chesimpilipili
Kuna hii ya majina yetu kwanza....
Wiki kama mbili tatu hivi nyuma, huyu mwandika katikati ya mistari alipata bahati ya kuhudhuria kijikongamano fulani hivi kuhusu mawasiliano kilichofanyika kwenye kijihoteli flani cha kitalii (wapi kwingine!) cha bei mbaya katikati ya jiji jema hili la Mzee Makamba la Dizim.
Mwandika katikati ya mistari bado anaamini kwamba kuteuliwa kwake na wahusika kuhudhuria kijisemina hicho kulitokana na ukweli kwamba kijiposho kilichokuwa kinatolewa kwenye kijikongamano hichi kilikuwa ni kijiposho mbuzi. kingekuwa beberu mwandika katikati ya mistari angeisikilizia kwenye bomba!
Ndio, unategemea nini kwa nchi ambayo kwenye kongamano la wasioona nje ya nchi inawakilishwa na wanaoona wengi kuliko wasioona.
Mwasikia sana? kabla ya kijikongamano hicho kuanza rasmi, washiriki tukatakiwa kuandika majina yetu, ya kwanza, ili yakatengenezewe beji ambazo tungetakiwa kuzivaa katika kipindi choote cha kijikongamano hicho kwa kile tulichoambiwa kuwa ni kurahisisha mawasiliano kati ya washiriki na watoa mada wazungu.
Basi bwana, huyu muandika hekaya akaandikisha jina lake la Mpilipili akiamini kwamba lilikuwa linajulikana zaidi kuliko lile la Chizi, mbali ya ile mantiki pana zaidi kwamba sisi wabantu tuna kawaida ya kujuana kwa majina ya ukoo zaidi kuliko yake 'kuazima' kutoka kwa wazungu na waarabu!
Akaja huyu mweupe mmoja mtayarishaji wa kijikongamano hicho na kuwasisitizia washiriki wote, lakini akielekea kumlenga zaidi muandika katikati ya mistari, kwamba tulitakiwa kuandika majina yetu ya kwanza, yaani yale ya kizungu na kiarabu, kwa vile haya yetu ya kibantu yalikuwa magumu na yangeweza kuzitoa jasho ndimi za weupe waliotarajiwa kutoa mada kwenye kijikongamano hicho!
Yaani, kwa maana ya kwamba washiriki walitakiwa kuandika majina yao 'mazuri' ya Noel, Gilbert, Priscah, Peter, Evelyn, David, Roy, Desmond na mengineyo ya dizaini hiyo kwa kile tulichoelezwa kuwa ingesaidia sana katika kuokoa muda ambao ungepotea wakati ndimi za watoa mada weupe zikijikanyaga kanyaga katika kutamka majina yetu ya kibantu!
Ndio, kwamba ati majina ya Mpambalyoto, Rugarabamu, Mwakambaya, Khasimbago Khaabuka, Ambakyise, Masayanyika, Mamtogolo, Shekuavu, Shengoto, Mambazi, Mamkai na kadhalika na kadhalika, yalikuwa na muelekeo wa kusababisha ndimi za weupe wa watu kurudi kwao zikiwa mahututi kama sio kuvishwa POP kabisa!
Kwa vile akili za muandika katikati ya mistari huwa ziko mbele kwa madakika kadhaa, papo hapo akatoa hoja kwamba yeye angefurahi zaidi kuandikwa Mpilipili kwenye beji yake badala ya chesi, pamoja na kwamba hata hio chesi yenyewe ni jina la kiswahili tofauti kabisa na baadhi ya watu wanavyodhani kwamba limetoholewa kutoka jina la kiingereza la Chase ama Charles!
Mwandika katikati ya mistari akatoa hoja pia kwamba kwa vile weupe hao walikuwa wamekuja kwetu, basi wao ndio walipaswa kuzipa mazoezi ndimi zao ili kuhakikisha kwamba zinaweza kula sahani moja na majina yetu na sio sisi kuwarahisishia kazi kwa hasara ya kuukana ubantu wetu!
Ndio, kama weupe wale walikuwa wanataka sana sisi tuachane na majina yetu ya kibantu, basi ilikuwa ni kiasi cha wao kutusubiri tu tukienda kwenye balozi zao kuomba viza na kutufanyizia, badala ya kuja hapa na kutaka tujikane kwa ajili tu ya kijiwarsha cha siku mbili tatu@
Naam, weupe hao wangejuaje kwamba waliishawahi kufika Afrika na Bongo, bila kwanza ndimi zao kupata 'frakcha' na kuwekewa POP wakati wakijaribu kutamka jina la Masalakulangwa, kama sio lile la Mwakamsondole!
Angalia basi kilichotokea na kumuacha hoi bin twaabani mwandika hekaya. mweupe yule wala hakuwa hata na haja ya kubishana na chesi. kazi hio waliifanya vizuri kabisa wabantu wenzake chesi waliong'ang'ania kwamba kulikuwa na umuhimu wa kutumia majina yetu ya kizungu ili kumrahisishia mweupe mmoja tu kazi yake!
Kwamba eti hata kama tungeamua kutumia majina yetu ya kibantu, mengi yao yalikuwa ni marefu mno kiasi kwamba yasingeenea kwenye beji tulizokuwa tunatayarishiwa! Wakafikia hata hatua ya kumtaka kikejeli muandika katikati ya mistari ajaribu kuandika kwenye kibeji chake jina la kibantu la Mzanzugwamko ama Jigulamajambazi!
Mwandika katikati ya mistari akajikuta akijuta mno kwa nini marehemu baba yake hakuwa na jina reeefu kama lile la mfalme Shokolokobangoshei wa enzi zilee Bulicheka na mkewe walipokwenda Mombasa kuiona nchi. kwa hakika angeuvaa mbeji wake ulioandikwa jina hilo kwa fahari kuu, potelea mbali kwamba ungekuwa umeenea kifua kizima, kwapa hadi kwapa!
Tukafikia hapo. washiriki wabantu wa kajikongamano kale wakaona ni mali sana kutumia majina yetu ya kizungu na kiarabu badala ya yale ya ukoo tunayoyatumia huko maofisini, kwa vile tu ulimi wa mweupe mmoja mtoa mada ulikuwa hautaki tabu.
Mwandika katikati ya mistari anashukuru kwamba yeye aling'ang'ania, na hatimaye kukubaliwa, potelea mbali kwamba ni kwa shingo upande, beji yake kuandikwa Mpilipili kwa kipindi chote cha kijikongamano hicho ambacho mtu angesomewa majina ya washiriki angedhani kwamba kilikuwa cha weupe watupu... Mary, Dennis, Robert, Albert, Michael, Susan, Stephen, Irene na mbantu mmoja tu, Mpilipili! (makofi, tafadhali!)
Naam, bila shaka mweupe yule alirudi kwao akiwaza kuwa dah, hajawahi kuona jitu bishi na king'ang'anizi kama yule Mpilipili wa kule Bongo. lakini kuna uwezekano pia kwamba pengine moyoni mwake aliwaza kuwa pamoja na yote, angalau bado kuna mijitu Afrika inaweza kuusimamia na kuutetea Ubantu wao. sijui ingekuwa nyinyi wasomaji wangu wapenzi mngefanyaje
1 comment:
SAWA MGOSI!
Hongera sana kwa makala yako Kaka. Ni ukweli usiokatalika kuwa wengi wetu 'Waswahili' hatupendi kutumia majina yetu ya asili, ambayo mengi yana maana nzuri tu. Majina Kama Alexander, John,George n.k. ndio tunayopenda kuyatanguliza, hasa tunapoona sura nyeupe. Lakini ni kwa faida ya nani? Kama utakumbuka baadhi ya sura za kitabu cha 'Song of Lawino/Ocol', mwandishi Okot P' Bitek aliliongelea suala hili kwa uchungu sana, la sisi kujidhalilisha namna hio. Nikabadilika tangu wakati huo, mara nyingi napenda kutanguliza jina langu la Kibantu katika matukio mbali mbali, kwa kuwa lina maana katika Kabila letu la Wasafwa wa Mbeya.
Hongera sana kwa mara nyingine Bw Mpilipili (sina uhakika kama kwa Kisambaa unatamka hizo 'L', kwa kuwa kule hazitamkwi.
Kazi njema. Nitembelee katika 'http://jadili.blogspot.com'
Post a Comment