Friday, February 29, 2008

Atafutaye hupata, lakini.....Mh!

Inawezekana kabisa kuwa watu wanaodhani kuwa mwana blogu anayeandika hapa ni muoga linapokuja suala linalohusu kugombea nafasi yoyote ya uongozi wana hoja. Inawezekana.

Inawezekana pia wana hoja wale wanaodhani kuwa sababu kuu ya mwana blogu huyu kuogopa kugombea nafasi yoyote ya uongozi ni kule kujifahamu kuwa sura yake haina mvuto` wa kuvuta kura za wapiga kura.

Bado pia Inawezekana wenye hoja wakawa wale ambao wanadhani kuwa kushindwa kwa Chesi kuwa mgombea wa nafasi yoyote ya uongozi kunatokana na mikono yake kugeuka mifupi ghafla linapokuja suala la kumwaga takrima.

Kwamba jamaa ana kawaida ya kuuugua kabisa homa pale anapolazimika kuingiza mkono mifukoni ili kutoa chochote kitu kwa ajili ya kuvuta kura za watoa kura!

Wote hawa wanaweza wakawa na hoja za msingi. Lililo wazi ni kuwa jibu la ni kwa nini miguu ya muandika katikati ya miguu ina kawaida ya kuota matende linapokuja suala la kuuchukua fomu ya kuomba madaraka ya aina yoyote ile, analo mwenyewe.

Ndio, ni yeye tu anayefahamu kuwa tangia mwaka ule wa 1972 akiwa darasa la tano pale shule ya msingi Chang’ombe alipojaribu kugombea kuwa monita wa darasa lao na kushindwa vibaya pamoja na kugawia wapiga kura kalamu, kichongeo na kifutio chake, jamaa alikata mguu kwenye masuala yote ya kugombea uongozi

Aibu ile aliyopata kwa kushindwa na mpinzani wake ambaye alikuwa hata hachezei timu ya shule kama yeye ikamtia woga na simanzi mno na kumfanya kuanzia siku ile aone kugombea nafasi yoyote ya uongozi ni sawa na kwenda kuomba pombe kwenye kaunta ya kituo cha Polisi!

Na kweli. Kuanzia 47 hiyo akakoma kugombea nafasi yoyote ya uongozi akichelea aibu na uchungu wa kugundua kuwa kumbe pamoja na watu wengi kucheka na kudai kuwa karibu naye, walikuwa hawamuamini sana kiasi cha kumpa nafasi ya kuwaongoza!

Kuanzia hapo, huu ukawa ndio msimamo wake na ukatetereka mara moja tu pale alipojiingiza kwenye kinyang’anyiro cha kugombea na hatimaye kushinda kwa kura za kishindo uchaguzi wa kugombea hili ‘Jimbo’ la uchaguzi ambalo si tu kwamba bado analishikilia kwa karibuni miaka ishirini sasa bali limeishamteua kabisa kuwa kiongozi wake wa maisha!

Kwa kifupi basi, hofu ya kugundua kuwa si kila aliye karibu naye ni mtoa kura wake mtarajiwa ndio kunakomfanya ayatupe kwa umbali unaozidi anvyoweza kuyatupa, masuala yote ya kugombea hiki ama kile. Uso umeumbwa na haya, ati!

Ni kutokana na hili ndio maana anashindwa awachukulie vipi hawa wabongo wenzake ambao kila aina ya uchaguzi unapotangazwa wao wanakuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kuuchukua fomu za kuwania kinachogombewa!

Ndio muandika globuni huyu anafahamu majina ya wabongo wenzake kadhaa ambao kila unapotokea uchaguzi wa aina yoyote hawasiti kutia timu. Ushujaa ulioje!

Anafahamu wabongo wenzake ambao wameishagombea kuongoza timu ya mpira wa miguu, chama cha mpira wa magongo, kamati kuu ya mpira wa vinyoya, timu ya mpira wa vikapu, timu ya mpira wa pete, baraza kuu la mpira wa Wavu na kote huko wamepigwa kibuti!

Anafahamu pia watu ambao wameishagombea kuongoza Chama cha Wapaa Samaki, Umoja wa Vijana wa Wafuga kuku, Kamati Kuu ya Halimashauri kuu ya Wapishi wa mahoteli, Ukuu wa jimbo kuu la Tamaa na hata nafasi za kuteuliwa za akina mama Wacheza bao, na bado hawakuambua kitu!

Kinachomuacha hoi zaidi ni kuona wabongo wenziwe hawa wameshindwa katika chaguzi husika pamoja na kudai, wakati wanachukua fomu, kuwa wameombwa na wazee kufanya hivyo!

Kwa hakika, najikuta nikiuonea wivu ushujaa wa watu hawa wa kuwa tayari kuuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hii ama nyadhifa ile tena na tena na tena pamoja na kwamba kila wakitia mguu wanatolewa kapa!

Ndio, Nasisimuliwa na ujasiri wa wabongo wenzetu hawa wa kujiona ama kudhani kuwa wao ndio wateule pekee wa kugombea kiila nafasi ya uongozi inayotangazwa kugombewa.

Kwa hakika, huwa nabaki nikijiuliza ni mpaka lini nyuso za wenzetu hawa zitakuwa na haya na ifike mahali wenye nyuso zao waamue wenyewe kuwa tumeishakataliwa kiasi cha kutosha, sasa basi!