Thursday, November 09, 2006

Hii makala yangu kuhusu katuni ya waandishi wa habari wa Bongo kumlamba miguu mheshimiwa ilikuwa itoke kwenye
kolamu yangu ya gazeti la kila jumapili. haikutoka
.

Aha, mkuki kwa kitimoto hai, sio...?


Kiasi cha wiki mbili hivi zilizopita, vyombo vya habari vya nchi njema ya Bongo hususani magazeti, viliibua kinachoweza kuitwa kuwa ni 'tufani ndani ya kikombe cha chai' kuhusiana na kibonzo kilichokuwa kimechorwa kwenye gazeti moja la jumapili la nchi jirani ya Kenya.

Kibonzo hicho kilikuwa kinaonyesha waliolezwa kuwa ni waandishi wa habari wa Bongo wakifanya kile mchoraji alichoona ni kama kumlamba miguu, kumtetemekea na kujigonga gonga kwa mheshimiwa wa awamu ya ari, nguvu na kasi mpya, JK.

Kupitia mchoro wake, mchoraji wa kibonzo ambaye kama kumbukumbu za muandika katikati ya mistari hazijaathirika sana na masika 47 ambazo ameishanyeshewa mpaka leo hii, ni mbongo mwenzetu anayefanya kazi huko kitambo sasa, ametumia uhuru na haki yake kuonyesha kile anachodhani kuwa kinaendelea katika medani ya uandishi wa habari hapa Bongo.

Inaelekea kibonzo kile kiliwakera mno wanahabari wa nchi njema ya Bongo ambao kila mara wamekuwa msitari wa mbele kudai haki na uhuru wa mtu kutoa na kupokea habari bila kuingiliwa na mtu alimradi tu havunji sheria za nchi.

Wakamuibukia mchora kibonzo husika na kwa kutumia silaha zao kali kabisa zisizo Patriot wala Mig wala AK 47 bali kalamu zao, kukemea, kuasa, kumuonya na kumtaka mchora katuni huyo aachane nao na ashike lake. Kwamba medani ya uandishi wa habari hapa Bongo ilikuwa na kanuni zake ambazo kufanya kazi kwa kumfurahisha mtu kamwe hakukuwa moja ya kanuni hizo!

Naam, baadhi ya makala zikawa na muelekeo wa wanahabari wetu kumwaga mboga kwa vile mchora kibonzo husika alikuwa amemwaga ugali. kwamba mchora katuni anaona ajabu gani waandishi wa habari wa Bongo kulamba miguu ya watawala wakati wao walikuwa wanfanya hayo hayo. ndio, yale yale ya shughuli afanye bata, akifanya kuku inakuwa balaa.

Step fulani, mtaaluma anayesimamia masuala ya habari kwenye ofisi ya mheshimiwa wa kasi, nguvu na ari mpya naye pia akatia timu kwenye sakata hilo kwa kutamka kuwa jumba jeupe lililoko Magogoni lilikuwa halijafurahishwa sana na katuni hiyo, lakini hata hivyo wasingeijibu mapigo.

Kidoogo hapa muandika katikati ya mistari akatatizika. hivi mtaaluma huyu anayesimamia habari pale Ikulu alikuwa akitegemea mchora katuni wa nchi jirani achore katuni kwa ajili ya kuifurahisha Ikulu ya Bongo? hivi mtaaluma alikuwa na maana kuwa kigezo cha kuchora katuni kwa nchi jirani kilikuwa ni katuni hiyo kuifurahisha ama kutoifurahisha Ikulu ya Dizim?

Waama, ilisisimua mno kuona vyombo hivi vya habari vya nchi njema ya Bongo ambavyo vinakuwaga mstari wa mbele kutetea uhuru wa mtu kutoa na kupokea habari bila kuingiliwa na mtu vikizusha 'tufani ndani ya kikombe cha chai' dhidi ya mwenzao aliyetumia uhuru wake wa kutoa na kupokea habari bila kuingiliwa na mtu!

Kilichomtatiza zaidi muandika katikati ya mistari ni kuona kuwa katika nyingi ya makala za ukali zilizoandikwa dhidi ya kibonzo husika, nyingi zililenga zaidi kujikosha jinsi taaluma ya habari ya Bongo inavyofanya kazi kwa kanuni zake badala ya kujibu hoja ya katuni ya kama waandishi wa habari wa Bongo walikuwa wanafanya kazi kwa muelekeo wa kumlamba na kujigongagonga kwa mheshimiwa ama la!

Ndio, muandika katikati ya mistari hakumbuki kusoma makala iliyokiri kwa uwazi kabisa bila kumung'unya maneno kwamba ndio, wapo baadhi ya waandishi na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vinafanya kazi kwa namna ambayo ingebidi mtu ujilazimishe sana kuamini kwamba sio kujigonga gonga kwa waheshimiwa wa kasi, ari na nguvu mpya!

Kwamba baadhi ya makala zilizokuwa zikiandikwa magazetini na baadhi ya waandishi kuhusiana na mheshimiwa zilikuwa ni pungufu kidogo tu ya barua za maombi ya kazi kutoka kwa waandishi husika kwenda kwa mheshimiwa na ofisi yake!

Kwa mawazo ya muandika katikati ya mistari, hili ndio lilikuwa la kujadili. sio lile la 'mbona wao wanafanya hivyo hivyo'. Hivi mtu akikuambia kuwa umeshika kinyesi unakimbilia kumjibu kuwa 'mbona wewe umeshika!', ama unakimbilia kunawa mkono na kumuacha yeye akiendelea kushika kinyesi!

Muandika katikati ya mistari anaamini kuwa suala la vyombo vya habari kufagilia na kujigongagonga kwa watawala ni suala ambalo limekuwepo tangia Adamu. kwa maana hiyo hakukuwa na haja ya watu kutoana macho. badaala yake, anaamini kuwa yapo mambo kadhaa ambayo watu wanaweza kuyafanya na yakapunguza kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari kuonekana vinalamba miguu ya watawala.

Wakati zogo hilo la 'wanamlamba ama hawamlambi miguu' likiendelea, tukaanza kushuhudia baadhi ya waandishi na vyombo vya habari vikiibatiza jina timu yetu ya mpira wa miguu, Taifa Stars,kutokana na mafanikio iliyokuwa ikiendelea kuyapata kwenye michuano, jina la 'JK Eleven'!

Muandika katikati ya mistari amejikuta akiiangalia ile katuni iliyowafanya watu wateme cheche na kisha kuwaza juu ya muandishi wa habari anayeamka asubuhi na kuamua mwenyewe kuwa kuanzia siku hiyo timu ya taifa itakuwa sio Taifa Stars tena bali 'JK Eleven'

Maana, kwa mtazamo wa kawaida kabisa muandika katikati ya mistari alidhani kuwa jambo kubwa na muhimu kama la kuipa jina jipya timu yetu ya mpira wa miguu, kama kuna ulazima wa kufanya hivyo, lilifaa kujadiliwa kwanza na wadau wa eneo husika na kisha wote kwa ujumla wetu tukafikia muafaka wa kuibalisha jina timu yetu ya Taifa.

Muandika katikati ya mistari hapingi mheshimiwa wetu kupendwa mno kiasi cha baadhi ya watu kuona ipo haja ya kuibatiza tinu yetu ya taifa jina lake. hata hivyo anaona picha inayokuja huko mbele iwapo kila mara tutapenda kubadili majina ya vitu kutokana na watawala waliopo madarakani wakati husika.

Anaona baada ya miaka kumi timu ya taifa ikibadilishwa jina na kuitwa 'CM Eleven' kwa tu vile raisi wa nchi wa wakati huo, mheshimiwa sana Chesi Mpilipili atakuwa ameinunulia jezi na baada ya miaka kumi mingine timu itabadilishwa jina na kuitwa 'DM Eleven' kwa vile raisi wa wakati huo Mtukufu sana Desi Mpilipili atakayekuwa amemrithi baba yake naye atakuwa ameinunulia mipira!

Waandishi wetu wana haki ya kuhoji mchora vibonzo wa nchi jirani kuwachora kuwa wanalamba miguu ya watawala. na wao basi angalau wajitahidi tahidi wasimpe mtu sababu ya kufanya hivyo. alamsik.

Monday, July 10, 2006

Kuna utata juu ya kutumika ama kutotumika kwa kile kinachoitwa 'Tiba ya mkojo'. Haya ndiyo mawazo
yangu...!
!


Kuna mzee wangu mmoja wa kisambaa alipata kusema karne hizoo za zamani. Akili nyingi huondoa maarifa, bila shaka akimaanisha kwamba kuwa na akili ni kitu chema lakini ukizitumia vibaya ni hasara tupu.

Najua, kuna watu wamezaliwa na ubishi kisha wakachanjia ubishi ambao hapa wataanza kubishia kauli yangu hii na kuanza kunitaka nitoe ushahidi kwamba maneno hayo yalitamkwa na mzee fulani wa kisambaa. Salaam zao. Wao watoe ushahidi kwanza kwamba hayakutamkwa na mzee wangu mmoja wa kisambaa!

Haya, katika miaka hii ya karibuni mwandika katikati ya mistari amekuwa akishuhudia mambo kadhaa ambayo tunaweza tukakubaliana kuyachukulia kama ushahidi tosha wa kwamba mzee wangu wa kisambaa alikuwa ameona mbali na kwamba kweli akili nyingi huondoa maarifa.

Tuanze na huu mfano mmoja mkubwa. Karne kadhaa zilizopita, hawa watu weupe ambao kwa hakika ndio wanaotawala dunia ‘walivumbua’ mavazi na binadamu akaanza kuvaa nguo badala ya kuwa akitembea mambo hazalani, kama alivyokuwa akifanya kabla ya uzinduzi huo wa albam ya nguo!

Katika karne zilizofuata, binadamu weupe wakaendelea ‘kuvumbua’ aina mbali mbali za mitindo ya nguo. Kuanzia suti hadi kanzu hadi gauni hadi kaptura hadi pensi hadi sketi na kadhalika na kadhalika, yote ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa binadamu anajisetiri kwa namna mbali mbali huku akipendeza.

Inaelekea kuwa akili za kuvumbua zikazidi na miaka machache tu iliyopita, baadhi ya weupe hawa ‘wakavumbua’ kuwa kumbe kuvaa nguo sio mali kitu tena na kulikuwa na burudani zaidi katika kutembea mambo hazalani kama karne zilee za kiza kabla nguo hazijavumbuliwa!

Ndio maana katika baadhi ya nchi zinazosemekana kuwa ni za walioendelea, kuna maeneo ambayo yametengwa maalumu kwa ajili ya wadau ‘waliovumbua’ kuwa kuna wakati binadamu anapaswa kuweka minguo yake kando na kuishi kama alivyozaliwa. Mambo hazalani!

Yaani wewe ukiishafika maeneno hayo basi sarawili yako, sijui suti yako ama gauni lako unalichojoa na viambatanishi vyote ulivyonavyo mwilini unaweka kando na kuanza kuvinjari ukiwa kama ulivyoingia duniani. Mambo hazalani!

Tena basi unaambiwa unashauriwa kabisa kuwa ukitaka kutinga maeneo hayo basi ni vema uende na mkeo, mkweo na vitukutu vyenu pengine katika jitihada za wanaosimamia maeneo hayo kuhakikisha kuwa macho balbu yako yanaishia kwa uliye naye na sio kwa wa wenzako!

Muandika katikati ya mistari ana kawaida ya kujifagilia mno kuwa akili zake ziko dakika tatu mbele, lakini hapa ameinua mikono juu. Ameshindwa kabisa kuingiza kichwani mwake picha ya yeye akiwa na mkewe, vitukutu vyao na mkw…..stafirulahi, mungu apishe mbali!

Muandika katikati ya mistari ana matumaini kuwa ‘akili nyingi’ hizi za ‘kuvumbua’ maisha bila nguo hazitapata wadau wengi hapa nchini ingawaje nyakati kadhaa anapoangalia kilichovaliwa na baadhi ya mabinti zetu anajikuta akajiuliza iwapo kweli hatupo tayari kwenye maeneo ya watembea uchi!

Yapo mengi. Kuna wakati pia ‘akili nyingi’ za hawa ndugu zetu weupe zilipata kutuambia kuwa ngoma zetu za kunengua viuno ni za kishenzi na kwamba binadamu mstaarabu ni yule tu anayecheza ‘ngoma’ zao za kistaarabu kama Tango, Waltz, Rumba na nini tena sijui.

Akili nyingi huondoa maarifa. Katika miaka ya karibuni tunashuhudia wasanii wa kizungu ‘wakivumbua’ kukatika na kunengua viuno kwenye video zao sio tu kama hawana akili nzuri bali pia kwa namna ambayo hata wanasindimba wetu hawaoni ndani..

Yapo mengi ya kudhibitisha kuwa kweli akili nyingi huondoa maarifa, lakini kiboko ni hili lililotuzukia katika miaka ya hivi karibuni la watu ‘kuvumbua’ kunywa…ashakum, mikojo yao wenyewe kwa kisingizio kwamba ati ni tiba!

Ndio, tunaambiwa na ‘wavumbuzi’ hawa wenye ‘akili nyingi’ kwamba ati iwapo mtu unataka mwili wako usiandamwe andamwe na magonjwa ya kiajabu ajabu na pia usizeeke haraka basi ulitakiwa kunywa glasi moja ya mkojo wako mwenyewe kila siku asubuhi.

Tukaambiwa pia kuwa kama kulikuwa na dawa bora kabisa ambayo ilikuwa na uwezo wa kutibu magonjwa sugu kibao tu yakiwemo yale yaliyowashindwa waganga wengine basi ilikuwa ni mkojo wako mwenyewe. Glasi moja iliyojaa mkojo kila siku asubuhi basi wee mambo yako swafi tu! Ukitoka hapo unaenda kumbusu mshikaki wako, raha tupu!

Katika kuhalalisha kwao hili, wadau hawa wa tiba ya mkojo wakanukuu hata maneno ya vitabu vitakatifu vya dini yasemayo ‘unywe maji kutoka birika lako mwenyewe’ na kujaribu kutushawishi kwamba yalikuwa na maana ya kumtaka mtu kunywa mkojo wake mwenyewe! Tumbaku kabisa!

Wadau hawa wanatuambia kuwa mkojo unapotoka mwilini unatoka na chembechembe za madini fulani ambayo yana faida kubwa mwilini. Swali la Chesi ni kuwa kama yana faida kubwa mwilini kwa nini yatolewe kupitia mkojo? Si ina maana madini hayo yamejaa tele mwilini ndio maana ziada yake inaondolewa kupitia mkojo??

Kwa vile kuna watu hawakawiagi kutupa ngumi, mwandika katikati ya mistari anaomba kuharakisha kusema kabisa kuwa hapa hapingi haki ya mtu kunywa mkojo wake mwenyewe. Na anywe tani yake maana kila mtu ana Uhuru wa kufanya anavyotaka mradi tu havunji sheria na hili ninaamini kwamba halijawekewa sheria ingawaje limeishapiga hodi kwa waheshimiwa pale Domdom na limeishatolewa tamko.

Labda tu hapa tuombe kutungiwa sheria ya kuzuia mtu kunywa limkojo lake na kisha kwenda kumbusu mwandani wake bila kumtahadharisha kwanza kuwa asubuhi alikuwa amepiga glasi moja ya mkojo na hivyo kumpa nafasi mwandani wake huyo ya kuamua mwenyewe kama aendelee na busu hilo ama la!

Ufahamu mdogo alionao chesi kuhusu mwili wake unamuambia kuwa mkojo ni njia maalumu iliyowekwa na Muumba kwa ajili ya mwili kutoa takataka zake za majimaji, full stop. hakuna cha madini wala nini. ni uchafu tu!

Ni kichekesho cha karne basi mwili ukusanye takataka zake za majimaji na kuzitoa mwilini halafu sisi kutokana na akili zetu nyingi kuzidi maarifa tukinge glasi zetu na kuurudisha tena mwilini kupitia mdomoni!

Kuna wakati mpaka muandika katikati ya mistari akawaza kimzaha kuwa isije ikawa jamaa walisikia kuwa tunakunywa 'mkojo wa punda' kama dawa ya kikohozi basi wakashawishika kudhani kuwa kama tunaweza kunywa mkojo wa punda basi wakituchomekea kunywa wa binadamu itakuwa ni kwa kwenda mbele!

Mwandika katikati ya mistari anaanza kuhofu pia kuwa iwapo leo tunakubali akili zetu nyingi zilizozidi maarifa zitushawishi kurudisha mkojo mwilini, basi kesho itakuwa ni jasho, kesho kutwa makamasi na mtondogoo ni mambo makubwa zaidi yanayotolewa mwilini mwetu kama uchafu!

Kumrandhi kwa kukuchefua, mdau wa eneo hili lakini huku ndiko tunakojilengesha maana kama alivyobainisha mzee wangu mmoja wa kisambaa (acha ubishi!), akili nyingi huondoa maarifa. Alamsik
kombe la dunia lina kasheshe zake. hususani kwa akina siye tunaolicheza kwa mdomo....

Kwa muda wa wiki mbili sasa, hii sehemu ambayo muandika katikati ya mistari haoni hata aibu ya kuiita ati sebule yake, imekuwa ni kijiwe ama kongamano la makocha, wachambuzi, wachambaji wataalamu na wataaluma wa soka ambao uchambuzi wao kuhusu mechi za kombe la dunia umemfanya Chizi kujiuliza kila mara watu hawa wanangoja nini hapa bongo!

Ndio, ni wataalamu na wataaluma mno wa soka kiasi kwamba nina hakika kabisa kuwa iwapo watajisumbua kidogo tu kuandika barua za maombi ya ukocha pale jiji la Manchester, basi kibarua cha mtafuna Big G mmoja aitwaye Sir Alex Ferguson kitaota magugu! hakya nani tena vile!

Halafu nimegundua pia mara nyingi kwamba utaalamu na utaaluma wa soka wa waheshimiwa hawa walio marafiki, majirani na ndugu zangu wanaokuja kukodolea macho haka katiivii kangu ka nchi kumi na mbili, huongezeka maradufu pale bi mkubwa wa nyumba na wadogo zake kadhaa wa kike wanapojiunga kuwa miongoni mwa watazamaji wa mechi husika. hapo tena, hakuna anayekubali kushindwa!

Nikagundua pia kuwa wengi wa waataluma na wataalamu wangu hawa wa soka la sebuleni walikuwa hawakuwahi kucheza japo chandimu utotoni mwao afadhali hata mimi ambaye niliishakipiga hadi ngani ya unahodha wa timu yetu ya darasa la tano mwaka 1972 pale Chang'ombe shule ya msingi!!

Naam, kwa hakika ni maoni ya wataaluma na wataalamu hawa wa kibongo yanayonifanya niamini kwamba ninachotizama sebuleni kwangu sio kombe la dunia bali soka la sebuleni la kimataifa!

Kwa mfano, kuna huyu mmoja ambaye ana shahada ya juu ya ukocha wa kuwakosoa wachezajiwa timu zinazocheza uwanjani: "Ayaa! mwangalie sasa yule migulu baja anakopeleka mpira! pale alitakiwa arudishe mpira nyuma kwa mwanangu mwenyewe Figo ama atie majalo kwa mzee mzima nanihii apige bao, badala yake anacheza mdundiko na mpira! mwangalie kwanza, jibukta kubwa kaa kisafleti!"

Ama: "Tatizo hawa Uingereza hawaijui hii infomesheni ya 3-5-2, sana sana wanalazimisha tu! pale yule Cole alitakiwa apande (sio mchicha, ndugu msomaji!) halafu huyu Ferdinand ashuke chini kama Libero, lakini waapi! ubishololo na baraka ya kuvaa mijikaptura mireeefu tu!"

Halafu yupo huyu mtaalamu mwenye shahada ya juu ya ukocha wa kuwakosoa makocha wenzake wa kombe la dunia...na hali yeye ni kocha wa sebuleni kwa chesi tu!! "Ama huyu kocha wa Uruguay ndio amepanga timu gani sasa hii! hawa lazima leo wapigwe bao tu! pale alitakiwa amtoe yule namba kumi na moja ambae anazunguka tu uwanjani kaa daladala na sio amtoe yule namba tisa ambaye mambo makubwa yake tunayaona! mii nakwambia hawa makoccha wengine basi tu! muone kwanza, suruali kaa yangu!!"

Alikuwepo pia mkereketwa mmoja aliyekuwa akiiona Ghana kama ni mkoa wa.. waaa... wa..ah, sijui wa ngapi vile wa bongo; "Angalieni wanaume hao! mi nakwambieni hawa ndio mabingwa wapya wa dunia mwaka huu! Si unaona mwenyewe alivyomtungua bao mbili kwa gurudumu yule mcheki?

Yatosha tu kusema kwamba baada ya Ghana kufungishwa virago, mkereketwa huyu hatukumuona tena kwenye uwanja wetu wa sebuleni na kwa kweli tukaukosa mno utaalamu wake mkubwa katika soka la kimataifa, hususani ilipokuja suala la 'mkoa' wake wa Ghana!

Alikuwepo pia huyu bwana mdogo wangu mmoja ambaye yeye alikuwa na kazi moja tu ya kufananisha mambo: "Ebwanaee! umecheki darizi lile la mzee Patrick Viera! Duh! yaani kama lile lile alilofanya yule nanihii wa wekundu wa Msimbazi kwenye ile mechi kati ya nanihii na nanihii pale uwanja wa taifa!"

Au: "Duh! Ebwanaee! hii midfield ya Ureno mwanangu sio mchezo! inagawa mavyumba na mapande kama anavyogawaga Nanihino wa Wanjano wa Jangwani! yaani, wee acha tu!"

Step fulani bwana mdogo wangu huyu katika kujaribu kwake kujijazia maujiko kwa mabinti zangu, akajaribu hata kufananisha viwanja: "Dah! lile jukwaa la uwanja wa Munich sio mchezo, mwanangu mwenyewe! Yaani, dah! kaa lile dude letu la Kirumba!"

Kauli hii ikaufanya uzalendo wa watazamaji walio wengi uyeyuke. wakamtaka bwaa mdogo wangu yule afunge bakuli lake, ama aende akalale na awaachie watu waangalie mpira. akakubali kufunga bakuli. nahisi alikuwa hana hata kitanda.

Alikuwepo pia mtaalamu wa kukandya: "Mii nawaambia hizi timu nyingine sijui hata zinafikaje kwenye fainali hizi, kama sio kubebwa tu! mtu utafungwaje gongo sita, bwana? ee? mtu utafungwaje gongo sita kaa umesimama! mi nawaambia hata taifa stars yetu ingepeta kichizi kwenye fainali hizi!"

Hata hivyo mtaaluma huyu akashindwa kutufafanulia ni kwa vipi basi hio Taifa stars yetu haijafanikiwa hata kunusa tu huko kwenye watu wanaopigwa gongo sita kaa wamesimama, na hali yenyewe ingepeta tu kwa sana!

Kipindi fulani, hata huyu bi mkubwa wa nyumba naye pia akataka kuonyesha kwamba hayuko nyuma katika mambo ya kandanda na kwamba akiamua kujisumbua kidogo tu kwenda Uingereza kutafuta kazi ya ukocha, kibarua cha mfaransa Arsene Wenge kitaota mbawa: "Yule kocha naye mbona amezubaa hivyo, kaa mkono wa kanzu! si anatakiwa awaambie wachezaji wake kwamba kila pale mwenzao anapopiga penati(akimaanisha kona!) wao waende wakamvamie kipa na kumsukuma ili wafunge goli!"

Ni ajabu kwamba pamoja na wataalamu na wataaluma kibao wa soka waliojazana sebuleni mwangu mule hakuna hata mmoja aliyediriki kuinua mdomo wake na kumsahihisha bi mkubwa wa nyumba kwamba kilichokuwa kikipigwa ni kona na wala sio penati! hakukuwa na mwenye jeuri hio.

Kiboko cha wote hata hivyo alikuwa huyu lastborn wangu wa miaka saba, mheshimiwa sana Desi. wakati wenzake tukiendelea kuangalia mpira yeye alikuwa akiendelea na michezo yake mingine. pale goli lilipoingia ndipo alipokuja mbio na kutaka kujua...ni rangi gani ambayo imefunga!

Naam, yeye alichokuwa anamaindi ni rangi tu, hayo mambo ya sijui Ghana, sijui Brazili ama Uingereza ama Trinidadi na Tumbaku alituachia tujaze wenyewe!!

Yote kwa yote, katika kipindi hiki kigumu ambacho kila kitu kimepanda bei, wataalamu na wataaluma hawa wa soka la kimataifa , kupitia tiivii ya nchi kumi na mbili iliyo kwenye sebule langu, wananipa angalau sababu ya kutabasamu!! jumapili njema ya kushabikia wenzetu!

Monday, June 05, 2006

wapo wanasi-hasa wengi tu wakibongo ambao wakiisha wekewa maikrofoni mbele ya midomo yao, basi. kwao, time inakuwa sio money tena...!

siku ya May Day mheshimiwa aliliona hili na kwa vile yeye huwa hakopeshagi, akalizungumzia kwa kuwaambia wanasi-hasa hawa.....



‘Sio lazima kila mtu aongee, jamani'...!

Naam, siku ile ya jumatatu ya wiki hii ambayo ilikuwa ni siku ya watumwa duniani, nikawa nimekaa mbele ya kijiredio changu cha mwaka 47 ili kusikiliza kile ambacho mkuu wa nchi alikuwa anataka kukisema.

Naomba kwanza nisisitize kusema kwamba sina kawaida ya kusikiliza redio kwa mantiki kwamba kuna faida gani kutumia masikio peke yake kusikiliza kitu ambacho Kumbe unaweza pia kukiona kwa macho kupitia kwenye kioo a.k.a tiivii.

Kwa Bahati mbaya, safari hii vituo vyote vya tiivii vikawa havina mpango wa kuonyesha live kile kilichokuwa kikiendelea Shinyanga, mji ambao tangia muandika katikati ya mistari alipouondoka mwaka 1977 akiwa denti wa pale Shaibushi ni kama alikung’uta mavumbi, chembilecho vitabu vya dini, maana mpaka leo hii hajaingiza mguu tena!

Haya basi, ili kupata live hotuba ya mheshimiwa tukalazimika kukumbuka viredio vyetu ambavyo wengine tuliisha vifungasha zamani tukingoja mtu anayekwenda kijijini awapelekee ndugu na jamaa zetu nao wajidai. ganda la muwa la jana ni kivuno kwa chungu.

Kama nilivyokwisha sema. Sina kawaida ya kusikiliza redio hasa ukichukulia kuwa nyingi ya redio zetu zinazosikika vyema siku hizi ni madebe masaa ishirini na tano. Kilichonisukuma kusikiliza redio siku ile ilikuwa ni kutaka tu kujua iwapo iwapo Mheshimiwa ataongeza chochote kitu kwenye masihara yetu ya mshahara, basi.

Nikanunua betri mpya na kisha nikakaa kusikiliza kilichokuwa kikiendelea kule Shinyanga. Waheshimiwa wakaanza kukaribishana jukwaani kuhutubia kwa staili yao ile ile ya miaka nenda rudi tangia mwaka 47aa ambayo sio ngeni sana kwetu…

Mheshimiwa huyu anamkaribisha yule ili amkaribishe huyo ambaye atamkaribisha huyu ambaye atashukuru kwa kupewa nafasi ya kumkaribisha huyu ambaye atazungumza maneno machache (yanayoishia kuwa rundo!) ya kumkaribisha yule ambaye atamkaribisha wa kumkaribisha huyu, ilimradi Kizunguzungu kitupu!

Ni kwa utaratibu huu ndio maana masaa kadhaa baadaye, muandika katikati ya mistari akawa hajamsikia yule ambaye alikuwa amemfanya aibue kiredio chake huko kilikokuwa na anunue betri mpya ili kumsikiliza.

Mwandika katikati ya mistari akajiuliza iwapo waheshimiwa wale waliokuwa wakiendelea kupokezana vijiti vya kukaribishana walikuwa kweli hawafahamu kuwa watu walikuwa wamejaa uwanjani pale kumsikiliza mheshimiwa na sio mtu mwingine yoyote.

kwamba wengine, kama huyu Chizi, walikuwa wamelazimika hata kuibua viredio vyao vya zamani kutoka walikokuwa wamevichimbia ili tu kusikia live kitakachosemwa na Mheshimiwa badala ya kutegemea RedioMbao FM!

Kwa hakika, muandika katikati ya mistari hakuona umuhimu wa kuanza kusomeshwa historia ya vyama vya wafanyakazi pale maana ameishahudhuria siku za wafanyakazi kama thelathini mfululizo kwa kwenda nyuma na kila siku yanayosemwa ni yale yale tu na anaweza kuyakariri hata kwa kinyume nyume!

Haya, unaambiwa stepu fulani pia tukachomekewa ratiba ya kuzawadia wanamichezo. Mwandika katikati ya mistari akajiuliza mno. Ile ilikuwa ni sikukuu ya wafanyakazi, wafukuza upepo na wacheza mpira walikuwa wapi na wapi pale, potelea mbali kwamba nao pia walikuwa wafanyakazi!

Ndio, kwa nini zawadi zao kwa washindi zisingekabidhiwa jana yake na siku ile wakatuacha tuendelee na programu nyingine? Ina maana tulitakiwa tutegemee sasa kwamba siku ya kuzawadia wanamichezo bora wa mwaka basi watazawadiwa pia dakitari bora wa mwaka, mwalimu bora wa mwaka na pengine hata mpiga debe bora wa mwaka?

Jamani wabongo, mbona tunapenda kuchanganya mambo hivi? Si ndio haya haya ya ile shughuli ya klabu bingwa ya warembo nchini kuchukua zaidi ya masaa matano hadi saba na pengine mpaka alfajiri wakati ile ya dunia inachukua masaa mawili tu?

Hatimaaaaaye, wakati huyu muandika katikati ya mistari akiwa ameishaanza kusinzia kwenye kochi ndipo watu wakakumbuka kuwa ala, Kumbe Mheshimiwa naye anatakiwa kuhutubia na hivyo kumualika jukwaani.

Nnachompendea huyu Mheshimiwa ni kutokukopesha maneno. Utafikiri ni mdau wa ‘katikati ya mistari’. Bila kuuma uma maneno cha kwanza alichotamka kikawa kile kile kilichokuwa kichwani mwa Chizi, kwamba siri moja ya shughuli kama zile ilikuwa ni ile ya kuamua kuwa sio lazima kila mtu azungumze!

Kwamba kulikuwa hakuna ulazima wowote wa kusoma kila salamu iliyotumwa kuanzia mwanzo hadi mwisho kwani ingetosha tu kusema kuwa tumepokea salamu kutoka kwa huyu na huyu na yule basi, bila kuanza kuzisoma zote! Makofi, tafadhali!

Kwamba hatari kuu ya kutaka kila mtu jukwaani azungumze ilikuwa ni ile ya kujikuta waheshimiwa mlioko jukwaani mko peke yenu na mnahutubiana wenyewe kwa wenyewe maana kila mwananchi ameishachoka na kuishia zake.

Kwa kifupi kabisa, ujumbe wa Mheshimiwa kwa waheshimiwa wale ulikuwa ni kukumbuka kuwa ‘time is money’. Kwamba kulikuwa kuna taratibu nyingine ambazo kwa hakika kwa karne tuliyonayo hazikuwa za lazima sana kuzifanya.

Kama tumemualika Mheshimiwa kuhutubia May day, basi na tumpe nafasi ya kufanya hivyo. salamu kibao na kuwazawadia wanariadha kwanza nako kunatoka wapi. Time is money, jamani.
chesimpilipili

wakati akina sisi bado tunapoteza muda kwenye mazungumzo, mikakati, mipango na maandalizi ya kutwaa kilicho chetu, wenzetu wanafanya kweli. ndio maana nikauliza.........


Wao wanaweza wana nini ?

Kuna huyu mheshimiwa mmoja kutoka katika nchi iliyopo eneo la Amerika ya kusini ambaye, kama alivyo huyu mheshimiwa mwingine kutoka hii nchi iliyopo mashariki mwa bara la Afrika, ndio kwanzaa amekabidhiwa uongozi wa nchi na wananchi wake.

Ni ajabu kwamba waandishi wa habari wa nchi hii iliyopo mashariki kabisa mwa bara la Afrika hawajasema kuwa mheshimiwa wao amepewa ulaji na wananchi kama wanavyo kimbiliaga kusema pale mtu anapoteuliwa kushika nafasi fulani muhimu ya uongozi. thubutu yao.

Turudi kwa huyu mheshimiwa wa nchi iliyopo Marekani ya kusini. huyu, tumeambiwa kuwa ni mheshimiwa wa kwanza kuongoza nchi hiyo akitokea kwenye kabila la aina fulani ya maponjoro ambalo katika nchi hiyo ni watu wa ngai ya chini kabisa.

Haya, mheshimiwa akatwaa ubingwa wa klabu bingwa ya kugombea uraisi wa nchi nchini humo. akaanza kuweka mambo sawa ambayo kabla ya hapo alikuwa anaona kuwa yalikuwa yakiendeshwa ndivyo sivyo. naam, kama afanyavyo sasa huyu mwenzake wa nchi iliyopo mashariki kabisa mwa Afrika mashariki.

Miongoni mwa rasilimali kubwa ambazo nchi hiyo ya Amerika kusini ilikuwa imebarikiwa kuwa navyo ni utajiri mkubwa wa mafuta. tunalazimika kuharakisha kufafanua mapema kuwa hapa tuna maana ya mafuta ya Petroli, maana kuna watu wakisikia tu mafuta mawazo yao yanakimbilia kwenye Chipsi!

Ndio, nchi hiyo ilikuwa na utajiri mkubwa wa mafuta, lakini kama ilivyo kwa nchi nyenza iliyopo mashariki mwa Afrika mashariki ambayo katika mambo ya railimali kutoka ardhini nayo wamo, mapato yatokanayo na rasimali hiyo waliyopangiwa na Mungu mwenyewe yalikuwa yanawanufaisha zaidi wachache kutoka nje ya nchi wakisaidiana na wachache wengine walio ndani ya nchi.

Mheshimiwa huyu wa nchi iliyopo kusini mwa Amerika akaamua kulifanyia kazi hili kwanza. asubuhi moja isiyokuwa na jina mwezi uliopita akaamka na bila kuuma uma maneno akatamka kwa kujiamini kabisa kuwa kuanzia siku ile visima vyote vya mafuta vitakuwa chini ya usimamizi wa serikali, nani anabisha.

Kama ilivyotegemewa, wakubwa wa dunia ambao ndio makampuni yao yalikuwa yamejazana huko yakichimba mafuta wkaja juu. wakakemea, wakafoka, wakatisha, wakanuna, wakachimba mkwara na kadhalika na kadhalika lakini wapi. mheshimiwa akashika uzi ule ule huku akiwaambia jamaa hapa hakieleweki mpaka kieleweke.

Halafu akatamka maneno ambayo yalimkuna mno muandika katikati ya mistari na kumfanya kuanzia wakati huo atamani sana kuyasikia yakitamkwa na watu fulani mahali fulani kwamba:

'kwa muda mrefu mapato ya rasilimali zetu yamekuwa yakiwanufaisha wajanja wachache badala ya wananchi wenye nchi yao lakini kuanzia wakati huo alikuwa ameamua kusimama kidete ili kuhakikisha kuwa wananchi wake wanafaidika na rasilimali waliyoachiwa na Mungu!'

Naam, maneno mazito kabisa haya ambayo haraka haraka yakaungwa mkono na huyu mheshimiwa mwingine kiongozi wa nchi jirani na huyu mheshimiwa wa kwanza na ambaye ana usongo mno na huyu raisi wa dunia, mheshimiwa Joji Bushi, kiasi kwamba aliisha wahi kusimama kadamnasini na kumuambia Joji lione kwanza, wee si mlevi tuu!

Naam, haya ni maneno ambayo kwa namna moja ama nyingine yalikuwa pia yameishatamkwa na waheshimiwa ambao ndio kwanzaa walikuwa wametwaa uongozi wa nchi njema iliyoko mashariki kabisa mwa Afrika mashariki.

Tofauti ilikuwa ni kwamba mheshimiwa wa nchi iliyo Amerika ya kusini alikuwa amekwenda hatua moja mbele kwa kuyaambatanisha maneno yake na vitendo ambavyo bila shaka aliamini kuwa vitwasaidia wananchi wake huku hawa waheshimiwa wa nchi iliyo mashariki ya Afrika mashariki wakiwa bado kwenye hatua za mazungumzo tu na wanaochimba nchi yao.

Naam, mazungumzo ya kuangalia uwezekano wa mkakati wa kuwezesha nchi ipate zaidi ya Marahaba tatu ipatazo sasa kutoka kwa wachimbaji wa rasilimali zetu ambao wao hupata Marahaba Tisaini na saba kutoka katika kila Shikamoo mia moja zinazochimbuliwa kutoka kwenye ardhi yetu. mwenye masikio na asikie.

halafu kama vile hili sio wazimu tosha, majuzi tumesoma taarifa kuwa hata katika hizo Marahaba tatu tunazopata, kuna kijikampuni fulani cha wenyewe ambacho kinachukua nusu ya Marahaba tatu tunazogaiwa na wakubwa, yaani Marahaba moja na nusu, kwa ajili ya eti sijui kuoditi, ile nusu nyingine ya Marahaba iliyobaki! hili ni jambo linaloweza kutokea Bongo tu.

Inapofika hapa, muandika katikati ya mistari anajikuta akimkumbuka mno yule mzee wetu wa Zimbabwe ambaye naye aliamka tu asubuhi moja na kuamua kuwa kuanzia asubuhi ile mashamba yote yenye rutuba yaliyokuwa yamehodhiwa na wachache sasa yatakuwa chini ya usimamizi wa serikali.

Yamesemwa mengi. ya kumuunga mkono na ya kumponda mzee wa watu. lakini mpaka majuzi mzee alikuwa ameshikilia uzi ule ule ingawaje alikuwa tayari ameishaulegeza kidogo wa kuwataka wanaotaka kurudi kwenye mashamba yao wafanye hivyo ingawaje kwa sasa ni kwa taratibu mpya zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Mwandika katikati ya mistari hapa hatataka kuzungumza kuhusu yule mheshimiwa Dada wa nchi ya jirani ambaye naye siku moja aliamka asubuhi na kuamua kuwa ili wananchi wake wapate faraja basi wahindi wote, out! huyu tumuache maana, amin amin nawaambia, alikwisha kupata thawabu yake.

Mwandika katikati ya mistari anadhani kwamba ni lazima na sisi tufike mahali asubuhi moja tuamke na na kuamua kuwa kuanzia asubuhi hiyo mashimo yoote yanayochimbwa rasilimali zetu sasa yapo chini ya usimamizi wa serikali hadi tutakapopanga taratibu nyingine, full stop.

Na kwa hili hatuna haja ya kumuigiza mtu maana tayari tuna ozoefu nalo. ndio, asubuhi moja ya mwaka 1967 mheshimiwa mmoja ambaye sasa ni marehemu aliamka na bila kujiuma uma wala kutafuta suluhu na mtu alitamka wazi kabisa kuwa kuanzia siku ile mabenki na majumba yoote makubwa yangekuwa sasa chini ya usimamizi wa serikali, nani anabisha.

Hakuna aliyethubutu kubisha. ndio maana muandika katikati ya mistari anadhani wakati umefika sasa wa kujiuluza kama walivyojiuliza wadogo zake fulani....kwani wao wanaweza wana nini hadi sisi tushindwe tuna nini? alamsik.

Monday, May 15, 2006

chesimpilipili

kweli haya mambo bado ni mageni kwa tulio wengi. hapa nilitaka kuwawekea picha moja kuonyesha jinsi ninavyoachia mdomo wakati ninapotafuta cha kuandika. katika kuminya huku na kule, nikashitukia zimetoka mbili tena sio pale nilipotaka zitokee. maana mimi nilitaka itoke moja tu ndogo hapo kwenye 'about me'. matokeo yae ndio haya. kweli, ndesyanjo bado ana kazi.......!!

Friday, May 05, 2006

chesimpilipili

Wakati kheshimiwa mpya wa Bongo alipotimiza siku mia moja ofisini, kila mtu aliandika makala. mimi niliamua kungoja hadi siku kumi baadaya ndio nikaandika hii niliyoiita...

Siku 110 ofisini...!



Alhamisi ileee, kama siku hivi kumi zilizopita, wakati hii awamu ya nne ya uongozi wa nchi njema ya Bongo inatimiza siku mia moja, tulishuhudia jinsi kila aliyekuwa anajua kuandika alivyochongoa kalamu yake na kuchonga.

Napenda kuamini kuwa maneno haya ni ya kistaarabu zaidi kuliko kama ningesema kuwa kila mwenye mdomo aliuchongoa na kuchonga.

Naam, siku ile ya Alhamisi wakati awamu ya nne ya uongozi inatimiza siku mia moja ofisini kila mwenye kalamu yake aliishika na kuandika kile alichoamini kuwa ni bonge ya makala.

Zilikuwa makala za kusisimua mno kiasi kwamba ungedhani watu wanasherehekea kutimiza miaka mia moja ya uongozi na kumbe ni SIKU mia moja tu!

Mwandika katikati ya mistari hataki kuamini kwamba siku mia moja zinatosha katika kukupa muelekeo wa jambo fulani.

Pengine ndio maana akaamua kuacha kitim tim cha kuandika kuhusu siku mia moja kitulie kwanza ndipo na yeye atie neno lake. maana wote tungeandika wakati ule sijui nani angemsoma mwenziwe.

Kikubwa alichogundua mwandika katikati ya mistari katika kitim tim kile ni kuwa nchi njema ya Bongo haina uhaba wa wafagiliaji na eeee, kidedea.

Wapo wa kumwaga. kulikuwa na makala nyingi zaidi za kufagilia kuliko zilizokuwa na alama za kuuliza.

Si nia ya muandika katikati ya mistari kuingilia uhuru wa mtu kutoa maoni yake. na ndio maana hata yeye hategemei mtu kuanza kumuona kuwa si mwenzetu kwa vile tu makala yake itakuwa imejaa maswali mengi zaidi kuliko mafagio. ndio, wenzake weengi wameishafagilia. yeye anaomba kuzungumzia zaidi upande wa pili wa gwala.

Haya, siku mia na kumi. kikubwa alichoona huyu last born wa marehemu mzee Mpilipili katika kipindi hiki cha siku mia moja na kumi ni maagizo, maelekezo na maonyo meengi ambayo wakati fulani yalianza kumfanya aone kama tulikuwa tumerudi tulikotoka. maagizo na maelekezo kibao yaliyokuwa na muelekeo wa kuishia kuwa hivyo hivyo, maagizo na maelekezo tu.

Anadhani kwamba waheshimiwa wa awamu ya nne walikuwa wanaenda kasi mno kiasi cha kutuacha sisi wengine wote nyuma. waama, Chesi anadhani kwamba sio vibaya iwapo waheshimiwa hawa wakasimama kidogo kutusubiri na pia kufuatilia kama yale maagizo na maelekezo yote wanayotoa huku nyuma yanatekelezwa.

Kuna hili la sirikali kuanza na migulu baja kwenye suala kubwa la kubana matumizi yake. tumeshuhudia tumizi kubwa la waheshimiwa walioteuliwa kuja Dizim na kuishi kwenye hoteli za bei mbaya wakisubiri nyumba, ushahidi kamili kwamba uamuzi wa kuuza nyumba za taifa kwa watu wawili watatu ni mchemsho wa karne, ingawaje nafasi bado ipo ya kulirekebisha hili kwa kurudisha nyumba zile kwa wananchi na kuwarudishia chao waliozinunua.

Basi waheshimiwa wenyewe waje peke yao, aa wapi. wengine walikuja na wake zao, na watoto wao na labda hata vijukuu na hivyo badala ya mheshimiwa kuchukua chumba kimoja tu katika hoteli ya bei mbaya, anachukua vitatu. cha kwake na mamaaa, cha watoto na sebule, maana wageni anaomtembelea mhishimiwa hawawezi wakaingia chumbani kwake moja kwa moja wasije wakaona deshi deshi zake zimeanikwa kwenye tendegu la kitanda!

Naam, hii ni tofauti iliyoje na pale huyu Chesi alipohamishiwa Darisalama mara ya kwanza miaka hiyoo ya 47 ambapo ili kubana matumizi alilazimika kutangulia yeye na bi mkubwa kwanza na kuishi kwenye kijigesti fulani cha uchochoroni hadi pale alipopata makazi ndipo aliporusu umati wake wote kutia timu jijini!

Muandika katikati ya mistari anatamani mno kuwa badala ya kugharamiwa na sirikali, kila mmoja katika waheshimiwa hawa angekatiwa kabisa posho yake ya safari na manaiti yake kama anavyofanyiwa yeye anapobahatisha kwenda safari, kisha tuone. thubutu kama mtu angekaa kwenye hoteli ya bei mbaya na kadamnasi yake!

Haya, katika siku mia moja na kumi tumemsikia pia mheshimiwa wetu akitamka bayana kuwa ana majina ya wala rushwa wote lakini anawapa muda kwanza ili kujirekebisha. hii ni kauli iliyomkumbusha sana mwandika katikati ya mstari juu ya kauli fulani ya hapo zamani za kale juu ya kwamba wala rushwa wote wangekiona cha mtema kuni lakini baadaye ikabadilika na kuwa ya kutaka ushahidi kwanza kabla ya cha mtema kuni!

Hawa watu wameishaitafuna sana kama mchwa nchi yetu njema hii ya Bongo. kuwapa tena muda wamalizie malizie kuitafuna haimuingii akilini muandika katikati ya mistari. hawa kwa hakika ni watu waliostahili kufanyiziwa kwa kasi ile ile iliyotumika kuwatoa mkuku wagonga kokoto kule kwenye machimbo yao ama wenye vibanda vyao katikati ya jiji. staili ya hakuna cha mswalie mtume!

Ndio, ili kuepusha kuonekana ni ' yale yale', kasi mpya inapaswa kuwa ni upanga wenye makali ya kukata kote kote badala ya kuwa na ukali wa ajabu pale tu inapokuwa ni suala la kuvunja vibanda vya Big Brother Manzese, lakini inapokuwa ni suala la kukata manyangumi na mapapa wala rushwa ghafla unakuwa butu na kuanza kusua sua!

Katika siku mia moja na kumi hizi pia tukaambiwa kukaa standby kusikiliza orodha ya majina ya wale walioaminika kuwa ni majambazi makubwa. muandika katikati ya mistari na walala hoi wenzake wakakaa mkao wa kula wakisubiri mijina mikubwa mikubwa ya mijambazi iliyokuwa inaivuruga Bongo yetu njema hii.

Jiji jema la Dizim likatangaza kile kilichosemekana kwamba ni majina ya mijambazi mikubwa mikubwa na muandika katikati ya mistari akajikuta akishindwa kuzua muayo wake. hakuna jina lolote lililoshitua mtu na kwa hakika muandika katikati ya mistari hatashangaa sana iwapo miongoni mwa orodha ile kutakuwa na wauza karanga wawili watatu. Hivi watu wanajua maana ya majambazi wakubwa kweli?

Ni kweli, yalikuwepo majina mawili matatu yaliyoshitua watu kiasi fulani lakini watajwa walipofikishwa mahakamani wakiwa wametinga magold na masuti yao huku wakitabasamu muandika katikati ya mistari akakata tamaa na kuona kama ni aina fulani ya mchezo wa kuigiza hasa pale anapokumbuka kuwa wadogo zake wanapofikishwa 'kaunta' (kama unadhani ni ya Bar, pole!) huamrishwa kuvua kila kinachoweza kuvuliwa, na kama huna bahati hata nywele!

Hapo hapo kwenye orodha ya majina tukaambiwa kuwa tungetajiwa pia orodha ya majina ya askari wa vyeo vya juu ambao walikuwa wakishirikiana na majambazi. tukasubiri, tukasubiri, tukasubiri wee. wakatajwa wawili watatu wenye vyeo ambavyo sio kitu cha kuandikia barua nyumbani kisha, kimya.
habari iliyokuwa ukurasa wa mbele sasa imeishia kuwa ya ukurasa wa matangazo...!

Ni mambo kama haya ambayo yanamfanya muandika katikati ya mistari aombe kwanza kuweka fagio lake mfukoni. ni mpaka hapo atakapoona mtu mzima ananyolewa nywele kwa kigae cha chupa ndipo labda, laabda atalitoa na kufagilia mtu. Asalaam aleikum.
chesimpilipili

hii niliiandika wakati nchi yetu njema ya Bongo inatimiza miaka 41 tangia tupate uhuru......


tuwaite, waje kuona ... ?

Mwandika hekaya alikuwa dogo wa miaka kumi na mbili tu na akisoma darasa la nne hapo katika shule ya msingi ya Chang'ombe wakati nchi njema hii ya bongo ikisherehekea miaka kumi ya uhuru wake pale mwaka na 1971.

Anakumbuka mno jinsi yeye binafsi alivyoshiriki kikamilifu katika sherehe hizo kwa kuwa miongoni mwa mamia ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za jiji jema la Dizim walioshiriki katika maonyesho kabambe ya halaiki yaliyofanyika pale uwanja wa taifa.

Naam, maonyesho ya halaiki ambayo mpaka leo hii wachokozi wa mambo bado wanakubaliana kwamba hayajapata kutokea tena mfano wake, pengine kutokana na ukweli kwamba ilifundishwa na waalimu wa kichina orijino kutoka china!

Haya, mwandika hekaya pia anakumbuka mno nyimbo kadhaa za muziki wa dansi zilizotungwa na wasanii wetu kwa ajili ya kipindi cha sherehe hizo.

Anakumbuka mno ule wa bendi marehemu ya Urafiki jazz, wakati huo ikiongozwa na mzee Mrisho, Ngulimba wa Ngulimba, wimbo ambao pamoja na mambo mengine, ulielezea mafanikio yaliyokuwa yamepatikana katika kipindi hicho cha miaka kumi ya uhuru.

Ikatajwa reli ya Tazara, chuo chetu kikuu, vyama vyetu vya ushirika, jeshi letu la mgambo( wakati huo likiwa jeshi la mgambo kweli na sio haya masulupwete tunayoshuhudia siku hizi!) na hata kisomo cha watu wazima kikatajwa kama moja ya mafanikio yetu!

Haya, mwandika hekaya pia akakumbuka mwimbo mwingine uliokuwa umeimbwa na hayati Mbaraka Mwishehe Mwaruka ambao ulielezea jinsi wakoloni walivyokuwa wametuchelewesha na hatua ambayo tulikuwa tumeifikia baada ya wao kung'atuka.

Lakini, zaidi mno muandishi wa hekaya anakumbuka mno wimbo ulioimbwa na Nuta jazz, kama hajakosea sana, ambao maneno yake anayakumbuka vizuri mpaka leo hii:

'sasa tutawaita waje kuona wenyewe,

hatutafanya kitu tukashindwa,

sasa tutawaita waje kuona wenyewe,

maendeleo yetu yanakwenda vyema....'



Naam, mwandika hekaya hana uhakika sawa sawa, lakini anadhani kwamba maneno ya wimbo huu yalikuwa yametokana na hotuba moja ya raisi wa nchi wa wakati huo, mwalimu Julius Nyerere, ambapo alikuwa amesema kwamba tungewaita wale waliotutawala waje kuona tulipokuwa tumefika katika kipindi cha miaka kumi.

Na kwa hakika wakati huo tulikuwa kweli na jeuri ya kuweza kuwaita waliotutawala na kudai kwamba tulikuwa bado kustahili uhuru, waje kuona mambo makubwa tuliyokuwa tumefanya katika kipindi hicho cha miaka kumi. ndio, tulikuwa na jeuri hio!

Ukiachilia mbali mambo makubwa kama yale ya ujenzi wa chuo kikuu, viwanda kama kile cha nguo cha Urafiki,na Mwatex na cha zana za kilimo cha Ufi na kadhalika na kadhalika, nchi hii ilikuwa imepiga hatua kubwa mno katika huduma za jamii.

Huyu muandishi wa hekaya anakumbuka mno kwamba katika kipindi hicho alikuwa akiishi na shemeji yake mmoja pale Chang'ombe mtaa wa Ngorogoro nyumba namba 98, na anakumbuka mno pia kwamba hakupata kushuhudia kitu kinachoitwa kukatika umeme ama maji kukatika kwa siku tatu nzima, never!

Kila mara muandika hekaya anapowahadithia haya wanawe, huishia kuona huruma jinsi wanawe wanavyobaki kung'aa macho kutoana na mshangao kwa vile wao katika kipindi hiki cha mgawo, umeme huja saa tano usiku na 'kuondoka'
saa kumi na mbili alfajiri!

Anakumbuka pia mno jinsi mitaa ya Magomeni, Ilala na kwingineko ilivyokuwa misafi ikiwa na lami, mbali na kila nyumba kuwa na pipa lake la takataka ambalo lilikuwa likija kuchukuliwa takataka zake na gari la site kila baada ya siku mbili!

Siku hizi ukiweka pipa la taka nje kesho hulikuti maana unakuwa umewapa watu kifaa cha kuhifadhia maji kutokana na maji kuwa ya mgawo!

Na hapa chesi anaogopa hata kudokeza kwamba yeye alisoma darasa la pili hadi la sita katika shule hio ya msingi ya Chang'ombe akiwa amekalia dawati lake la mtu mmoja mmoja tu, sio watatu, kwa kuchelea kwamba watu hawatamuamini, kwa vile hata watoto ake tu wanadhani anayowaambia ni fiksi zake tu!

Ni wazi basi kwamba baada ya wabongo walio wengi kushuhudia mafanikio haya ya miaka kumi, walitegemea kwamba hadi nchi hii itakapofikia miaka thelathini ama arobaini ya uhuru, ingekuwa pungufu kidogo tu ya peponi! ole wao. ole wetu.

Muandika hekaya angependa kuwahoji wabongo wenzake. ni kweli kwamba katika kipindi hiki wakati nchi njema ya bongo inasherehekea kutimiza miaka arobaini na moja ya uhuru wake, tunayo jeuri ya kuwaita waliotutawala waje kuona mafanikio yetu, kama alivyofanya baba wa Taifa wakati wa kusherehekea miaka kumi ya uhuru wetu mwaka na 1971??

Tuwaite? waje kuona nini? barabara za katikati ya jiji walizoziacha na lami na ambazo sasa baada ya miaka 40 ya Uhuru ni vumbi tupu, hata zile za kwao akina chesi kule Bumbuli zina nafuu?

Waje kuona nini? bomba kuu kukuu la kuleta maji jijini ambalo toka waondoke wao hakuna mtu ambaye ameishapata angalau kuwaza kutafuta vyanzo vingine vya maji badala ya waheshimiwa kila mara kujazana mahali bomba linapopasuka na kuahidi wananchi kwamba maji yatatoka baada ya siku mbili tatu!!

Tuwaite waje kuona nini? hospitali zisizokuwa na dawa? shule zisizokuwa na madawati? nyumba za watumishi wa serikali walizoziacha ambazo sasa kwa kisingizio cha sirikali kushindwa kuzimeintein, sasa zinapigwa bei kama nguo za mitumbani?

Mwandika hekaya anaweza kuandika mengi lakini lililo wazi ni kwamba, pamoja na kwamba kuna watu watabisha, yeye haoni kama tunao ubavu wa kuwaita walee waliotuwala ili waje kuona maendeleo yetu baada ya miaka AROBAINI NA MOJA ya uhuru wetu! alamsik.

Thursday, April 27, 2006

chesimpilipili

kuna hii ambayo inawahusu hawa waheshimiwa wanaotutunzia vi-akiba vyetu vya uzeeni......




Kwa hesabu za haraka haraka, huyu mwanaGlobu mpya atatimiza birthday yake ya sitini mnamo mwaka 2019, miaka michache sana kumi na mbili tu ijayo.

Huo ndio mwaka ambao hawa watu wanaomtunzia vijisenti vyake vya uzeeni wamemuambia kwamba ndio ataweza kuchukua kilicho chake, kwa maana ya hatimaye kulia kivulini baada ya miaka kibao ya kuchumia juani.

Kwa jinsi kazi ya kuuza kila kilicho chetu ilivyoshika kasi na hao wanaovinunua wanavyotustaafisha kushoto, kulia na katikati kama vile hawana akili nzuri, Chesi ana uhakika kwamba kufikia mwaka huo wa 2019 yeye atakuwa aliishastaafishwa kazi miaka miaka kumi na nne kabla, yaani mwaka 2008.

Atakuwa ameachishwa kazi mwaka huo wa 2008 akiwa dogo wa miaka 49 tu, lakini kutokana na hii sheria ambayo kwa hakika inaweza kupitishwa nchi kama ya bongo tu, atakuwa amezuiwa kuchukua chake ati mpaka afikishe miaka sitini, yaani huoo mwaka wa 2019! mungu wangu!

Ndio, kwa hakika hii ni sheria ambayo inaweza ikapitishwa nchi kama ya bongo tu! yaani mtu ufanye kazi miaka thelathini, ustaafishwe ukiwa na miaka hamsini halafu mtu akuambie huwezi kuchukua akiba yako mpaka utakapofikisha miaka sitini!

MwanaGlobu anajiuliza kama sheria hii ingepitishwa iwapo hawa walioipitisha nao wangeambiwa hawawezi kuvuta kiinua mgongo chao cha milioni thelathini na kitu,(baada ya 'kufanya kazi' kwa miaka mitano tu) hadi pale na wao watakapofikisha miaka 60, hapana,80, kutokana na ukweli kwamba wengi wao tayari wako kwenye anga za miaka 60!!!

Thubutu kama sheria hii ingeona jua la nje!

Haya, kwa rehema za Mungu huyu mwanaGlobu anafanikiwa kufikisha miaka yake sitini. bila shaka atakuwa amejichimbia huko kwao Bumbuli, kutokana na ukweli kwamba baada ya kustaafishwa kazi, hakuwa na jeuri yoyote ya kuendelea kubanana hapa hapa mjini kama wenzake!

Atafikisha miaka yake sitini na atajikongoja kutoka huko kwao na kuliingia jiji la Dizim la mwaka 2019. labda wakati huo stend ya mabasi itakuwa Kibaha. Pengine pale mtaa wa Samora jengo fupi kuliko yote litakuwa la tughorofa thelathini. mengine yote yatakuwa mawinguni.

Anaweza pia akakuta hata ile sanamu ya askari pale imebinafsishwa na mwekezaji kuamua kuivunja na kuweka kijifast food cha nguvu katikati ya ule mzunguko! hakuna kisichowezekana Bongo.

Na ni kutokana na wingi wa majengo mareeeefu, ndio maana pengine Chesi atapata tabu sana kulipata jengo ambalo lilikuwa ndio makao makuu ya shirika ambalo lilikuwa linamtunzia visenti vyake hadi atakapofikisha miaka 60.

Ni hatimaye sana, na baada ya kuzunguka mno ndipo pengine Chesi atabahatisha kuliona jengo hilo nje kabisa ya mji likiwa na tugorofa thelathini tu! bila shaka nje ya mji wakati huo itakuwa kibaha maili moja!

Ataingia mapokezi na kumkuta huyu binti ambaye bila shaka bibi yake mzaa mama alifanya kazi na chesi miaka hio, sio ofisi moja bali kwa rika.

Na kwa vile pengine enzi hizo watu watakuwa bize sana zaidi ya ilivyo sasa, binti yule hatapoteza muda kumuamkia kizee Chesi na moja kwa moja: "sema shida yako, wee mzee!"

Chesi ataeleza shida yake, kwamba amekuja kuchukua masimbi yake kwa vile amefikisha miaka sitini. binti atamuelekeza chesi kwa ofisi husika. atamuelekeza, huku macho yake 'yakiuliza' wazi kabisa inakuwaje mpaka siku ile chesi awe bado anapeta tu wakati vizee vyenzake vimeishauona ufalme wa mbingu kitambo!

Haya, chesi anapanda gorofa ya kumi na saba kwa muhusika ambaye anamuelekeza gorofa ya tatu kwa muhusika ambaye anamuelekeza gorofa ya saba kwa nuhusika ambaye anamuelekeza gorofa ya kumi na nane kwa muhusika mwingine na mwingine tena. mpaka hapa, mambo kwa Babu Chesi ni kizunguzungu kitupu!

Hatimaaaye, anampata huyu muhusika ambaye anamfahamisha Babu Chesi kwamba Ofisi yake haina kumbukumbu zozote zinazohusu kampuni aliyokuwa akidundia mzigo chesi, hivyo... chesi alie tu....! na labda miaka hio msemo utakuwa....chesi acheke tu!

Na kweli, chesi anatamani kulia na kucheka kwa pamoja. Yaani baada ya kusubiri kwa miaka kumi na tatu mizima baada ya kustaafu, leo hii anaambiwa hana chake!kwa hakika ni jambo la kushukuru kwamba haanguki na kufaint na kufariki pale pale kutokana na mshituko!

Huyu mhusika wa mwisho angalau anaonyesha kutaka kumsaidia chesi kadri ya uwezo wake,hususani baada ya kutamka kwamba "alaa! kumbe wewe ndio mzee chesi mpilipili! mama huwa ananihadithia kwamba alipokuwa kijana alikuwa akipenda sana kusoma makala za mwindishi mmoja aliyekuwa akiitwa chesi mpilipili! kumbe ndio weewee!"

Kijana yule anamsaidia chesi kwa kupanda gorofa hili na kushukia lile, kuingia ofisi hii na kutokea ile na kufungua disketi hii na CD ile, lakini waaapi. mwisho wa yote hakuna rekodi yoyote inayopatikana kuonyesha kwamba chesi anapaswa kulipwa masimbi yake wakati atakapofikisha miaka sitini!

"unajua, mzee chesi, hapa katikati tumehama hama sana kiasi kwamba bila shaka baadhi ya nyaraka zetu zitakuwa zimemisiplesiwa na tarakilishi zetu zimekrashi !"

"eniwei, wee njoo tena baada ya miezi sita na nitaangalia ni vipi!ninaweza kukusaidia! napenda kukufahamisha pia kwamba mama atafurahi sana leo nikimfahamisha kwamba nimekutana na mzee chesi!" kijana anatoa tamati na mchezo unaishia hapo.

chesi anaondoka jijini kipara na kurudi kijijini Bumbuli akiwa amezeeka ghafla na kuonekana ni kizee wa miaka 85 badala ya 60 aliyonayo. anazeeka zaidi anapokumbuka kwamba kijijini aliondoka kwa mkwara mzito kwamba atakaporudi kutoka mjini, watu watajua yeye ni nani!

Naam, ni kwa mlolongo huu wa mawazo ndio maana chesi anadhani kwamba anapostaafishwa ni afadhali akamilishiwe chake kabisa aangaze mbele, na kama kuna kasoro katika rekodi zake, aweze kuzishughulikia akiwa bado na nguvu zake.

Ndio, hii 'bahati nasibu' ya kusubiri hadi afikishe miaka sitini, potelea mbali kwamba ni hapo kwenye kona tu, ndipo aambiwe ahana chake yeye haafikiani nayo.

vinginevyo, hata wale walioipitisha sheria hii ya ajabu nao wanapomaliza miaka yao mitano ya kudunda mzigo, waambiwe kiinua mgongo cha cha milionizao 30 watalipwa pale watakapofikisha miaka 80, kwa mantiki ile ile kwamba wengi wao tayari wapo kwenye anga za miaka 60, tuone kama watakubali! nawakilisha.

Tuesday, April 25, 2006

chesimpilipili

Kuna hii ya majina yetu kwanza....


Wiki kama mbili tatu hivi nyuma, huyu mwandika katikati ya mistari alipata bahati ya kuhudhuria kijikongamano fulani hivi kuhusu mawasiliano kilichofanyika kwenye kijihoteli flani cha kitalii (wapi kwingine!) cha bei mbaya katikati ya jiji jema hili la Mzee Makamba la Dizim.

Mwandika katikati ya mistari bado anaamini kwamba kuteuliwa kwake na wahusika kuhudhuria kijisemina hicho kulitokana na ukweli kwamba kijiposho kilichokuwa kinatolewa kwenye kijikongamano hichi kilikuwa ni kijiposho mbuzi. kingekuwa beberu mwandika katikati ya mistari angeisikilizia kwenye bomba!

Ndio, unategemea nini kwa nchi ambayo kwenye kongamano la wasioona nje ya nchi inawakilishwa na wanaoona wengi kuliko wasioona.

Mwasikia sana? kabla ya kijikongamano hicho kuanza rasmi, washiriki tukatakiwa kuandika majina yetu, ya kwanza, ili yakatengenezewe beji ambazo tungetakiwa kuzivaa katika kipindi choote cha kijikongamano hicho kwa kile tulichoambiwa kuwa ni kurahisisha mawasiliano kati ya washiriki na watoa mada wazungu.

Basi bwana, huyu muandika hekaya akaandikisha jina lake la Mpilipili akiamini kwamba lilikuwa linajulikana zaidi kuliko lile la Chizi, mbali ya ile mantiki pana zaidi kwamba sisi wabantu tuna kawaida ya kujuana kwa majina ya ukoo zaidi kuliko yake 'kuazima' kutoka kwa wazungu na waarabu!

Akaja huyu mweupe mmoja mtayarishaji wa kijikongamano hicho na kuwasisitizia washiriki wote, lakini akielekea kumlenga zaidi muandika katikati ya mistari, kwamba tulitakiwa kuandika majina yetu ya kwanza, yaani yale ya kizungu na kiarabu, kwa vile haya yetu ya kibantu yalikuwa magumu na yangeweza kuzitoa jasho ndimi za weupe waliotarajiwa kutoa mada kwenye kijikongamano hicho!

Yaani, kwa maana ya kwamba washiriki walitakiwa kuandika majina yao 'mazuri' ya Noel, Gilbert, Priscah, Peter, Evelyn, David, Roy, Desmond na mengineyo ya dizaini hiyo kwa kile tulichoelezwa kuwa ingesaidia sana katika kuokoa muda ambao ungepotea wakati ndimi za watoa mada weupe zikijikanyaga kanyaga katika kutamka majina yetu ya kibantu!

Ndio, kwamba ati majina ya Mpambalyoto, Rugarabamu, Mwakambaya, Khasimbago Khaabuka, Ambakyise, Masayanyika, Mamtogolo, Shekuavu, Shengoto, Mambazi, Mamkai na kadhalika na kadhalika, yalikuwa na muelekeo wa kusababisha ndimi za weupe wa watu kurudi kwao zikiwa mahututi kama sio kuvishwa POP kabisa!

Kwa vile akili za muandika katikati ya mistari huwa ziko mbele kwa madakika kadhaa, papo hapo akatoa hoja kwamba yeye angefurahi zaidi kuandikwa Mpilipili kwenye beji yake badala ya chesi, pamoja na kwamba hata hio chesi yenyewe ni jina la kiswahili tofauti kabisa na baadhi ya watu wanavyodhani kwamba limetoholewa kutoka jina la kiingereza la Chase ama Charles!

Mwandika katikati ya mistari akatoa hoja pia kwamba kwa vile weupe hao walikuwa wamekuja kwetu, basi wao ndio walipaswa kuzipa mazoezi ndimi zao ili kuhakikisha kwamba zinaweza kula sahani moja na majina yetu na sio sisi kuwarahisishia kazi kwa hasara ya kuukana ubantu wetu!

Ndio, kama weupe wale walikuwa wanataka sana sisi tuachane na majina yetu ya kibantu, basi ilikuwa ni kiasi cha wao kutusubiri tu tukienda kwenye balozi zao kuomba viza na kutufanyizia, badala ya kuja hapa na kutaka tujikane kwa ajili tu ya kijiwarsha cha siku mbili tatu@

Naam, weupe hao wangejuaje kwamba waliishawahi kufika Afrika na Bongo, bila kwanza ndimi zao kupata 'frakcha' na kuwekewa POP wakati wakijaribu kutamka jina la Masalakulangwa, kama sio lile la Mwakamsondole!

Angalia basi kilichotokea na kumuacha hoi bin twaabani mwandika hekaya. mweupe yule wala hakuwa hata na haja ya kubishana na chesi. kazi hio waliifanya vizuri kabisa wabantu wenzake chesi waliong'ang'ania kwamba kulikuwa na umuhimu wa kutumia majina yetu ya kizungu ili kumrahisishia mweupe mmoja tu kazi yake!

Kwamba eti hata kama tungeamua kutumia majina yetu ya kibantu, mengi yao yalikuwa ni marefu mno kiasi kwamba yasingeenea kwenye beji tulizokuwa tunatayarishiwa! Wakafikia hata hatua ya kumtaka kikejeli muandika katikati ya mistari ajaribu kuandika kwenye kibeji chake jina la kibantu la Mzanzugwamko ama Jigulamajambazi!

Mwandika katikati ya mistari akajikuta akijuta mno kwa nini marehemu baba yake hakuwa na jina reeefu kama lile la mfalme Shokolokobangoshei wa enzi zilee Bulicheka na mkewe walipokwenda Mombasa kuiona nchi. kwa hakika angeuvaa mbeji wake ulioandikwa jina hilo kwa fahari kuu, potelea mbali kwamba ungekuwa umeenea kifua kizima, kwapa hadi kwapa!

Tukafikia hapo. washiriki wabantu wa kajikongamano kale wakaona ni mali sana kutumia majina yetu ya kizungu na kiarabu badala ya yale ya ukoo tunayoyatumia huko maofisini, kwa vile tu ulimi wa mweupe mmoja mtoa mada ulikuwa hautaki tabu.

Mwandika katikati ya mistari anashukuru kwamba yeye aling'ang'ania, na hatimaye kukubaliwa, potelea mbali kwamba ni kwa shingo upande, beji yake kuandikwa Mpilipili kwa kipindi chote cha kijikongamano hicho ambacho mtu angesomewa majina ya washiriki angedhani kwamba kilikuwa cha weupe watupu... Mary, Dennis, Robert, Albert, Michael, Susan, Stephen, Irene na mbantu mmoja tu, Mpilipili! (makofi, tafadhali!)

Naam, bila shaka mweupe yule alirudi kwao akiwaza kuwa dah, hajawahi kuona jitu bishi na king'ang'anizi kama yule Mpilipili wa kule Bongo. lakini kuna uwezekano pia kwamba pengine moyoni mwake aliwaza kuwa pamoja na yote, angalau bado kuna mijitu Afrika inaweza kuusimamia na kuutetea Ubantu wao. sijui ingekuwa nyinyi wasomaji wangu wapenzi mngefanyaje
chesimpilipili

Wakuu, naomba mniruhusu niweke baadhi ya makala zangu hapa wakati Ndesanjo akiendelea kunipa somo juu ya kuhifadhi makala ndeeefu...

Thursday, April 20, 2006

chesimpilipili

Ndesanjo, nadhani somo lako kuhusu kublogu limeingia barabara. nakushukuru sana. sasa na tuanze kazi.....

Thursday, April 13, 2006

Napenda kuamini kuwa kwa wasomaji wa magazeti wengi walioko bongo jina la Chesi Mpilipili sio geni kwao kwa maana ya kwamba watakuwa wameishasoma makala zangu kadhaa za kiswahili na kiingereza kupitia magazeti mbali mbali yanayochapishwa bongo.

naamini kuwa huu utakuwa ni uwanja mpana zaidi wa kuwasiliana nao, wasomaji na waandishi wengine sehemu mbali mbali za ulimwengu huu. naomba kupiga (ama ni kubisha?) hodi.

Monday, April 03, 2006

salamu, bloggerz. mimi ni mpya hapa na ndio kwanza nafungua blogg yangu. maelezo mengine yanafuata.