeuvaa mbeji wake ulioandikwa jina hilo kwa fahari kuu, potelea mbali kwamba ungekuwa umeenea kifua kizima, kwapa hadi kwapa!

Tukafikia hapo. washiriki wabantu wa kajikongamano kale wakaona ni mali sana kutumia majina yetu ya kizungu na kiarabu badala ya yale ya ukoo tunayoyatumia huko maofisini, kwa vile tu ulimi wa mweupe mmoja mtoa mada ulikuwa hautaki tabu.

Mwandika katikati ya mistari anashukuru kwamba yeye aling'ang'ania, na hatimaye kukubaliwa, potelea mbali kwamba ni kwa shingo upande, beji yake kuandikwa Mpilipili kwa kipindi chote cha kijikongamano hicho ambacho mtu angesomewa majina ya washiriki angedhani kwamba kilikuwa cha weupe watupu... Mary, Dennis, Robert, Albert, Michael, Susan, Stephen, Irene na mbantu mmoja tu, Mpilipili! (makofi, tafadhali!)

Naam, bila shaka mweupe yule alirudi kwao akiwaza kuwa dah, hajawahi kuona jitu bishi na king'ang'anizi kama yule Mpilipili wa kule Bongo. lakini kuna uwezekano pia kwamba pengine moyoni mwake aliwaza kuwa pamoja na yote, angalau bado kuna mijitu Afrika inaweza kuusimamia na kuutetea Ubantu wao. sijui ingekuwa nyinyi wasomaji wangu wapenzi mngefanyaje
chesimpilipili

Wakuu, naomba mniruhusu niweke baadhi ya makala zangu hapa wakati Ndesanjo akiendelea kunipa somo juu ya kuhifadhi makala ndeeefu...

Thursday, April 20, 2006

chesimpilipili

Ndesanjo, nadhani somo lako kuhusu kublogu limeingia barabara. nakushukuru sana. sasa na tuanze kazi.....

Thursday, April 13, 2006

Napenda kuamini kuwa kwa wasomaji wa magazeti wengi walioko bongo jina la Chesi Mpilipili sio geni kwao kwa maana ya kwamba watakuwa wameishasoma makala zangu kadhaa za kiswahili na kiingereza kupitia magazeti mbali mbali yanayochapishwa bongo.

naamini kuwa huu utakuwa ni uwanja mpana zaidi wa kuwasiliana nao, wasomaji na waandishi wengine sehemu mbali mbali za ulimwengu huu. naomba kupiga (ama ni kubisha?) hodi.

Monday, April 03, 2006

salamu, bloggerz. mimi ni mpya hapa na ndio kwanza nafungua blogg yangu. maelezo mengine yanafuata.