Wadau, wanasema ni kwenda na wakati kalini sina hakika nyinyi mnalichukuliaje hili la kushughulikia misiba Bar….
Kwanza, nilidhani sikusikia vizuri tangazo lile. nitenga vizuri sikio langu kuukuu lililokwisha ona, kama sio kusikia, siku njema na kusikiliza tena kwa makini.
Na si kwamba nilichokuwa nataka kusikia kwa ukamilifu kilikuwa ni jina la marhum, la hasha. Hilo nilikuwa nimelisikia vizuri na kutambua kuwa alikuwa ni mtu ambaye japo hakuwa ndugu yangu, nilikuwa nikimfahamu vizuri. Kulikuwa na kingine kilichonivuta kusikiliza tena tangazo lile.
Na bila khiyana mtoa matangazo akarudia tena. Kwamba alikuwa anasikitika kutangaza kifo cha fulani bin fulani kilichotokea hukoo katika hospitali ya nanihii, habari ziwafikie huyo na yule na mipango ya mazishi ilikuwa inafanywa kwenye baa maarufu ya nanihino!
Eh? Mipango ya mazishi inafanywa kwenye baa ya nanihii!
Hiki ndicho ndicho nilichodhani kuwa nilikuwa sijakisikia vizuri. Nikawa nimedhibitishiwa kwamba nilichokuwa nimesikia ni kweli na kwamba antena zangu, kwa maana ya masikio, hazikuwa kuu kuu kiasi hicho!
Kwamba marehemu fulani bin fulani alikuwa amefariki dunia na ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanakutana kwenye Grosari fulani ili kupanga mipango ya kusafirisha mwili wake kwenda kuzikwa alikozaliwa. Mipango ya mazishi Bar!
Nikakumbuka kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa watu wachache hasa ambao ni wacha Mungu kwa maana halisi tofauti na akina Chesi ambao ucha Mungu wao unaonekana zaidi siku za jumamosi kwenye harusi badala ya jumapili kwenye misa!
Haya basi, tukanyanyuana na Bi mkubwa na kuelekea huko kwenye msiba, njiani tukiulizana ni masahibu gani yaliyokuwa yameikumba nyumba ya marehemu hadi ikaamuliwa mipango ya mazishi yake ikafanyiwe kwenye baa.
Ndio, nikajiuliza maswali kibao yasiyokuwa na majibu huku kubwa kuliko yote likiwa lile la jinsi marehemu alivyokuwa mcha Mungu na jinsi atakavyokuwa anajisikia huko aliko akiangalia mipango ya kuuzika ya mwili wake ikifanyika ndani ya Bar!
Tukafika pale nyumbani kwa marehemu ambapo palikuwa na liuwanja likubwa tu la kumwaga na kwa maana hiyo kuondoa dhana kwamba labda watu walikuwa wameamua kwenda kufanyia mipango ya kuusafirisha mwili wake Bar kutokana na kukosa nafasi kwenye makazi yake.
Nikambwaga mkuu mwenzie pale na kuelekea kule nilikoambiwa ndiko mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu na mazishi yake ilikuwa inafanyika. Nanihino Bar.
Nikafika pale na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wake kwa waume wakipanga na kupangua kipi kifanyike na kipi kisifanyike kuhusiana na msiba wa ndugu yetu huku mezani kukiwa kumesheheni 'vituliza majonzi’ kibao.
Kwa hakika, mtu yoyote ambaye angefika pale na kuona kilichokuwa kikiendelea, asingelaumiwa iwapo angedhani kuwa kilichokuwa kikiendelea ni kikao cha maandalizi ya harusi! Dhahiri angeshituka mno kuambiwa kuwa kile kilikuwa ni kikao cha maandalizi ya mazishi ya mtu!
Naomba niwe muwazi na kukiri kuwa nilijiunga kukaa kwenye kikao kile kwa machale huku kila mara nikigeuka huku na kule nikitegemea saa yoyote marehemu mcha Mungu kuwazukia pale na kutuuliza kwa nini tulikuwa tunafanyia Bar mipango ya kuzika mwili wake!
Ndio, kwa nini tulikuwa tunafanya mipango ya kusafirisha na kuzika mwili wake kwenye eneo ambalo meza ya pembeni kulikuwa na kikao cha maandalizi ya harusi, kandokando yake kulikuwa na kikao cha maandalizi ya Send-off ya mtu na pembeni kulikuwa pia na kikao cha usuluhishi wa ndoa ya mtu iliyokuwa juu ya mawe!
Naam, nimeishakiri mara kadhaa huko nyuma kuwa huwa huwa ninafanya jitihada za za ziada kuhakikisha kuwa siachwi nyuma na huku kunakoitwa kwenda na wakati lakini kila mara kumekuwa kunatokea jambo ambalo hunithibitishia kuwa amekuwa nikiachwa kwenye mataa na huo wakati!
Ndio, niliachwa nikishangaa watu walipoanza kuvaa sare za misiba, watu walipoanza kubeba makamera ya video makaburini, watu walipoanza kuwavalisha suti marehemu wakati hawakupata kuwanunulia suti walipokuwa hai, na wafiwa walipoanza kwenda saluni kabla ya shughuli ya kuaga miili ya marehemu wao.
Kwa hakika, kushangaa kwangu hili lililoanza kushika kasi siku za karibuni la vikao vya mipango ya kusafirisha na mazishi ya marehemu kufanyikia kwenye kumbi za starehe linamfanya adhibitishe wazi kabisa kuwa bado yeye ni mshamba aliyepitwa na wakati. Kwa hili, anakubali aendelee kubaki hivyo. Alamsik.
No comments:
Post a Comment